Habari

Mawaziri walio na ndimi telezi

November 20th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

TUKIO ambapo Waziri wa Elimu Profesa George Magoha anadaiwa kumtusi mkurugenzi wa elimu Kaunti ya Uasin Gishu, Dkt Gitonga Mbaka limeendeleza tabia ya mawaziri wa serikali ya Jubilee ambao wamekuwa na kiburi, kutoa habari za kupotosha na kudharau umma.

Profesa Magoha ni miongoni mwa mawaziri kadhaa ambao wamewahi kuonyesha kiburi, dharau, kukaganya na kupotosha umma kupitia kauli wanazotoa.

Wenzake Najib Balala, James Macharia, Mutahi Kagwe na Peter Munya wamekuwa wakikosolewa na Wakenya kwa kauli na maamuzi yao yanayoudhi, au hata kutoa ahadi zsiizotimia.

Mbali na kisa anachochunguzwa kwa kutusi afisa anayehudumu chini yake, Profesa Magoha amekuwa akikosolewa kwa kauli zake kuhusu elimu wakati huu wa janga la corona.

Waziri huyo ambaye alihudumu kama naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi kwa miaka kumi amekuwa akifoka kwa hasira anapotakiwa kufafanua masuala katika wizara yake. Kati ya Juni na Agosti, alidai kwamba walimu walioajiriwa na bodi za shule walikuwa wamelipwa ilhali walikuwa wakiteseka baada ya shule kufungwa. Mnamo Oktoba, alilaumiwa kwa kutokuwa na msimamo kuhusu ufunguzi wa shule. Japo alikuwa ametangaza kuwa masomo yatarejelewa Januari, alibadilisha nia na kuagiza wanafunzi wa kidato cha nne, darasa la nane na gredi ya nne waripoti shuleni Oktoba 12. “

MUTAHI KAGWE, AFYA

Ingawa amesifiwa kwa juhudi zake za kukabili janga la corona, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe naye aliudhi Wakenya kwa kupuuza chanjo ya ugonjwa huo zinazovumbuliwa na kampuni kubwa ulimwenguni. Hii ni licha ya majaribio ya chanjo kuanza kufanywa nchini na watu wanaoambukizwa na kuuawa na ugonjwa huo kuongezeka nchini.

Aidha, wizara yake imekumbwa na madai ya ufisadi ukiwemo wa mabilioni ya pesa zilizotengwa kukabiliana na janga la corona.

Waziri Kagwe hakuhusishwa na ufisadi ambao uliathiri shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu (KEMSA). Licha ya kudai nchi ilikuwa na vifaa vya kutosha na bora vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya corona, madaktari wamekanusha madai hayo na kusema hawataendelea kuhatarisha maisha yao. .

JAMES MACHARIA, UCHUKUZI

Waziri wa uchukuzi James Macharia amekuwa akijikwaa katika matangazo yake kuhusu hatua muhimu zinazochukuliwa na wizara yake. Ahadi nyingi anazotoa huwa hazitmii na ni za kuudhi. Hii ni pamoja na kuanzishwa kwa mabasi ya mwendo wa kasi jijini na usafirishaji wa mizigo yote kutoka bandari ya Mombasa hadi kituo cha kupakua mizigo jijini Nairobi.

Wiki jana, Mahakama Kuu iliamua agizo hilo halikufuata sheria na kuamuru likome kutekelezwa.

NAJIB BALALA, UTALII

Naye waziri wa utalii Najib Balala amelaumiwa kwa kufanya maamuzi yanayosababishia nchi hasara.

Mnamo 2018 alitoa matamshi kukashifu waliomlaumu kufuatia vifo vya vifaru 10 waliohamishiwa mbuga ya Tsavo kutoka mbuga ya Nairobi.

Bw Balala alijipata motoni alipowaambia waliomtaka kuwajibika na kujiuzulu kufuatia vifo vya vifaru hao waende kuzimu akisema hawakumteua.

“Sitajiulzuu na wanaonitaka nijiuzulu wanaweza kwenda kuzimu,” alisema Bw Balala.

Baadaye alilazimika kuomba msamaha kuhusu matamshi hayo joto lilipozidi.

“Ninajuta kwa kutoa matamshi hayo,” alieleza kamati ya bunge iliyomuita wakati wa kuchunguza vifo vya wanyama hao.

Wizara yake pia ilipigwa darubini kufuatia madai ya matumizi mabaya ya pesa.

Mnamo 2018, aliitwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu madai ya kutoa zabuni ya Sh100 ya kuandaa mkutano uliofanyika Nairobi- 2017 Destination Expo Conference.

Bw Balala pia alilaumiwa kwa kutofautiana na waziri mwenzake alipotetea matumizi ya shisha ilipopigwa marufuku na aliyekuwa Waziri wa Afya Cleopa Mailu mnamo 2017.

PETER MUNYA, KILIMO

Tangu ateuliwe waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya ameanzisha mabadiliko kadha wa kadha ambayo yamemfanya kulaumiwa. Wakulima na wafanyabiashara wa miraa wamemlaumu kwa kutumia chama cha ushirika anachodaiwa kuwa na uhusiano nacho kusambaza pesa za hazina ya miraa. Aidha, anapigwa darubini baada ya kufichuliwa kuwa sukari kutoka nje inaingizwa nchini licha ya marufuku aliyotangaza Julai mwaka huu.

RAYCHELLE OMAMO, ULINZI

Waziri wa Ulinzi Raychelle Omamo aliwakasirisha wabunge alipotapatapa walipomuuliza sababu ya serikali kutowaleta nchini Wakenya waliokuwa wamekwama Wuhan, China, wakati nchi nyingi zilipositisha safari za ndege virusi vya corona vilipozuka. Badala ya kujibu swali aliloulizwa, Bi Omamo alisema kwamba hakuwa na uwezo wa kubaini mwelekeo ambao ugonjwa ungechukua.

KERIAKO TOBIKO, MAZINGIRA

Mnamo Septemba 2020 Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko alijipata motoni kwa kumwita Naibu Rais William Ruto karani katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

“Heshima ni nipe nikupe. Iwapo hauwezi kumheshimu rais, basi haufai kutarajia uheshimiwe. Hata Naibu Rais ni karani wa rais, ikiwa ninaheshimu rais, Naibu Rais anafaa kumheshimu,” alisema.