Mawakili wa SNOLEGAL waambia Omanyala baibai siku tatu baada ya DBA Afrika kukatiza uhusiano naye

Mawakili wa SNOLEGAL waambia Omanyala baibai siku tatu baada ya DBA Afrika kukatiza uhusiano naye

Na GEOFFREY ANENE

Mawakili wa nyota Ferdinand Omanyala, SNOLEGAL wametangaza kutengana na mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika ya mbio za mita 100 mnamo Septemba 29.

Kampuni hiyo, ambayo imeorodhesha dereva jagina Azar Anwar, klabu ya Kariobangi Sharks na Nairobi City Stars zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) kama baadhi ya wateja wake, imesema kuwa ilihisi ni muhimu kuweka wazi mchango wake kwa mtimkaji Ferdinand Omanyala Omurwa.

“Kampuni ya sheria ya SNOLEGAL inayojihusisha na masuala ya michezo na burudani ilimpa Omanyala huduma za ushauri wa kisheria, udhibiti wa sifa, ulinzi wa haki zake za ubunifu, uhusiano wema na mawasiliano hadi Septemba 7, 2021 wakati tuliamua kwa kauli moja kuacha kumwakilisha na hatujahusika katika uamuzi anaofanya tangu wakati huo,” kampuni hiyo ilitanguliza.

“Tunapongeza timu yetu kwa kazi imefanyia Ferdinand ambayo inaendelea kuzaa matunda.

“Tunajivunia hasa juhudi zetu za kurekebisha hadithi za uongo ama za kuchafua jina la Ferdinand kupitia vyombo vya habari kuhusu mambo ya zamani yaliyopita ya uvunjaji wa sheria zinazopiga marufuku matumizi ya dawa za kusisimua misuli, katika kumpigania kuhakikisha anajumuishwa katika timu ya Olimpiki, kuanzisha njia za mawasiliano na uhusiano mwema, kuingilia kati na kujadiliana masuala ya nafasi ya kupata udhamini unaofaa, kwa kupeana mawazo ili kutafuta njia mpya za kufanyia kazi, kuanzisha na kumuundia chapa yake mpya na kuhakikisha haki hiyo haikiukwi ambayo tunatumai itampa yeye na familia yake mapato hata baada ya kustaafu.

“Kampuni yetu ilielewa jukumu lake na ilifanya kwa uadilifu na heshima anayostahili mwanamichezo yeyote mashuhuri. Hata hivyo, pia tunaelewa wakati wa kutengana na mteja wetu wa zamani ili kumpa fursa ya kukuwa na kuwajibikia safari yake.

“Tunaendelea kusherehekea ukuaji wa Ferdinand na ufanisi wake na kila mara tutajivunia hatua atakazopiga mwenyewe na katika ukimbiaji wa mbio fupi nchini Kenya,” taarifa yake kampuni hiyo ilisema.

SNOLEGAL inajiondoa siku chache baada ya kampuni ya DBA Afrika iliyokuwa ikisimamia shughuli za mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 25 zikiwemo safari nje ya Kenya kabla ya Olimpiki 2020 na mazoezi kukatiza uhusiano naye.

DBA Afrika ilidai kuwa Omanyala hakudumisha maadili ya kampuni hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Joash Onyango na Gonzalez warejea Harambee Stars kwa...

Korti yaamuru raia wa Tanzania anayeishi uingereza akamatwe...