Habari Mseto

Mawathe na mbunge wa Ugenya kurudi debeni

December 22nd, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Embakasi kusini Julius Mawathe na Ugenya Bw David Ochieng hawatafurahia sikukuu ya Krismasi baada ya Mahakama ya Juu kuharamisha uchaguzi wao.

Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Njoki  Ndung’u na Isaac Lenaola walisema kuwa wawili hao hawakushinda viti vyao vya ubunge kwa mujibu wa sheria.

Majaji hao waliamuru tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) waandae uchaguzi mpya na huru katika maeneo hayo ya uwakilishi bungeni.

Katika kesi ya Embakasi  Bw Mawathe alikuwa ametangazwa mshindi na afisa aliyesimamia uchaguzi huo mnamo Agosti 8 2017.

Ushindi wa Bw Mawathe ulipingwa na Mbunge wa zamani wa eneo hilo Bw Irshad Sumra.

Bw Sumra alilalamika kuwa uchaguzi katika eneo hilo la Embakasi ulikumbwa na undanganyifu, utoaji hongo na kutozingatiwa kwa sheria za uchaguzi.

Mbunge wa Embakasi kusini Julius Mawathe (pili kulia). Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilifahamishwa na Bw Sumra aliyewania kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Bw Mawathe aliwania kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Wiper ambacho kinara wake ni Bw Kalonzo Musyoka.

Bw Sumra aliyewania kiti hicho kwa tikiti ya chama cha ODM alilalamika kuwa hakuna matokeo kamili kuhusu mshindi wa kiti hicho.

Kwa mujibu wa afisa aliyesimamia  uchaguzi huo Bw Mawathe alizoa kura 33,949 naye Bw Sumra akafaulu kupata kura 33,708.

Mbali na matokeo hayo kulitolewa matangazo mengine  yaliyoonyesha kwamba Bw Mawathe alijipatia kura 33, 348 naye Bw Sumra akapata kura 33,004.

Mbunge wa zamani wa Embakasi kusini Irshad Sumra (kati). Picha/ Richard Munguti

Seti nyingine ya matokeo hayo ilikuwa Bw Mawathe alikuwa amejipatia kura 33,880 naye Bw Sumra akapata kura 33,000.

Majaji hao watano walikubaliana na  uamuzi wa mahakama ya rufaa kwamba Bw Mawathe hakushinda kiti hicho kwa njia inayokubalika kisheria.

“Tunakubaliana na mahakama aya rufaa kwamba  hakuna matokeo kamili ya kuonyesha kuwa Bw Mawathe alitwaa ushindi kwa njia nzuri,” walisema majaji hao watano.

Mahakama ilisema kuwa afisa aliyesimamia uchaguzi huo hakuwa ameshtakiwa nab w Sumra na wala pia hakuwasilisha Fomu nambari 35 iliyokuwa imejazwa matokeo ya uchaguzi huo.

Bw Sumra. Picha/ Richard Munguti

“Bila hati hizi zilizojazwa matokeo ya kura ya kila mwaniaji kiti hiki cha Embakasi itakuwa vigumu kubaini mshindi,” walisema majaji hao watano.

Pia walisema afisa aliyesimamia uchaguzi huo hakufikas kortini kijitetea kisa na maana ni mwanachama wa chama cha Wiper kilichomdhamini Bw Mawathe.

“Afisa huyu alimbagua Bw Sumra kwa vile alikuwa ni afisa wa chama cha Wiper naye mlalamishi alikuwa ODM,” walisema majaji hao.

Baada ya kufikia uamuzi kuwa Bw Mawathe hakuchaguliwa kwa njia halali.

“Twaamuru IEBC iandae uchaguzi mwingine katika maeneo ya  Embakasi kusini na Ugenya kisha ufanywe kwa mujibu wa sheria za uchaguzi,”mahakama iliamuru.