MAZINGIRA NA SAYANSI: Faida tele za kuendesha baiskeli na kutembea

MAZINGIRA NA SAYANSI: Faida tele za kuendesha baiskeli na kutembea

Na MWANDISHI WETU

WATU wasiopungua wawili waendao kwa miguu hugongwa na kuuawa na magari katika barabara za humu nchini kila siku.

Kulingana na takwimu za Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA), watu 485 wamefariki baaada ya kugongwa na magari kati ya Januari 1 na June 4, mwaka huu. Watu 445 waligongwa na magari na kufariki katika kipindi sawa mwaka jana.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa waendeshaji baiskeli, 31 waliuawa katika kati ya Januari na Juni, mwaka huu.

Hii ni ithibati kwamba barabara za humu nchini, haswa maeneo ya mijini ni sumu kwa waendao kwa miguu na waendeshao baiskeli.

Kuendesha baiskeli na hata kutembea kwa miguu kuna manufaa tele kiafya na pia kunasaidia kupunguza gesi iliyotanda angani ambayo husababisha joto jingi hapa duniani.

Kuendesha baiskeli au kutembea hufanyisha mwili mazoezi hivyo kuwezesha moyo, mapafu na mishipa ya damu kufanya kazi vyema.

Aidha hupunguza mafuta mwilini hivyo kumfanya mhusika kuwa na afya bora. Kuendesha baiskeli pia ni aina ya burudani.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa mwaka jana, matumizi ya baiskeli yanaweza kupunguza uchafuzi wa anga kwa gesi hatari kwa asilimia 7.

“Ikiwa asilimia 10 ya safari katika maeneo ya mijini zingekuwa kwa baiskeli au kutembea, gesi chafu zilizojazana angani zingepungua kwa asilimia 7,” inasema ripoti hiyo ya UN.

Tofauti na pikipiki, baiskeli haitoi moshi ambao huchafua anga. Moshi ambao hutoka katika pikipiki, magari au viwanda hurundikana angani na kusababisha joto hapa duniani kuongezeka. Joto hilo limesababisha barafu iliyokuwa imeganda katika milima mirefu kama vile Mlima Kenya au Kilimanjaro nchini Tanzania kuyeyuka.

Mlima Kenya ndio wa pili barani Afrika kwa urefu na ndicho chanzo cha maji ya mito inayoingiza maji ndani ya Mto Tana na mabwawa ya Masinga na mto Ewaso Nyiro.

Wataalamu wanatabiri kwamba barafu yote iliyoko juu ya Mlima Kenya itaendelea kuyeyuka katika kipindi cha miaka 30 ijayo kutokana na ongezeko la joto duniani.

Inaaminika kuwa mito na mabwawa ambayo yamekuwa yakipata maji kutoka Mlima Kenya huenda ikakauka hivyo kusababisha uhaba wa maji nchini.

Kulingana na UN, kuendesha baiskeli au kutembea umbali mfupi ni moja ya njia za kukabili ongezeko la joto duniani.

Wanasayansi waliokuwa wakitafiti Safu ya Milima ya Himalaya ambayo inajumuisha Everest, mlima mrefu zaidi duniani, walionya kuwa milima hiyo inapoteza b

arafu kwa kasi ya juu kutokana na kuongezeka kwa joto duniani.

Watafiti hao walisema milima hiyo imepoteza asilimia 25 ya barafu ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mnamo 1975.

UN imeonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi ikiwa joto litaongezeka duniani kwa sentigredi 3°C.

Kwa sasa joto limeongezeka kwa sentigredi 1.5°C na wataalamu wanaonya kuwa huenda likafikia 3°C iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kukabiliana na hali hiyo.

Nchini Kenya, hakuna barabara zilizotengwa mahususi kwa ajili ya waendeshaji baiskeli. Hivyo, waendesha baiskeli hulazimika kutumia barabara moja na magari au pikipiki na kuhatarisha maisha yao.

Jijini Nairobi, kwa mfano, njia ndogo zilizoachwa kwa ajili ya waendao kwa miguu ndizo hutumiwa na wahudumu wa bodaboda, kuna msongamano wa wachuuzi na mikokoteni pia.

“Serikali zinafaa kuweka sera mwafaka za kuhakikisha kuwa kuna barabara za kutosha zinazotumiwa na baiskeli,” inasema ripoti ya UN.

“Serikali haina budi kujenga barabara za baiskeli na kisha kuhamasisha wananchi kuhusu manufaa ya kuendesha baiskeli au kutembea,” inaongezea.

UN inasema kujengwa kwa barabara salama za baiskeli kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika maeneo ya mijini kwani watu wengi wataanza kutumia baiskeli kwenda kazini badala ya magari.

Jiji la London (nchini Uingereza) lilipatia usafiri wa baiskeli kipaumbele mnamo 2003 na idadi ya magari ilipungua kwa asilimia sita ndani ya miaka miwili huku gesi chafu iliyoenda angani ikipungua kwa asilimia 20 kufikia mwaka 2008.

Mnamo 2015 serikali ya Kaunti ya Nairobi ilizindua sera kuhusu kuhamasisha wakazi wa jiji kutumia baiskeli kwenda kazini.

Sera hiyo pia ilipendekeza ujenzi wa barabara spesheli ambazo zingetumiwa na waendeshaji baiskeli au waendao kwa miguu. Lakini sera hiyo imebaki tu maandishi kwenye kumbukumbu.

You can share this post!

AFYA: Kukabili maumivu makali ya kichwa

USALAMA BARABARANI: Serikali kutumia Sh1bn kuimarisha sekta...

adminleo