Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Magari na ndege zinazotumia umeme kuteka mwaka 2020

December 31st, 2019 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

IKIWA wewe hupendelea kusafiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba huenda ukaabiri ndege au gari lisilotumia mafuta kabla ya Desemba 2020.

Watengenezaji wa magari katika mataifa ya Ulaya wanasema kuwa mwaka wa 2020 utakuwa na idadi kubwa ya magari yanayotumia kawi ya umeme badala ya mafuta.

Hii ni katika juhudi za kupunguza moshi angani unaosababisha ongezeko la joto duniani.

Kuongezeka kwa joto duniani kunasababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huleta mvua kupita kiasi yenye mafuriko na vimbunga au ukame kupindukia.

Ripoti iliyotolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) inaonyesha kuwa joto limeongezeka hadi digrii 1.1 ikilinganishwa na miaka ya zamani ambapo hakukuwa na viwanda.

Mpango wa serikali kuhusu nanma ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi (NAP) unaonyesha kuwa kuongezeka kwa joto hadi digrii 2 kutasababisha Kaunti ya Mombasa pamoja na asilimia 30 ya maeneo mengineyo ya Pwani kuzama.

Serikali ya Kenya, Juni mwaka huu, ilitangaza kuwa magari yanayotumia umeme yanayobeba zaidi ya watu 10 yatapunguziwa ushuru kwa asilimia 50.

Miezi miwili iliyopita, washikadau mbalimbali katika sekta ya uchukuzi na wawekezaji katika kawi walikutana jijini Nairobi kujadili mikakati ya kuingiza humu nchini magari yasiyotumia mafuta.

Asilimia 25 ya fedha zinazotokana na matatu au teksi hutumika katika kununua mafuta.

Gari linalotumia umeme linasafiri umbali wa kilomita 150 kabla ya kuhitaji kuchajiwa tena.

Ikiwa umewahi kuabiri teksi inayofahamika kama Nopi, basi umechangia katika juhudi za kupambana na uchafuzi wa anga kwa moshi.

Gari la Nopi lilizinduliwa mnamo Agosti 2018 na kampuni ya EkoRent ya nchini Finland.

Kufikia sasa, kampuni hiyo imetengeneza vituo vitatu vya kuchaji magari yake. Vituo vya kuchaji magari hayo vipo katika majumba ya kibiashara ya Two Rivers Mall, The Hub, Karen na Thika Road Mall, jijini Nairobi.

Magari yanayotumiwa kwa sasa nchini Kenya yanatumia mafuta ambayo huchangia katika uchafuaji wa anga.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa gesi chafu ya kabon-dayoksaidi (CO2) inayotolewa na sekta ya uchukuzi imeongezeka maradufu jijini Nairobi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Lakini, katika ahadi yake kwa Umoja wa Mataifa (UN), Kenya inalenga kupunguza uchafuaji wa anga kwa asilimia 30 kufikia 2030.

Wawekezaji katika sekta ya uchukuzi wanataka serikali kuondolea ushuru magari yanayotumia umeme ili kuwezesha idadi kubwa ya Wakenya kuyakumbatia na kuachana na magari ya mafuta.

Kulingana na mtandao wa The Guardian, kufikia mwishoni mwa 2020, aina ya magari yatakayokuwa yakitumia umeme itafikia 175. Inakadiriwa kuwa kufikia 2025, aina 330 ya magari yatakuwa ya umeme.

Nchini Uingereza, mauzo ya magari yasiyotumia petroli yanatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 5.5 mwaka kesho ikilinganishwa na 3.4 mwaka huu.

Takwimu zinaonyesha kuwa magari 80,000 yasiyotumia umeme yaliuzwa nchini Uingereza mwaka huu na magari 131,000 yanatarajiwa kuuzwa 2020.

Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU), kuanzia Januari mwaka ujao, utatoza faini kampuni ambazo magari yake yatatoa zaidi ya gramu 95 ya moshi kwa kila kilomita.

Kampuni ambazo magari yake yatapitisha kiwango hicho zitatozwa faini ya Sh11,000 kwa kila gramu ya moshi. Hiyo inamaanisha kwamba kampuni za kutengeneza magari sasa zitalazimika kukumbatia magari yanayotumia umeme kuepuka adhabu hiyo.

Sekta ya usafiri huchangia asilimia 15 ya gesi chafu zinazosababisha joto duniani.

Huku soko la magari ya umeme likikadiriwa kupanuka, mapema mwezi huu, ndege isiyotumia mafuta ilifanyiwa majaribio jijini Vancouver, Canada.

Ndege hiyo ilitengenezwa na kampuni ya MagniX kwa ushirikiano na kampuni ya ndege ya Harbour Air, na husafirisha abiria takribani nusu milioni kwa mwaka kati ya Vancouver na visiwa vilivyoko karibu.

Ripoti ya UN iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha kuwa gesi chafu inayotolewa na ndege imeongezeka kwa asilimia 70 kufikia mwaka jana ikilinganishwa na 2013.

Abiria mmoja anaposafiri kilomita moja kwa ndege, huchangia gramu 285 za gesi ya CO2. Hiyo inaamaanisha kwamba ikiwa ndege ina abiria 40, gesi itakayotolewa kwa kila kilomita ni kilogramu 11 za CO2.

Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria sita imezua matumaini kwamba kufikia mwisho wa 2020 ndege kadhaa zitakuwa zinatumia umeme badala ya mafuta.

Ndege hiyo iliruka kwa dakika 15.

Wataalamu wanasema kuwa mbali na kuhifadhi mazingira, ndege zinazotumia umeme, zinahitaji gharama ya chini kukarabati.

Kampuni ya Harbour Air, hata hivyo, itasubiri kwa miaka miwili kabla ya kupewa idhini ya kuzindua ndege zake zaidi ya 40 zitakazotumia umeme badala ya mafuta.