Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mafuriko husababisha msongo wa mawazo

February 18th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI mnamo Desemba ilitangaza kuwa imetenga Sh6.1 bilioni kwa ajili ya kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko wanaoishi kambini kupata makao.

Msemaji wa serikali Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna alisema sehemu ya fedha hizo pia itatumiwa kukarabati miundomsingi iliyoharibiwa na mafuriko kote nchini.

Takwimu za serikali zilizotolewa miezi miwili iliyopita zilionyesha kuwa jumla ya Wakenya 17,000 walifurushwa makwao kutokana na mafuriko. Watu zaidi ya watu 140 walifariki. Aidha watu 330,000 walikuwa wameathiriwa na mafuriko kufikia Desemba, mwaka jana.

Lakini idadi ya waathiriwa huenda imeongezeka kwani kumekuwa na visa vingi vya mafuriko ndani ya muda wa miezi miwili iliyopita.

Baadhi ya waathiriwa waliofurushwa makwao na mafuriko na kisha kurejea tayari wamesahaulika. Wachache ambao watajengewa makazi na serikali watasahaulika pindi baada ya kupewa nyumba.

Lakini utafiti uliofanywa nchini Uingereza unaonyesha kuwa waathiriwa wa mafuriko wanahitaji msaada mkubwa zaidi mbali na kujengewa nyumba au kupewa chakula.

Watafiti hao wanasema kuwa mafuriko yana athari kubwa zaidi kwa afya na waathiriwa huhisi makali kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa watafiti, mikasa ya mafuriko husababisha waathiriwa kuwa na matatizo ya msongo wa mawazo kwa muda mrefu.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Aberdeen, Uingereza, pia walibaini kwamba waathiriwa wa mafuriko hupoteza uzani, hupatwa na presha ya damu, matatizo ya ubongo na wengine hujitosa katika ubugiaji wa pombe.

Kwa muda wa miaka mitatu, watafiti kutoka chuoni hapo walichunguza waathiriwa 300 wa mafuriko yaliyotokea kati ya 2015 na 2016 mashariki mwa Scotland kwa kipindi cha miezi 41.

“Utafiti huo ni wa kwanza kuonyesha madhara ya muda mrefu yanayosababishwa na mafuriko kwa waathiriwa,” akasema Dkt Mags Currie wa Chuo Kikuu cha Aberdeen aliyeongoza watafiti hao.

Baadhi ya waathiriwa walisema kuwa walipatwa na kikohozi kisichopona. Baadhi walianza kuwa na presha ya damu baada ya mkasa wa mafuriko.

“Kumekuwa na itikadi kwamba baada ya waathiriwa kujengewa nyumba na kutibiwa majeraha, hali huwa ni shwari na wanaweza kuendelea na maisha yao ya kawaida kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini utafiti wetu umedhihirisha kuwa waathiriwa tuliowahusisha wangali wana matatizo mbalimbali ya kiafya takribani miezi 43 baada ya mafuriko,” akasema Dkt Currie.

Utafiti huo pia ulibaini kwamba baadhi ya jamaa na majirani za waathiriwa wa mafuriko pia walikumbwa na matatizo ya msongo wa mawazo.

Januari 2020 serikali ya Uingereza ilianzisha kampeni ya kuwahamasisha raia wake kuhusu athari za mafuriko na kuwataka kujiandaa kimawazo.

Kulingana na taarifa ya serikali iliyotiwa katika tovuti rasmi www.gov.uk, asilimia 50 ya waathiriwa wa mafuriko hupatwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ambayo huwasumbua kwa zaidi ya miaka miwili baada ya mkasa.

“Msongo wa mawazo hutokea kwa sababu waathiriwa hupoteza wapendwa wao, mali na vitu vinginevyo vya thamani. Kugura makazi yao kwa kuhofia mafuriko pia huwasababishia msongo wa mawazo kwa muda mrefu,” ikasema taarifa hiyo.

“Kujiandaa kwa ajili ya mafuriko kunasaidia kupunguza hasara na msongo wa mawazo kwa asilimia 40,” inaongezea.

Maradhi mengine yanayohusishwa na mafuriko ni kipindupindu, malaria, ‘leptospirosis’, mafua, homa ya matumbo (taifodi) kati ya mengineyo.

Kipindupindu husababishwa na mtu kula chakula au maji yaliyo na viini vinavyojulikana kama ‘Vibrio cholerae’, ambavyo hupatikana kwenye kinyesi.

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na viini vinavyojulikana kama ‘Plasmodium’ na husambazwa na mbu jike aina ya Anopheles. Mbu anapouma mtu huachilia viini hivyo ambavyo huingia kwenye damu.

Wataalamu wanashauri kuwa wakazi wa maeneo yaliyo na visa vingi vya malaria kama vile Pwani, Nyanza na Magharibi watumie vyandarua kuepuka kupatwa na maradhi hayo.

‘Leptospirosis’ husababishwa na mafuriko haswa watu wanapotumia maji yaliyo na mkojo au kinyesi cha wanyama, haswa panya, walioambukizwa maradhi hayo.

Mafua (Influenza au flu) ni ugonjwa ambao husababishwa na virusi vinavyolenga mfumo wa upumuaji. Ugonjwa wa taifodi husababishwa na viini vinavyojulikana kama ‘Salmonella Typhi’, ambavyo huenezwa kwa kula chakula kilichochanganyikana na mkojo au kinyesi cha binadamu.