Michezo

Mazembe jagina wa soka aliyesahaulika

March 18th, 2019 3 min read

NA PHYLIS MUSASIA

UNAPOMUONA kwa mara ya kwanza, mwili wake ni dhaifu, lakini ujasiri na ukakamavu unadhihirika wazi ndani ya macho yake.

Bw Patrick Imbusi almaarufu ‘Mazembe’ mwenye umri wa miaka 52 ni mkazi wa Ronda eneobunge la Nakuru Mashariki. Yeye ni mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa zaidi ya timu saba za mpira katika eneo hilo.

Licha ya bidii na ukakamavu wake wa kuona kwamba vijana wa Ronda wananufaika na kujiendeleza maishani, jamvi la umasikini na mahangaiko limeendelea kumgubika yeye pamoja na familia yake.

Ziara ya Dimba nyumbani kwake ilibaini maisha magumu anayopitia Mazembe ndani ya chumba chake kidogo kilichotengenezwa kwa udongo. Wingi wa mataji na vikombe alivyotuzwa kwa muda wa miaka 19 kupitia ushindi wa michuano ya timu zake ni ishara ya mafanikio yake.

Alieleza kwamba alihamia mjini Nakuru mnamo 1984 kutoka Butere, Kakamega akiwa na matumani mengi ya kupata riziki.

“Mwazo, nikiwa kijana mdogo nilikuwa mmoja wa wanadensi katika kundi moja lililojulikana kama Mazembe kule Butere. Kuanzia wakati huo, watu walinitambua kwa jina la Mazembe, nadhani kutokana na sarakasi za muziki na densi kwa jumla na hadi sasa kila mtu huniita kwa jina hili,” akaeleza.

Baadaye Bw Mazembe alisema aliachana na kundi hilo na kujiunga na timu ya mpira wa kandanda ya Rhino FC mtaani kwao ambayo baadaye ilibadili jina na kujiita Green Buffalo.

Rhonda na Ponda Mali ilikuwa mitaa hatari sana. Wakazi walionekana wakiporwa hadharani na hamna aliyewatetea. Hata hivyo, Mazembe alisema alichagua kuishi Ronda kwa sababu gharama ya maisha huko ilikuwa chini na ilitoshana na hali aliokuwa akiishi. Kuwakusanya vijana ambao walikuwa wamezozea kuvuta bangi na kujihusisha na mambo mengi hatari ikawa ni changamoto kubwa sana.

Lakini Mazembe alisema alitoboa hilo mnamo 2000 kupitia usaidizi wa kanisa moja la Calvary Baptist mtaani Ronda.

Miaka ilisonga na Bw Mazembe akashuhudia jinsi timu ziendelea kuzaana na hata kufanya vyema Zaidi. Timu kama vile Mwariki FC, Makadara, Small Simba, Wembley FC, Everstars na Asek FC zote zikazaana chini ya mamalaka ya Mazembe.

Lakini licha ya bidii hiyo ambayo imechukua zaidi ya miaka 19 Mazembe bado hajaweza kupata uhisani wowote wala usaidizi wa wizara ya michezo au hata kutoka kwa kiongozi yeyote.

Alisema pesa wanazopata kutokana na ushindi wa mechi mbalimbali huwawezesha tu kununua jezi na sare na inapofika wakati wa kusajili timu zao kwa viwango tofauti vya mechi wao hujikuta hawana chochote. Wamelazimika mara si moja kukosa kuorodheshwa katika mechi mbalimbali ikiwemo ligi kwa sababu ya fedha.

“Vijana wangu wanao uwezo wa kufanya vyema zaidi na wameonyesha ukakamavu wao kwa kushinda karibu kila mechi wanayo jitoza ndani. Jambo linaloturudisha nyuma ni hela za usafiri katika mechi za nje na zile za kumlipa refarii,” akaeleza Mazembe.

Bw Alexander Ang’ana kocha wa timu hitajika ya Asek aliwakumbuka Bw Eric Ambuya wa Tusker FC, Kennedy Owino wa KCB, Charles Kwakha wa Chemilil, Haron Mwale wa timu ya Ulinzi na Moses Mudavadi Mwale wa Bandari FC huku akisema wote ni matunda ya Bw Mazembe baada ya kupitia mikononi mwake kama vijana wa mtaa wa Ronda.

Bw Ang’ana alisema vijana wa timu hizo wameweza kupata vikombe mbalimbali kama vile kutoka kwa mchwano mkali wa Ogada uliohusisha timu 32, mchwano wa Murugu uliong’anag’aniwa Disemba 2018, mchwano wa Lotto miongoni mwa michwano mingine mingi.

Aliomba wizara ya michezo pamoja na serikali kwa jumla iingilie kati na iwape msaada jambo ambalo alisema anamatumaini makubwa itawezesha vijana hao kwenda mbali zaidi.

“Tumeweza kuwapeleka vijana wengi ambao wamejiunga na timu za kitaifa humu nchini na bado kunao wengi ambao wanaazimia kufika kule pia. Tukipata msaada wa serikali au wizara husika tutasaidika sana,” akaeleza.

Uwanja waotumia kuchezea vijana wa Ronda umebandikwa jila la Mazembe na hata magari ya usafiri wa abiria wanaoishi eneo hilo yamenyakuwa lebo ya jina la Mazembe kwa miaka mingi.