Habari Mseto

Mawakili wajaa mahakamani kumtetea mwenzaao Prof Ojienda

December 31st, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI mwenye tajriba ya juu Profesa Tom Ojienda Jumatatu aliwakilishwa na mawakili zaidi ya 30 alipofikishwa kortini kujibu mashtaka ya ulaghai wa Sh89 milioni.

Mawakili hao walifika kwa wingi kuonyesha ushirikiano wao katika kupinga ‘kukandamizwa kwa haki za mawakili’.

“Mawakili hawapasi kukamatwa na kudhulumiwa kwa kulipisha wateja wao pesa nyingi,” alisema wakili Danstan Omari mmoja wa mawakili waliomtetea Prof Ojienda aliyetiwa nguvuni Ijumaa wiki iliyopita na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Muthaiga.

Mawakili Okong’o Omogen James Orengo. Picha/ Richard Munguti

Prof Ojienda anatazamia kupigiwa kura na mawakili  wengi kuendelea kuwawakilisha katika tume ya kuajiri watumishi katika idara ya mahakama (JSC) kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Kundi la mawakili hao liliongozwa na mawakili wenye tajriba ya juu kama Mabw James Orengo, Okong’o Omogeni, Dkt John Khaminwa, Dkt Otiende Amolo, Danstan Omari, Nelson Havi na Charles Omanga.

Profesa Tom Ojienda akiwa mahakamani Desemba 31, 2018. Picha/ Richard Munguti

Walipofika mahakamani walijigawanya wakwa vikundi viwili.

Kundi moja lilienda kumwakilisha Prof Ojienda mbele ya Jaji Enock Chacha Mwita na kundi lingine lilienda mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Mbele ya Bi Mutuku Prof Ojienda alitarajiwa kushtakiwa kwa ulaghai wa mamilioni ya pesa.

Anadaiwa alipokea kwa njia ya kuilaghai kampuni ya kutengeneza sukari ya Mumias (MSC).

Hakimu mwandamizi Martha Mutuku. Picha/ Richard Munguti

Mashtaka sita aliyofunguliwa wakili huyo yanaonyesha kuwa alitia kibindoni zaidi ya Sh89 milioni.

Bi Mutuku alikabidhiwa agizo la mahakama kuu iliyoonyesha mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji amezuiliwa kumshtaki wakili huyo.