Habari Mseto

Mawimbi ya redio yafichua kuhusu waliomuua Willy Kimani

October 13th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MTAALAMU wa masuala ya teknolojia katika Idara ya Polisi ameeleza mahakama kuu jinsi washukiwa wa mauaji ya wakili mtetezi wa haki za binadamu Willy Kimani, mteja wake na dereva wa teksi walivyotambuliwa.

Bw Kennedy Kiradi Mwadime alisema akitumia teknolojia ya mtandao wa Google aliweza kuandama jinsi Inspekta Fredick Leliman alikokuwa mnamo Juni 23 na 24 , 2016.

Akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji dhidi ya Insp Leliman na maafisa wengine wanne wa polisi Leonard Maina, Sylvia Wanjohi, Stephen Morogo na kachero Peter Ngugi Kamau alisema mawimbi ya redio hiyo ndiyo yalitambua kule washtakiwa hao walienda.

Jaji Jessie Leesit alielezwa Kimani, Mwenda na Muiruri walitekwa nyara na Insp Leliman kisha wakazuiliwa katika kituo cha polisi  wa utawala cha Syokimau.

Waliondolewa kwenye seli na kuuawa katika eneo la Soweto kisha maiti zao zikatupwa katika mto Athi eneo la Ol Donyo Sabuk kwenye mpaka wa kaunti za Machakos na Kiambu. Washtakiwa hawa wamekanusha waliwaua watatu hao.

Jaji Lesiit alifahamishwa na Bw Mwadime kuwa redio ya polisi ya mawasiliano aliyokuwa nayo Inspekta Leliman ilionyesha kule kwote alikoenda kati ya Mahakama ya Mavoko hadi eneo la Ol Donyo Sabuk ambapo maiti za Kimani , mwendeshaji boda boda Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri zilipatikana kama zimeoza.

Washukiwa wa mauaji ya wakili Willy Kimani wakiwa kortini Alhamisi watazama picha za Google na wakili Cliff Ombeta huku mawakili na washtakiwa wajadiliana baada ya kusikizwa kwa kesi. Picha/ Richard Munguti

Maiti za watatu hao zilipatikana siku saba baada ya kutoweka kwao kuripotiwa.

Akiongozwa kutoa ushahidi na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Nicholas Mutuku , Bw Mwadime alisema redio aliyokuwa nayo Insp Leliman ilionyesha alikuwa katika mahakama ya Mavoko mwendo wa saa sita mchana , kisha akatoka hapo akaenda katika kampi ya maafisa wa polisi wa utawala ya Syokimau.

Redio hiyo ilionyesha afisa huyo aliyesimamia kituo hicho cha polisi cha Syokimau alirudi tena hadi kituo cha Polisi cha Mavoko ambapo alikaa hadi usiku na kurudi tena Syokimau.

Redio yake ilionyesha ilitoka  kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau hadi eneo la mauaji la Soweto.

Hatimaye redio hiyo ilionekana ikirudi barabara kuu ya Mombasa na kwenda City Cabanas.

Kimitandao , redio hiyo ilifuatwa hadi Juja kisha mawasiliano yakapotea hadi tena eneo la Valley View ambap Insp Leliman alikuwa akiishi.

“Kwa kutumia ujuzi wa kimitandao tuliweza kuandama kule redio aliyokuwa amepewa Leliman iliko kati ya Juni 23 na 24 2016 alikoenda na wakati aliporudi  katika makazi yake mtaa wa Valley View eneo la Syokimau,” alisema Bw Mwadime.

Ushahidi uliowasilishwa wasema kuwa maafisa hao wa polisi waliwatoa kwenye seli Kimani, Mwenda na Muiruri na kuwaua na kusafirisha maiti zao hadi mtoni Athi River eneo la Ol Donyo Sabuk na kuitupa mle.

Kesi itaendelea kusikizwa Novemba 12-16, 2018.