Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Hewa chafu inakupunguzia hadi miaka 3 ya kuishi – Utafiti

March 10th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

HEWA chafu tunayopumua kila siku, haswa mijini na maeneo ya shughuli nyingi kama vile viwandani, marundo ya taka, stendi za magari au matimbo ni hatari kuliko maradhi ya Ukimwi, uvutaji wa sigara na malaria.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kemia ya Max Planck na Chuo Kikuu cha Medical Centre Mainz kwa lengo la kubaini maradhi hatari yanayosababisha idadi kubwa ya vifo duniani, ulibaini kuwa hewa chafu; iliyosheheni vumbi na moshi wenye sumu, inaua watu wengi zaidi ikilinganishwa na maradhi kama vile malaria, virusi vya HIV, malaria, vita, na kadhalika.

Watafiti hao pia walibaini kuwa hewa chafu inafupisha maisha kwa zaidi ya miaka miwili. Hiyo ina maana kuwa watu wanaoishi katika maeneo yenye hewa chafu hufariki mapema ikilinganishwa na wenzao wanaoishi sehemu zilizo na hewa safi.

Hesabu iliyofanywa na watafiti hao ilibaini kuwa hewa chafu inapunguza muda wa kuishi kwa miaka mitatu. Sigara hupunguza maisha ya wavutaji wake kwa miaka miwili. Maradhi ya Ukimwi hupunguza muda wa kuishi kwa mwaka mmoja.

Watafiti hao walibaini kwamba hewa chafu ndiyo inaongoza kwa kusababisha kuharibika kwa mimba na vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa takribani watoto 600,000 wa chini ya umri wa miaka 15 hufariki kila mwaka kutokana na maradhi yanayohusiana na hewa chafu.

Wengi wao hufariki kwa kupumua hewa iliyosheheni moshi wa kuni, mafuta ya taa kati ya vitu vingine vinavyochafua hewa nyumbani.

Kulingana na Sensa ya 2019, karibu familia 9 milioni zinatumia kuni, makaa au mafuta ya taa kupika hasa katika maeneo ya vijijini.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa hewa chafu husababisha asilimia 11 ya vifo barani Afrika, ikiwemo Kenya. Hiyo inamaanisha kuwa kwa kila watu 100 wanaofariki humu nchini, 11 huaga dunia kutokana na maradhi yanayohusiana na upumuaji wa hewa chafu.

Bara Asia, linalojumuisha nchi kama vile China, linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyosababishwa na hewa chafu kwa asilimia 32.

Huo ni utafiti wa kwanza kutathmini madhara ya hewa chafu kwa afya ya binadamu ikilinganishwa na maradhi hatari.

Ripoti ya utafiti huo inaonyesha kuwa Australia ndio inaongoza kwa kuwa na hewa safi zaidi duniani. Hewa chafu inahusishwa na maradhi ya moyo na kiharusi.

Kulingana na watafiti, karibu asilimia 60 ya vifo vinavyotokana na hewa chafu vinaweza kuepukika.

Utafiti uliofanywa nchini China na Chuo Kikuu cha Beijing Normal uliochapishwa mwaka jana ulihusisha hewa chafu na kuharibika kwa mimba.

Watafiti hao walihusisha jumla ya wajawazito 255,668 jijini Beijing kati ya 2009 na 2017. Watafiti hao walipima ubora wa hewa nyumbani na kazini kwa kila mshiriki.

Watafiti hao walibaini kuwa mimba za wanawake 17,497 ziliharibika ndani ya miezi mitatu ya kwanza.

Wanasayansi hao wanasema hewa chafu huzuia mtoto kukua tumboni na kufariki polepole bila mama kuhisi uchungu. Hali hiyo hutokea ndani ya wiki 12 za ujauzito na mara nyingi huwa mama hajui kwamba tayari amepoteza mtoto.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sydney nchini Japan ulibaini kuwa hewa chafu inaweza kusababisha moyo kusimama ghafla.

Utafiti mwingine uliofanywa na watafiti wa Uhispania ulibainisha kuwa hewa chafu husababisha watu kuwa na mifupa dhaifu ambayo huvunjika kwa urahisi.

Watafiti hao walisema kuwa wakazi wa maeneo ya mijini wana mifupa dhaifu haswa katika maeneo ya nyonga na mgongo na wako katika hatari ya kuumia mara kwa mara.

Wanasayansi hao wanaamini kuwa chembechembe za vyuma zilizo kwenye hewa chafu huingia kwenye damu na kumfanya mtu kuzeeka haraka licha ya kuwa na umri mdogo.

Utafiti uliofanywa miongoni mwa watu 4,000 ulibaini kwamba mifupa ya watu wanaopumua hewa chafu ni dhaifu na katika sehemu ya chini ya mgongo, nyonga na mapaja.

Hewa chafu huathiri homoni ya parathyroid ambayo hudhibiti uzalishaji wa madini ya calcium ambayo yanahusika katika kufanya mifupa kuwa migumu.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa hewa chafu inasababisha kujikunja na kuzeeka kwa ngozi.

Gesi inayojulikana kama ozone (O3), ambayo pia huhusika katika kuchafua hewa, huhusika pakubwa katika kufanya ngozi kulegea na kumfanya mtu kuonekana aliyezeeka.

Tafiti pia zimehusisha hewa chafu na matatizo ya ubongo miongoni mwa watoto na watu wazima.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Cincinnati cha nchini Amerika ulibaini kuwa japo hewa chafu huathiri ukuaji wa ubongo wa watoto zaidi, watu wazima pia wako hatarini.

Madhara ya hewa chafu

1. Maradhi ya moyo, mapafu, kansa

2. Kuharibika kwa mimba

3. Huathiri ukuaji wa ubongo wa watoto

4. Husababisha mifupa ya nyonga na mgongo kuwa dhaifu

5. Kujikunja na kuzeeka kwa ngozi