Mawakili waliowakilisha Jumwa walia kuitiwa DCI

Mawakili waliowakilisha Jumwa walia kuitiwa DCI

Na PHILIP MUYANGA

MAWAKILI waliokuwa wakimwakilisha Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa katika kesi inayohusu madai ya ufisadi, wamelalamikia uamuzi wa mahakama kutumia Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwaita ili wafike mbele ya hakimu.

Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bi Edna Nyaloti alikuwa amewaagiza mawakili Jared Magolo, Danstan Omari, Shadrack Wambui na Titus Kirui wafike mbele yake, akiwalaumu kwa kile alikiita ni “mienendo inayochelewesha kesi hiyo”.

Kulingana nao, ilikuwa makosa kwa mahakama kuwatumia maagizo kupitia kwa DCI ilhali kuna mbinu nyingine zinazoweza kutumiwa.

“Kuna mbinu zinazostahili kutumiwa ikiwa tunatakikana kufika mahakamani. Hakuna wakili yeyote kati yetu ambaye ni mshukiwa,” akasema Bw Omari.

Bw Omari alisema waliamua kujiondoa katika kesi ya Bi Jumwa na washukiwa wengine sita kwa sababu waliona kama kwamba mahakama inapendelea upande mmoja.

Alisema wamewasilisha barua kwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kulalamikia mienendo ya korti hiyo.

Hata hivyo, hakimu aliwaambia mawakili hao kwamba aliwaita ili kuharakisha kesi hiyo kwa kuhakikisha kuwa wamemkabidhi wakili mpya, Bw Duncan Osoro, stakabadhi za kesi.

“DCI walikosea kwa kuwachukulia kama wahalifu. Hii mahakama huheshimu mawakili. Sijawahi kufunga wakili yeyote seli, kila wakili amekaa mahali ambapo anastahili kukaa,” akasema Bi Nyaloti.

Aliongeza kuwa hana mapendeleo kaitka kesi hiyo kwani hajawahi kutoa hukumu bila kutegemea ushahidi unaowasilishwa mahakamani.

Alilazimika kuahirisha kesi, akisema haitakuwa haki kuendelea kuisikiliza ilhali Bw Osoro hajakutana na washtakiwa ili ajiandae.

Bi Jumwa alishtakiwa kwa madai ya kushiriki katika njama ya ufisadi wa Sh19 milioni zilizolipwa kwa kampuni ya Multiserve kupitia kwa zabuni nambari MLD/NG-CDF/01/2017/2018 iliyotolewa na afisi ya NG-CDF ya Malindi.

Washtakiwa wenzake ni Wachu Omar, Kennedy Otieno, Bernard Riba, Sophia Saidi, Margaret Kalume, Robert Katana na kampuni ya Multiserve.

Imedaiwa kuwa kitendo hicho kilitokea kati ya Mei 14 na Oktoba 12, 2018 katika kaunti ndogo ya Malindi, Kaunti ya Kilifi.

You can share this post!

WASONGA: Uadilifu ndicho kiungo muhimu uchaguzini wala si...

GWIJI WA WIKI: Sharon Nafula Wekesa