Mawaziri 4 wampuuza Naibu Rais

Mawaziri 4 wampuuza Naibu Rais

Na CHARLES WASONGA

MAWAZIRI wanne wa serikali jana walikataa kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Naibu Rais William Ruto kujadili masuala mbalimbali kuhusu usimamizi wa fedha katika serikali za kaunti.

Dkt Ruto alikuwa amewaalika mawaziri Ukur Yatani (Fedha), James Macharia (Uchukuzi), Peter Munya (Kilimo), Prof George Magoha (Elimu) na waziri wa Ugatuzi, Charles Keter kuhudhuria mkutano wa Baraza la Masuala ya Bajeti na Uchumi linaloshirika wawakilishi wa ngazi mbili za serikali (IBEC).

Hata hivyo, ni Bw Keter pekee ndiye aliyehudhuria mkutano huo uliofanyika katika makazi rasmi ya Naibu Rais katika mtaa wa Karen, Nairobi.Bw Yatani ambaye ni mwanachama wa kudumu wa IBEC kwa kushikilia cheo cha Uwaziri wa Fedha, alisema hangehudhuria mkutano huo kwa sababu yuko katika ziara nje ya nchi.

“Niko nje ya nchi lakini maafisa wangu watahudhuria,” akanukuliwa akisema. Bw Yatani aliwakilishwa katika mkutano huo na katibu katika wizara yake Julius Muia ambaye aliwasilisha taarifa kuhusu sera ya bajeti (BPS) ya mwaka ujao wa kifedha wa 2022/2023.

Kwa upande wake, Bw Macharia alisema ameandamana na Rais Uhuru Kenyatta katika ziara ya siku tatu nchini Afrika Kusini. Kiongozi wa Taifa anafanya ziara hiyo kwa mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambapo masuala yenye umuhimu kati ya Kenya na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Mawaziri Munya na Magoha hawakutoa maelezo yoyote kuhusu sababu zilizochangia hatua yao ya kutohudhuria mkutano huo.Aidha, hawakutuma maafisa wao katika kikao hicho ambacho kilijadili masuala kama ubinafsishaji wa viwanda vya miwa na ufadhili wa vyuo vya kiufundi (TVET).

Baraza la Magavana (CoG) lilihudhuria mkutano huo likiongozwa na mwenyekiti wake Martin Nyaga Wambora ambaye ni Gavana wa Embu.Hata hivyo, Bw Wambora hakuwepo Dkt Ruto alipohutubia kikao cha wanahabari baada ya mkutano huo.

Magavana wengine waliohudhuria ni pamoja na Anne Waiguru (Kirinyaga), Ndiritu Mureithi (Laikipia), Paul Chepkwony (Kericho), Josephat Nanok (Turkana) na gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago.

Mawaziri Munya, Macharia na Yatani wametofautiana kisiasa na Naibu Rais kwa kujitokeza waziwazi kuunga mkono azma ya kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022. Wamekuwa wakihudhuria mikutano ya waziri mkuu huyo wa zamani ya kuuza sera zake chini ya kauli mbiu ya Azimio la Umoja.

Aidha, mawaziri hawa wamekuwa mstari wa mbele kukosa mpango wa kukuza uchumi kuanzia ngazi ya mashinani, maarufu kama Bottom Up unapigiwa debe na Dkt RutoMbw Munya na Macharia ni miongoni mwa mawaziri ambao mnamo 2019 walielekezewa tuhuma za kupanga njama ya kumuua Naibu Rais.

Mawaziri katika serikali ya Jubilee walianza kutomheshimu Dkt Ruto baada yake kudai ametengwa serikalini na majukumu yake kupewa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.Hii ni baada ya uhusiano wake kudorora tangu Machi 9, 2018 Rais Kenyatta aliporidhiana kisiasa na Bw Odinga.

Duru zinasema kuwa tangu wakati huo Dkt Ruto amekuwa akikwepa mikutano ya baraza la mawaziri na Baraza la Kitaifa kuhusu Usalama (NLC).Ni katika sherehe za kitaifa pekee ambapo Naibu Rais amekuwa akishiriki jukwaa moja na Rais Kenyatta pamoja na mawaziri wa serikali.

You can share this post!

Mada nzito Raila, Ruto wanakwepa

STEVE ITELA: Wadau washirikiane kutatua changamoto za makao...

T L