Mawakili wamtoroka Sonko ‘apambane na hali yake’

Mawakili wamtoroka Sonko ‘apambane na hali yake’

Na RICHARD MUNGUTI

KUNDI jipya la mawakili sita waliokuwa wanamwakilisha aliyekuwa gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko Jumanne walijiondoa katika kesi ya ufisadi ya Sh10 milioni inayomkabili.

Mawakili hao, Dkt John Khaminwa, Assa Nyakundi, Wilfred Nyamu, Philip Kahigu, Martin Kuruga na Evans Ondieki, waliondoka katika kesi hiyo huku wakimwacha Sonko akipambana na mashahidi walioitwa na upande wa mashtaka unaoongozwa na Bw Taibu Ali Taibu akisaidiana na mawakili wengine watatu wa serikali.

Dkt Khaminwa na mawakili hao walimlaumu hakimu mkuu Douglas Ogoti anayesikiza kesi hiyo kwa kuonyesha upendeleo kwa kuwanyima fursa ya kupata nakala za ushahidi na kujiandaa kuwakabili mashahidi watakaoitwa katika kesi hiyo ya ufisadi dhidi ya Sonko.

Dkt Khaminwa alisema Sonko aliwasihi waanze kumtetea mwezi jana na hawajapokea nakala za ushahidi kutoka kwa mawakili waliokuwa wanamwakilisha hapo awali Mabw Cecil Miller na George Kithi.

Mawakili hao walimsihi Ogoti aahirishe kesi hiyo kuwezesha Sonko kupata afueni baada ya kuagizwa apumzike kwa siku 14 aliporuhusiwa kutoka Nairobi Hospital alikolazwa kwa muda wa miezi miwili.

Pia walisema washukiwa wengine wawili walioshtakiwa kwa ugaidi pamoja na Sonko wameambukizwa maradhi ya Corona na huenda gavana huyo wa zamani amepata virusi hivyo.

Mawakili  waliojitoa katika kesi hiyo ni Wilfred Nyamu (kushoto) , Philip Kahigu na Assa Nyakundi (kulia). PICHA/ RICHARD MUNGUTI

“Tunaomba uahirishe hii kesi kwa vile Sonko alitangamana na wahasiriwa wa corona. Sisi wote hatuko salama. Ahirisha hii kesi kwa siku 14 tu ndipo Sonko apate afueni,” Dkt Khaminwa alisema.

Pia Dkt Khaminwa alisema Sonko anakabiliwa na changamoto za maradhi ya ubongo na madaktari wamesema kesi “isitishwe apokee matibabu.”

Mahakama ilielezwa kuwa anatakiwa kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji wa nyonga.

“Mshtakiwa hawezi kaa kwa muda mrefu na hii mahakama huendeleza vikao hadi usiku.Ataumia,” akasema Dkt Khaminwa.

Wakili mwenye tajriba ya juu alieleza mahakama “afya ya mtu yapasa kuzingatiwa. Hakuna haja ya kuendelea na kesi na mmoja sio buheri wa afya.”

Mahakama ilielezwa aliyekuwa afisa mkuu kaunti ya Nairobi John Gakuo alifia jela kwa ukaidi wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi iliyokataa kumwachilia akapate matibabu.

“Hatutaki Sonko aumie. Ahirisha hii kesi,” akasema Dkt khaminwa. Lakini Bw Taibu alipinga ombi hilo la kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuomba kesi iendelee.

Mawakili hao walikabiliana na Bw Taibu lakini hakimu akakataa kuahirisha kesi na kuamuru shahidi aliyefichwa aanze kutoa ushahidi.

Ni wakati huo mawakili wote sita waliondoka na kumwacha Sonko ajipiganie licha ya kuwa mgonjwa.

Wakili huyo alisema Bw Sonko ni mgonjwa na madaktari sita wa Nairobi Hospital walimwamuru apumzike kwa siku 14 kuanzia Machi 11,2021.

“Hatujapokea nakala za mashahidi kutoka kwa EACC na kamwe hatuwezi endelea na kesi bila nakala za mashahidi tuandae utetezi wa Sonko,” alisema Dkt Khaminwa.

Wasaidizi wa Sonko wambebea mito ya kukalia. PICHA/ RICHARD MUNGUNTI

Bw Ogoti alikataa kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa siku 60 kuwezesha Dkt Khaminwa na mawakili wengine watano kupokea ushahidi kutoka kwa mawakili Cecil Miller na George Kithi na tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC).

Hakimu huyo aliamuru kesi iendelee akisema mawakili hao walikuwa na muda wa kupokea ushahidi kutoka kwa EACC.

Lakini Dkt Khaminwa na wenzake walisema kuwa hawawezi kamwe kuendelea na kesi hiyo kama hawajajiandaa kuendelea na kesi hiyo.

“Tuliombwa na Bw Sonko tuanze kumtetea mwezi uliopita. Tuliomba muda tuwasiliane na Mabw Miller na Kithi kupokea ushahidi wa mashahidi walioorodheshwa kutoa ushahidi dhidi ya Bw Sonko lakini mahakama ikasisitiza tuendelee na kesi,” alisema Dkt Khaminwa.

Wakili huyo alisema mahakama iliamuru EACC iwatumie ushahidi kwa njia ya mtandao.

Dkt Khaminwa alisema bado hawajapokea ushahidi na hakimu anataka kesi iendelee faraghani bila wananchi kujua kinachoendelea.

“Yamkini hakimu anataka kumsukuma bw Sonko jela kwa haraka,” alisema Dkt Khaminwa. Bw Ogoti aliamuru kesi dhidi ya Bw Sonko iendelee bila wakili.

Wasaidizi wa Sonko walimletea mto (pilo) za kukalia ili asiumie mno makalio kwa vile viti ni vigumu.

You can share this post!

NCPB yaahidi kuboresha huduma kwa wakulima wa mahindi

Hofu wanaofariki baada ya kupata chanjo wakiongezeka