Makala

AKILIMALI: Mazeras stones yalivyoteka soko la ufundi

February 21st, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

SIKU za mbeleni wajenzi na wasanifu mijengo walipendelea kutumia mawe ya kawaida pamoja na saruji kusimamisha kuta za nyumba.Matofali ya kuchoma au mawe yalibadilishana nafasi kutegemea chaguo la wajenzi husika.

Baadaye ikagundulika kuwa kujenga nyumba ukitumia matofali tu bila kuongeza nakshi ya urembo haikupendeza sana wala kuleta umaridadi.

Ndipo wajasiria mali kwa ushirikiano na wamiliki wa migodi wamekuja na mbinu nyingine ya kupatia mawe taswira tofauti ya kupendeza. Mawe ya mazeras yanatumika katika viwanda kwa ajili ya maonyesho na wakati mwingine kitega uchumi kwa wafanyibiashara.

Aidha inasemekana nondo na wadudu wengine hawawezi kupenya kutokana na udhabiti wake.

Licha ya kuleta ushindani mkubwa dhidi ya bidhaa nyinginezo za kujenga mawe ya  mazeras yameteka soko la ufundi sio tu barani bali pia kimataifa.

Japo wajuzi wa kuchonga mawe haya ni wachache humu nchini,juhudi zaidi zinahitajika  ili kuwahamasisha vijana wanaosumbuka wakitafuta kazi wachangamkie ulingo huu unaolipa.

Kaunti zinazojihusisha na uchongaji mawe nchini ni Machakos, Kisii na Kwale.Ni wazi kuwa hii ni nafasi nzuri ya ajira ambayo haijagunduliwa na wawekezaji wengi mijini.

Francis Kioni alisomea taaluma ya uhandisi , lakini baadaye aliamua kujiajiri mnamo 2018 ili ajiongezee kipato.Akiwa mtaalam wa miundo msingi alifanya utafiti wa kina kuhusu mawe ya kujengea nyumba za kisasa.

Alitaka kuwapunguzia wawekezaji  gharama ya kujenga nyumba kwa kuzingatia ubora na udhabiti wa mijengo.Anasema aligundua kuwa wamiliki wa nyumba za makazi na ofisi za kibiashara walipenda kutumia mawe ya Mazeras isipokuwa tatizo kubwa ilikuwa ni uagizaji.

Alistawisha kiwanda cha kuyachonga katika mji wa Nakuru na kuajiri vijana sita wanaomsaidia.

Anaeleza kuyachonga mawe panahitajika kuwa na  mtambo maalum wa kuyalainisha baada ya kutolewa kwenye eneo la uchimbaji mawe hayo.

Pili; yahifadhiwe katika sehemu iliyo salama yasije yakaibiwa, ikiwa hili ndilo jambo la maana.

Anahimiza kuwa mawe haya mbali na kuwa bei nafuu,  matokeo yake hayana mfano.

Kila jiwe huwa na upekee wake kinyume na jingine. Yaani mawe ya mazeras ni tofauti kwa umbo, rangi, na mwonekano.

Bw Francis Kioni akionesha baadhi ya mawe ya Mazera baada ya kuchongwa na kulainishwa katika mji wa Nakuru. Picha/ Richard Maosi

“Mawe ya mazera yanaweza kutumika katika majukwaa hasa sehemu za kuwakaribishia wageni (reception), bafu, jikoni, vidimbwi vya kuogelea na mikahawa ya kifahari. Rangi yake ya kawaida huwa ni hudhurungi,nyeupe au nyekundu.Mawe haya huchukua muda wa miaka mingi kukolea vizuri na kukua yakiwa ndani ya ardhi kabla ya kuchimbuliwa,”alisema.

Yamejaa madini ya quartize yanayoyapatia ugumu wake na michirizi mieupe ya kupendeza .Hufanya vyema kwenye maeneo ya maji ya chumvi au matimbo yaliyojaa mchanga wa sandy.Mawe hayo hutiwa kwenye mtambo yakachongwa na kufanywa vifusi laini virefu kwa kina.

Maumbo ya mstatili yakiwa ndio mwafaka zaidi.

“Matumizi ya mazeras ni tofauti kulingana na lengo la anayehitaji.Tukianzia na mijini ambapo miundo mbinu imenawiri yanaweza kujengea kuta na kuzirembesha kwa wakati mmoja au kutengeneza sakafu.Majumba ya kibinafsi na ya kibiashara yakilengwa zaidi.Vilevile soko lake humu nchini na hata ulaya ni pana huku kiwango  kinachotengezwa kwa siku hakitoshi kuyakidhi mahitaji ya wanunuzi wanaozidi kuongezeka kila kukicha.Kioni anasema kwa siku anaweza kuchonga mawe 800 huku soko likihitaji zaidi ya mazera 4000 kila siku,” akasema.

Hata hivyo alifichulia Akilimali kuwa mazeras hayaathiriki na mvua wala joto jingi.

Ubora wake hutegemea namna ya kuyatunza.

Baada ya kuchonga kitu laini kama pamba kinaweza kuwekwa baina ya mazera ili yasivunjike yanapogongana wakati wa kupakia na kusafirisha.Biashara hii iliyoanza katika kaunti ya Machakos imepenya hadi katika maeneo ya Nakuru ambapo yamepatiwa jina la ‘Machakos silver stone’.

Mbali na kuleta ushindani mkali kwa mawe ya kawaida.Aidha yanaweza kutengeneza sehemu ya kuegesha gari au ukumbi wa kubarizi.

Sio tu kwa sababu ya rangi yake bali pia wahandisi wameonekana kuyapigia upatu mawe ya mazeras kutokana ugumu usiokuwa wa kawaida.

Kioni anasema huyapata mawe kutoka kwenye matimbo viungani mwa mji wa Nakuru.Ametengea sehemu mbali na mji inayotumika kama karakana ya shughuli zake kuyakata, kuchonga na kuyalainisha.

Kazi zake ni pevu siku zote za wiki akishirikiana na wafanyikazi  aliowaajiri.

Kila mmoja hupokea mshahara usiopungua 30,000 kwa mwezi na marupurupu.Kiwanda chake kimesaidia vijana wanaosumbuka kutafuta kazi.

Anashauri kuwa kwenda chuo kikuu bila kupata ujuzi wa kujikimu maishani ndiyo changamoto inayozidi kuwalemaza vijana.

Hivyo basi pana haja washika dau kuhimiza vijana waanze kufanya kazi za mikono ili kuongeza kama ziada ya vitabuni.