MAYATIMA WA BBI

MAYATIMA WA BBI

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Mahakama Kuu kubatilisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba 2020, maarufu kama Mpango wa Maridhiano (BBI), imeweka mashakani wanasiasa waliomezea mate nyadhifa zilizopendekezwa.

Iwapo Mahakama ya Rufaa haitabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na jopo la majaji watano; Prof Joel Mgugi, Jaji George Odunga, Jaji Chacha Mwita, Jaji Jairus Ngaah na Teresia Matheka, baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe BBI, wakiwemo viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA),  huenda wakajipata wakisuka upya mikakati yao kujiokoa kisiasa.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa viongozi walio chini ya muungano wa OKA – Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Seneta Gideon Moi (Kanu), Bw Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta Moses Wetang’ula wa Ford Kenya – walikuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na BBI.

Bw Mudavadi na Bw Musyoka wamekuwa katika baradi ya kisiasa tangu 2013 na katika BBI waliona fursa ya kujiunga na serikali kwenye uchaguzi wa 2022.

Wengine ambao wameachwa kwenye mataa ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na magavana Bw Hassan Joho (Mombasa), Bi Ann Waiguru (Kirinyaga) na Bi Charity Ngilu (Kitui); na wabunge Bw Junet Mohamed (Suna Mashariki) na Bw John Mbadi (Suba Kusini) kati ya wengine ambao walikuwa msitari wa mbele kupigia debe mchakato huo.

Mahakama Kuu ilitoa sababu 20 zilizowashawishi kuharamisha Mswada wa BBI. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Rais Uhuru Kenyatta hana mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kurekebisha Katiba.

Viongozi wa muungano wa OKA wamekuwa wakitarajia kuwa mmoja wao angeungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Seneta wa Baringo Moi ndiye amekuwa akipigiwa upatu kuungwa mkono na Rais Kenyatta ili kurudisha hisani kwa Rais Mstaafu Hayati Daniel arap Moi.

Moi aliwaacha vinywa wazi wanasiasa wenye uzoefu, akiwemo kiongozi wa ODM Raila Odinga na Bw Musyoka, alipotangaza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta kuwania urais 2002 kupitia chama cha Kanu licha ya kutobobea katika siasa wakati huo.

Endapo Seneta Moi ataungwa mkono, viongozi wengine wa OKA wangenufaika na nyadhifa zaidi zilizopendekezwa ndani ya Mswada wa BBI kama vile nafasi ya waziri mkuu atakayekuwa na manaibu wawili.

Alhamisi, Seneta wa Kitui Enoch Wambua alifichua kwamba alipiga kura ya kuunga mkono BBI baada ya kushawishiwa na Bw Musyoka.

Kulingana na Wambua, Musyoka anahofia kuwa azma yake ya kutaka kuwa rais 2022 itasambaratika endapo juhudi za kutaka kurekebisha Katiba ya 2010 zitagonga mwamba.

Seneta wa Kitui pia alifichua kuwa majadiliano kuhusu namna wakazi wa eneo la Ukambani, ikiwemo Kaunti ya Kitui, watakavyonufaika na serikali ya OKA, yanaendelea miongoni mwa viongozi wa juu serikalini.

Bw Wambua ni miongoni mwa maseneta waliokuwa wakipinga Mswada wa BBI lakini wakabadili misimamo yao wakati wa kupiga kura.

“Inaonekana kila kiongozi ndani ya OKA ameahidiwa kuungwa mkono kuwa rais 2022 na Rais Kenyatta. Hiyo inamaanisha kwamba rais hajawaeleza viongozi wa OKA atakaye muunga mkono kuwa rais,” anasema Profesa Medo Misama.

Bw Musyoka hajatoa tamko lolote kuhusiana na uamuzi wa Mahakama Kuu. Lakini Bw Mudavadi Ijumaa alipokuwa katika eneo la Kilgoris, Kaunti ya Narok, alikosoa uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kusema kuwa ilikosa kuweka maanani maslahi ya umma kwa kubatilisha Mswada wa BBI.

Bw Mudavadi aliyeoneka kuwa mwenye hamaki pia alishutumu majaji kwa ‘kumkosea heshima’ Rais Kenyatta.

Lakini jana, kiongozi huyo wa Amani National Alliance (ANC), kupitia taarifa yake aliyotuma kwa vyombo vya habari, alibadili kauli na kuwataka wanasiasa wenzake kuheshimu uamuzi wa mahakama.

“Mswada wa BBI una mengi mema kama vile mgawo wa fedha kwa wadi na kuongeza fedha zinazopelekwa kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35. Hatufai kutupilia mbali BBI badala yake tuketi tushughulikie masuala yaliyoibuliwa na Mahakama Kuu,” akasema Bw Mudavadi.

Bw Atwoli na Bw Murathe wamekuwa wandani wa Rais Kenyatta tangu kuanzishwa kwa BBI miaka mitatu iliyopita – hali ambayo imezua tetesi kwamba huenda wanamezea mate viti serikalini endapo mswada huo utapitishwa.

Wawili hao na aliyekuw mbunge wa Gatanga Peter Kenneth wamekuwa wakikutana na Bw Odinga kuweka mikakati ya BBI.

Jana, Bw Atwoli alisema  kuwa hana haja na wadhifa serikalini. Alisisitiza kuwa Mswada wa BBI utaendelea kama ilivyopangwa licha ya kupigwa breki na Mahakama Kuu.

Bw Junet na Bw Mbadi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM wamekuwa wakipigania BBI ili kudhihirisha uaminifu wake kwa Bw Odinga ili kuongeza nafasi yao ya kushinda viti katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Junet ametangaza kutetea kiti chake cha ubunge huku Bw Mbadi akijiandaa kujitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay.

Gavana Joho – akiwa kigogo wa siasa katika eneo la Pwani – alikuwa na nafasi nzuri ya kunufaika na wadhifa serikalini iwapo  Mswada wa BBI utapitishwa na Wakenya.

Huku Bi Waiguru akikabiliwa na ushindani mkubwa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kirinyaga 2022, wadadisi wanasema BBI ilimuweka karibu na Rais Kenyatta ambaye angali anadhibiti siasa za eneo la Mlima Kenya.

Wiki iliyopita, Bw Murathe alifichua kuwa Rais Kenyatta ataendelea kuwa mwenyekiti wa Jubilee hata baada ya kustaafu mwaka ujao.

Gavana Ngilu amekuwa akihusishwa kwa karibu na Rais Kenyatta katika mchakato wa BBI

You can share this post!

Ruto aonywa asifurahie masaibu ya Rais Uhuru

Vifo 174 na mahangaiko Israeli ikizidi kuwalipua Wapalestina