Mawakili wamrai Kangogo ajisalimishe

Mawakili wamrai Kangogo ajisalimishe

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha Mawakili Kenya (LSK) kimejiunga na watu wengine kumrai afisa wa polisi anayesakwa, Caroline Kangogo kujisalimisha, kikiahidi kumwakilisha mahakamani.

Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho, Bi Mercy Wambua, alisema lazima haki za mshukiwa huyo zizingatiwe kama mshtakiwa mwingine yeyote kwa mujibu wa sheria. Alisema taharuki inaendelea kuongezeka nchini kwani haijabainika aliko polisi huyo hadi sasa.

“Kwa wakati huu, wasiwasi uliopo ni kuwa akiendelea kukosekana, anahatarisha maisha ya wananchi wengine kwani inasemekana amejihami vikali,” akasema Bw Wambua.

Alimwomba Bi Kangogo kusalimisha bunduki yake ama silaha nyingine ambayo huenda anayo kwa taasisi za usalama nchini, akisema chama hicho kitamwakilisha mahakamani.

Hata hivyo, alisema mshukiwa huyo hajawasiliana naye kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari. Alisema chama hicho ndicho kilichomteua wakili mkongwe John Khaminwa, Jumanne, kumwakilisha Bi Kangogo mahakamani ikiwa atajisalimisha.

Ilipotajwa kuwa Dkt Khaminwa ndiye angemwakilisha Bi Kangogo, kulizuka uvumi kwamba alikuwa amewasiliana na mawakili kuiomba mahakama kumwachilia kwa dhamana iwapo angejisalimisha.

Ilidaiwa alihofia usalama wake ikiwa angewekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Hata hivyo, Dkt Khamiwa aliiambia Taifa Leo kuwa ataenda mahakamani kutafuta agizo la kuwazuia polisi kumkamata Bi Kangogo.

Licha ya hayo, alitoa masharti kadhaa kwa mshukiwa kabla ya kumpa usaidizi.

“Lazima asalimishe bunduki yake ama silaha yoyote anayomiliki kwa sasa kwa polisi, afisi za kampuni yangu au afisi nyingine ya serikali inayofaa,” akasema, akiongeza kuwa yuko tayari kumwakilisha mahakamani hadi suala lake litakapoamuliwa.

Bi Kangogo anadaiwa kuwaua watu wawili wiki iliyopita katika kaunti za Nakuru na Kiambu.

Babake mshukiwa, Barnaba Kipkoech, amemrai kujisalimisha kwa polisi na kueleza anachojua kuhusiana na matukio hayo mawili badala ya kutoroka.

“Anaelewa sheria na anajua hatua mwafaka zaidi anayofaa kuchukua kwa sasa ni kujisalimisha. Hata hivyo, wito wangu ni apewe ulinzi wa kutosha,” akasema.

Maafisa wanaochunguza aliko mshukiwa wamewahoji watu kadhaa wanaoaminika kuwasiliana na Bi Kangogo. Miongoni mwao ni daktari na polisi mmoja mwanamke anayeaminika kuwa rafiki wake wa karibu.

Bi Kangogo anahusishwa na mauaji ya polisi mwenzake, John Ogweno, Jumatatu wiki iliyopita.

Vile vile, anasakwa kuhusiana na mauaji ya Bw Peter Ndwiga, aliyepatikana ameuawa katika hoteli moja, Kiambu, siku moja baada ya mauaji ya Ogweno.

You can share this post!

Mmoja wa wanaotaka cheo cha kamishna wa IEBC apendekeza...

Kesi ya Jumwa kuanza mwaka 2022