Mawimbi ya BBI yanavyoyumbisha kundi la Kieleweke

Mawimbi ya BBI yanavyoyumbisha kundi la Kieleweke

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a kumwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta mapema wiki hii kwamba huenda wenyeji wa Mlima Kenya wakakosa kuunga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), imeibua hali ya sintofahamu ya kisiasa katika kundi la ‘Kieleweke’.

Imeibuka kuwa baadhi ya wanasiasa katika kundi hilo sasa wanapanga kuhama na kujiunga na mirengo mingine ya siasa, baada ya kugundua kuwa idadi kubwa ya wenyeji hawaungi mkono ripoti hiyo.

Hilo linafuatia hatua ya Seneta Maalum Isaac Mwaura kutangaza kujiunga na kundi la ‘Tangatanga’ wiki iliyopita, ambapo alikaribishwa na viongozi wa mrengo huo, akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Duru zimeliambia Jamvi la Siasa kuwa baadhi ya viongozi wanaopanga kuhama mrengo wa ‘Kieleweke’ ni wabunge Sabina Chege (Murang’a), Mary Wamaua (Maragua), Gathoni Wamucomba (Kiambu), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) na wengine.Uamuzi wao umetajwa kuchangiwa na idadi kubwa ya wenyeji kuhisi kuwa huenda ripoti hiyo ikakosa kuwafaa kwa vyovyote vile, kutokana na kudorora kwa sekta muhimu kama vile kilimo.

“Wenyeji wengi wa Mlima Kenya wanahisi BBI ni njama ya kuwafaa viongozi wachache. Hivyo, idadi kubwa haitaki kusikia lolote kuihusu. Wanataka kujua ni mikakati ipi ambayo serikali imeweka ili kuimarisha masuala muhimu kama vile kilimo cha kahawa, majanichai, pareto kati ya mazao mengine. Ni kutokana na hilo ambapo niliamua kuhama ‘Kieleweke’,” akasema Bw Mwaura.

Baadhi ya viongozi waliozungumza na ukumbi huu walisema imekuwa vigumu kuipigia debe ripoti hiyo katika eneo hilo, kwani wenyeji pia wanahisi kusalitiwa na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Baadhi yao pia wanaiona BBI kama mpango wa kumtengenezea njia kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, njia ya kuwania urais mwaka wa 2022. “Imekuwa vigumu kuipigia debe BBI Mlima Kenya. Ndio uhalisia wa mambo, ila viongozi wengi katika ‘Kieleweke’ hawataki kusema hilo hadharani,” akasema mbunge Kimani Ichung’wa wa Kikuyu, ambaye ni miongoni mwa washirika wakuu wa karibu wa Dkt Ruto.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya Seneta Kang’ata inapaswa kumfungua macho Rais Kenyatta na washirika wake wanaoipigia debe ripoti hiyo kuwa huenda hali isiwe kama wengi wanavyofasiri.Kwa mujibu wa Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU, Nairobi, huenda mwelekeo huo unaashiria kuna mengi yanayopaswa kufanywa kabla ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwa wananchi.

“Huenda wakati umefika ambapo Rais Kenyatta na washirika wake wanafaa waende mashinani na kusikiliza hisia za wananchi kuhusu malalamishi yao. Pengine huenda hilo likampa taswira kamili kuhusu hali ya kisiasa ilivyo kuihusu ripoti hiyo,” akasema Prof Munene.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiendesha harakati za kuipigia debe ripoti hiyo ni Mbunge Maalum Maina Kamanda, Kiongozi wa Wengi Bungeni Amos Kimunya, magavana Francis Kimemia (Nyandarua), Anne Waiguru (Kirinyaga), Mutahi Kahiga (Nyeri), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Kiraitu Murungi (Meru) kati ya wengine.

Viongozi hao wamekuwa wakishikilia kwamba kinyume na hisia za wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao unamuunga mkono Dkt Ruto, ukanda huo ndio utakaofaidika zaidi ikiwa Wakenya wataipitisha ripoti hiyo.Hivyo, wanaeleza kuwa viongozi kama Dkt Kang’ata ni “wanasiasa wabinafsi ambao lengo lao ni kuipotosha nchi kuhusu hali ya kisiasa ilivyo katika ukanda huo.”

“Mimi hutangamana na wenyeji wa kaunti yangu kila siku kupitia shughuli mbalimbali. Ninawafahamu kwa undani kuliko viongozi kama maseneta, ambao huendesha shughuli zao nyingi jijini Nairobi. Kwa hivyo, Dkt Kang’ata na viongozi wengine wanapaswa kukoma kuipotosha nchi kuhusu uungwaji mkono wa BBI,” akasema Gavana Kiraitu Murungi wa Meru.

Kulingana na Bw Murungi, kuna uwezekano Dkt Kang’ata anatumiwa kimakusudi na ‘Tangatanga’ kuchora taswira na dhana ya uwongo kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo na maeneo mengine nchini.Vilevile, alisema kuna uwezekano kiongozi huyo anapanga kuhamia ‘Tangatanga’ kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa.

“Ikiwa kiongozi anapanga kuhama kutoka mrengo mmoja na kujiunga na mwingine, hapaswi kuzua mifarakano isiyofaa. Anapaswa kufanya maamuzi yake kwa njia ya amani. Huo ndio uungwana katika siasa kwani hakuna yeyote anayelazimishwa kufuata mrengo wowote ule,” akasema Bw Murungi.

Naye Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa masuala ya siasa, anasema huu ni wakati wa wanasiasa kufanya maamuzi yatakayowafaa, hasa uchaguzi mkuu wa 2022 unapoendelea kukaribia.

“Yanayoendelea kwa sasa si nadra kwani hujitokeza kila uchaguzi mkuu unapokaribia. Wanasiasa lazima wahamie mirengo wanayohisi ina umaarufu miongoni mwa wafuasi wao,” akasema Bw Muga.

Mbunge Kanini Keega (Kieni) aliwataja wanasiasa wanaohama ‘Kieleweke’ kama “wasaliti” ambao kamwe hawawezi kuaminiwa kisiasa hata kidogo.Anasema kundi hilo bado liko imara, kwani linaendeleza ajenda za maendeleo za Rais Kenyatta.

You can share this post!

Matokeo ya uchaguzi mdogo Kwale yalivyowapa maadui wa Joho...

Magufuli ampongeza waziri wa China kwa kutovaa maski