Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Matumaini huenda dawa ya Ebola ikatumika kukabiliana na homa ya Corona

March 3rd, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANASAYANSI sasa wameweka matumaini yao kwa dawa ya Ebola katika kukabiliana na homa ya Corona.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Alberta cha nchini Canada sasa wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba dawa ya Ebola huenda ikatibu homa ya Corona.

Wanasayansi hao wanasema kuwa dawa ya Ebola inayofahamika kama remdesivir, ina uwezo wa kutibu maradhi mengine yenye asili sawa na virusi vya Corona.

Maradhi yenye virusi vinavyofanana na Corona na huathiri mfumo wa kupumua ni Ebola, Middle East Respiratory Syndrome (MERS) na Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS).

Wanasayansi hao wanasema kuwa homa ya Corona ina uhusiano wa karibu na MERS na SARS hivyo kuna uwezekano kwamba ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,800 kote duniani, hasa nchini China, unaweza kutibiwa kwa kutumia dawa ya remdesivir.

Maradhi ya MERS yaliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Saudi Arabia mnamo 2012 kabla ya kusambaa katika mataifa mengineyo duniani. Dalili za ugonjwa huo ni joto jingi mwilini, kikohozi na kupungukiwa pumzi.

Maradhi ya MERS yanaambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu na miongoni mwa mifugo walio na uwezo wa kusambaza virusi vya ugonjwa huo ni ngamia.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa MERS uliambukiza watu 2,519 na kati yao 866 walifariki.

Maradhi ya SARS yalianzia nchini China mnamo 2002. Jumla ya watu 8,098 waliambukizwa virusi vya ugonjwa huo na 774 kati yao walifariki.

Sawa na homa ya Corona, wengi wa waathiriwa waliofariki kutokana na SARS walikuwa watu wa umri wa juu.

Ripoti ya pamoja ya WHO na wataalamu wa nchini China inaonyesha kuwa kati ya watu zaidi ya 88,000 walioambukizwa virusi vya Corona, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ni asilimia 2.4 pekee.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa wengi wa walioathiriwa ni watu wa umri wa miaka 40 na zaidi na wagonjwa ambao kinga zao za mwili ni hafifu.

“Dawa ya remdesivir inatibu virusi vinavyosababisha maradhi ya MERS na SARS. Virusi vya Corona vinafanana na vile vinavyosababisha ugonjwa wa SARS. Hivyo ni sahihi kusema kuwa dawa ya remdesivir ina uwezo mkubwa wa kutibu homa ya Corona,” wanasema wanasayansi hao kupitia utafiti wao uliochapishwa katika jarida la Journal of Biological Chemistry.

Dawa ya remdesivir ilitengenezwa na kampuni ya Gilead Sciences ya nchini Amerika katika juhudi za kukabiliana na maradhi ya Ebola.

Chuo Kikuu cha Nebraska pia kimeanza majaribio kutathmini ikiwa dawa ya remdesivir inafaa kutumiwa kutibu homa ya Corona au la.

Mmoja wa wagonjwa wanaofanyiwa majaribio ya dawa hiyo na chuo hicho ni raia wa Amerika aliyeokolewa kutoka kwenye meli ya Diamond Princess iliyokumbwa na mkurupuko wa homa ya Corona ikitoka China kuelekea Japan.

Kampuni ya Gilead Sciences pia imeanza kufanyia majaribio dawa hiyo ambapo inahusisha wagonjwa 1,000 wa homa ya Corona nchini China.

Wagonjwa watakaoshiriki jaribio hilo, 400 watakuwa wale wako katika hali mahututi na wengine 600 watakuwa waathiriwa ambao hawajalemewa na maradhi hayo.

Wagonjwa wote watapewa dawa hivyo kwa siku 10 mfululizo.

Katika kongamano la hivi karibuni jijini Beijing, naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Bruce Alyward, alisema kuwa dawa ya remdesivir ndiyo dawa ya pekee ambayo kwa sasa inategemewa kukabiliana na homa ya Corona ( Covid-19).

“Utafiti wetu umebaini kuwa dawa ya remdesivir ina uwezo wa kuzuia virusi kuzaana. Inawezekana dawa hiyo pia inazuia virusi vya Corona kuongezeka,” wanasema watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Alberta.

Alisema kuwa taarifa kamili kuhusu ikiwa dawa ya remdesivir inaweza kutibu homa ya Corona itatolewa mwezi ujao baada ya kutathmini vipimo vya maabara kuhusu ufaafu wake.

“Kadhalika, kuna dalili kwamba huenda tukahitaji zaidi ya aina moja ya dawa kutibu homa ya Covid-19 sawa na virusi vya HIV na hepatitis C,” wanasema wanasayansi hao.

Kulingana na WHO, zaidi ya kinga 20 za maradhi ya Corona zinaendelea kufanyiwa uchunguzi kote duniani.

Ugonjwa wa Ebola unaaminika kutoka kwa wanyama kama vile popo, tumbiri, nyani au sokwe.

Virusi vya Corona pia vinaamika kutoka kwa popo au nyoka japo wanasayansi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kiini chake.

Mbali na remdesivir, watafiti pia wanasayansi nchini China na Thailand wameanza kufanyia majaribio dawa ya kupunguza makali ya virusi vya HIV (ARVs).