Habari za Kitaifa

Mawakili walafi wamulikwa kula fidia za waathiriwa wa ajali

April 24th, 2024 3 min read

NA JOSEPH OPENDA

BAADHI ya mawakili wanawatesa na kuwahangaisha waathiriwa wanyonge wa ajali kwa kuwapokonya fidia kutoka kwa kampuni za bima, Taifa Leo imebaini.

Waathiriwa wamekuwa wakiteseka licha ya mawakili kulipwa fidia na kampuni za bima na kukataa kuwalipa inavyopaswa.

Bw Anthony Muchiri, 50 alikuwa mkulima hodari takriban miaka 30 iliyopita eneo la Nakuru kabla ya ajali kuzima ndoto ya maisha yake na sasa anategemea misaada.

Mkasa ulitokea mnamo Aprili 15, 2003 na kumnyima mwendo wa kawaida kwa kuwa anatembea kwa kiti cha magurudumu.

Akiwa katika harakati ya kukagua shamba lake Subukia, alihusika katika ajali katika barabara ya Bahati–Subukia eneo la Kirengero.

Matatu aliyosafiria iligongana na gari jingine na kumsababishia majeraha mabaya – miguuni, kifuani, kichwani na kumpotezea meno kadhaa.

Alikuwa miongoni mwa waliopelekwa hospitalini na wasamaria wema.

Katika hali hiyo, Bw Muchiri alipatana na mtu aliyetaka kumsaidia apate fidia kufuatia ajali hiyo.

Hapo ndipo masaibu yake yaliongezeka kwa sababu alimkubali mtu bila kumchunguza kama ni wakili mwadilifu ama la.

Mnamo Julai 9, 2003, mashtaka yaliwasilishwa katika mahakama ya Nakuru na kampuni moja ya mawakili kwa niaba ya Bw Muchiri na wengine 10 dhidi ya dereva na mmiliki wa matatu kwa kusababisha ajali kupitia uendeshaji hatari wa gari.

Mkondo tofauti

Gari hilo lilikuwa limekatiwa bima ya Standard Assurance Kenya Limited. Licha ya kampuni hii kukubali kutoa fidia, kesi kortini ilichukua mkondo mwingine usiotarajiwa.

Kupitia makubaliano ya mawakili wa pande mbili, kampuni ya bima ilielekezwa kufidia asilimia 85 ya hasara na kuwaachia waathiriwa asilimia 15 iliyobaki.

Katika uamuzi wa Oktoba 16, 2003, mahakama ilimtuza Bw Muchiri fidia ya Sh127,000.

Sasa, mwathiriwa huyu anadai hajawahi kupokea hata ndururu licha ya kushiriki hatua zote za kesi na kutoa ushahidi.

Ilimchukua miaka 20 kugundua kuwa kesi hiyo ilikamilika mwaka wa 2003.

Alibaini haya alipoenda kortini kuchukua stakabadhi za kesi hiyo mwaka jana.

Taifa Leo imethibitisha kuwa Standard Assurance Kenya Limited ilitoa hundi ya Sh903,000 kwa kampuni ya uwakili ya Ng’ang’a Kiarie and Company advocates kufidia waathiriwa 11 wa ajali.

“Nilikuwa nikihudhuria shughuli za korti hadi 2005 kisha nikachoka kwa sababu sikuwa na uwezo wa kuenda kortini. Nilipigwa na butwaa kugundua kesi iliamuliwa 2003,” Bw Muchiri alisikitika.

Anakiri kuwa juhudi zake kumfikia wakili zimefeli na kumvunja moyo.

“Alibadilisha namba za simu na hajawahi kuwasiliana nami tena. Nilimtafuta kila mahali hadi katika biashara zake Nairobi lakini sikuruhusiwa kumuona,” akateta.

Bw Muchiri anasubiri uamuzi kutoka kwa Tume ya Kusikiliza Malalamishi dhidi ya Mawakili baada ya kuwasilisha kesi mnamo Machi 18, 2023

Yaliyomkumba Bw Muchiri ni moja kati ya visa vingi ambapo watu wameteswa na mawakili.

Bw Cyprian Salanya, 22, alijikuta katika hali hii baada ya kupata ajali kazini katika kampuni ya Faida Seeds mjini Nakuru alipokuwa akipakia na kupakua magunia ya nafaka.

Akiwa kazini, magunia 14 ya nafaka yalimwangukia na kumvunja uti wa mgongo.

Bw Salanya alitibiwa katika hospitali ya Nakuru Level Five kwa siku tisa ambapo awali mwajiri wake alikuwa analipa bili ya matibabu ya kima cha Sh230,000.

Baba huyu wa mtoto mmoja aliachwa aendelee kulipa bili zilizofuata.

“Baada ya miezi 4, kampuni hiyo iliwasiliana nami na kutaka kunilipa Sh200,000 kama fidia. Nilitafuta ushauri kutoka kwa wakili ambaye alinishauri nisichukue pesa hizo. Baadaye nilitambulishwa kwa wakili wa Kituo Cha Sheria ambaye alishauri nisichukue pesa na badala yake ataenda kujadiliana na kampuni iongeze fidia,” akasema.

Kulingana na Bw Salanya, wakili huyo alikutana na mwajiri wake na baadaye aliahidi kuwashtaki kortini.
Baada ya mwezi mmoja, wakili alimwelekeza Bw Salanya aende achukue hundi na amtumie Sh5,000 kabla ya kutoweka.

“Baada ya kumpa Sh5,000, nilitumia pesa zilizobaki kwa matibabu hadi zikaisha. Bado ninahitaji kutibiwa lakini sina pesa,” akasema.

Juhudi zetu za kumfikia wakili huyo hazikufua dafu kwani hakupokea simu ama kujibu jumbe fupi tulizotuma.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK) tawi la Nakuru, Bw Henry Opondo amekiri kuwa wamepokea malalamishi hususan kuhusiana na ukiukaji wa mikataba kati ya mawakili na wateja wao pamoja na matapeli wanaojifanya mawakili.Bw Opondo anashauri waathiriwa kuripoti kwa Tume ya Kusikiliza Malalamishi dhidi ya Mawakili ambayo itafanya uchunguzi na kutoa mapendekezo kutegemea matokeo.

Sehemu ya 60 (1) ya Sheria ya Mawakili inafafanua kuwa utovu wa maadili katika taaluma ya sheria ni mwenendo wa aibu na usio na heshima ambao hauendani na hadhi ya wakili.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili nchini (LSK) tawi la Nakuru, Bw Henry Opondo amekiri kuwa wamepokea malalamishi hususan kuhusiana na ukiukaji wa mikataba kati ya mawakili na wateja wao pamoja na matapeli wanaojifanya mawakili.

Bw Opondo anashauri walalamishi walioathiriwa na visa hivi watoe ripoti kwa Tume ya Kusikiliza Malalamishi dhidi ya Mawakili ambayo itafanya uchunguzi na kutoa mapendekezo kutegemea matokeo.

“Baada ya tume kubaini kuna utovu wa maadili, kesi hiyo huwasilishwa kwa Jopo la kutoa adhabu la LSK ili litoe mwelekeo zaidi. Hata hivyo, matapeli watachukuliwa hatua upesi. Kama mteja ana shaka na wakili, kabla ya kuelewana, anafaa kupiga ripoti katika kituo cha polisi bila kuchelewa,” alisema.

Kadhalika, Bw Opondo aliongeza kuwa LSK itafanya kazi na polisi kuthibitisha kama wakili anayeshukiwa ni mkora ili kusaidia hatua za kesi kortini.

LSK inashauri umma kutumia majukwaa ya kidijitali ya chama hicho kuthibitisha kama mawakili wamesajiliwa kabla ya kutia sahihi makubaliano.