Habari Mseto

Maziko ya mjane wa Ronald Ngala ni leo

May 2nd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed ameomboleza mwendazake Mama Esther akimtaja kama mtu aliyependa nchi yake ya Kenya na kujitolea katika kuinua kina mama pamoja na masuala ya elimu kote nchini.

Mama Esther, ambaye ni mkewe marehemu shujaa Ronald Ngala, alifariki Aprili 26 katika hospitali ya Mombasa baada ya kuugua kwa wiki tatu.

Mama Esther alikuwa mamaye waziri wa zamani Noah Katana Ngala na shangaziye mwandishi maarufu wa michezo katika kampuni ya Nation Media Group, Larry Ngala, miongoni mwa wengine wengi.

“Kwa kumpoteza Mama Esther, familia kubwa ya Ngala na watu wa Kaloleni, kaunti ya Kilifi imepoteza mama aliyekuwa shujaa na mfano kwa wengi. Busara yake, ujuzi na upendo wake kwa wakazi wa Kilifi ni kitu ambacho kitakumbukwa milele. Mungu awapatie utulivu na ujasiri familia yake, watu wa Kilifi na eneo la Pwani kwa jumla,” alisema Waziri Amina Mohamed siku ya Ijumaa.

Mama Esther pia alikuwa mama mkwe kwa mawaziri wa zamani Kazungu Kambi na marehemu Mathias Keah.

Mazishi ya Mama Esther ni leo Jumamosi nyumbani kwake Vishakani katika kaunti ndogo ya Kaloleni.

Kutokana na janga la virusi vya corona, familia yake ndiyo itahudhuria mazishi.