Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mazingira yenye miti kitulizo cha mawazo

September 24th, 2019 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

KWA kawaida madaktari hushauri wagonjwa kula matunda, mboga na kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Lakini sasa wamebaini tiba nyingine ambayo huenda ikasaidia watu kuboresha afya zao.

Utafiti uliofanywa nchini Uingereza umebaini kuwa kutembelea mazingira yenye mimea asili kama vile misitu, milima, mbuga za wanyamapori, kuna manufaa kiafya sawa na kula matunda au kufanya mazoezi.

Watafiti hao wanasema kutembea au kupumzika katika mazingira yenye mimea ya asili angalau kwa muda wa saa mbili kwa wiki ni tiba tosha ya kukuondolea mzongo wa mawazo na hata kufanya mwili wako kuhisi vyema.

Watafiti hao kutoka katika Chuo Kikuu cha Exeter, Uingereza walibaini kuwa mwili wa mtu anayetembea au kupumzika katika mazingira yaliyo na mimea ya asili kwa saa mbili kwa wiki anapata faida sawa na mwenzake ambaye anakula matunda matano kwa siku au anayefanya mazoezi kwa dakika 150 kwa wiki.

Watafiti hao walihoji watu 20,000 nchini Uingereza kuhusu shughuli walizokuwa wakifanya kuboresha afya yao.

Idadi kubwa ya watu waliosema kuwa hawajawahi kupanda mlima, kutembea katika mbuga za wanyama au misituni walidai kuwa walikuwa na mzongo wa mawazo pamoja na matatizo mengine ya kiafya.

Lakini asilimia 90 ya wenzao waliokuwa na mazoea ya kutembea kwenye mazingira yenye mimea asilia, walihisi vyema kiafya na hata walisema waliridhika na maisha yao.

Endapo tafiti zaidi zitafanywa na kuthibitisha hili, basi huenda kuzuru maeneo yenye miti, maua na mimea mingineyo ya asili ikawa miongoni mwa mambo ambayo madaktari watashauri wagonjwa wao kufanya bali na kula matunda, mboga na kufanya mazoezi.

“Faida za kuzuru mazingira yenye mimea ya asili ni sawa kwa wazee, vijana, maskini, matajiri, wanaoishi mijini au vijijini, watu wenye ulemavu, wagonjwa, na kadhalika,” akasema Dkt Mathew White wa Kitivo cha Matibabu katika Chuo Kikuu cha Exeter, Uingereza.

Faida tele

Kulingana na watafiti hao, hata kuketi tu katika mazingira yenye miti au maua kuna manufaa makubwa kiafya.

“Kutembea katika mazingira yenye mimea ya kiasili kunamfaa kila mtu na si lazima ufanye mazoezi, hata kuketi chini ukiangalia miti na maua kuna manufaa makubwa kwa afya,” akasema White.

Profesa Helen Stokes-Lampard, Mwenyekiti wa Chuo cha Afya cha Royal, Uingereza alisema, “Utafiti huu ni muhimu kwani utatia watu motisha wa kutoka nje na kwenda kutembea katika mazingira yaliyo na mimea ya kiasili kama vile misitu, mbuga za wanyama au fukwe za bahari zilizo na mimea ya asili.

Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika jarida la kisayansi; Scientific Reports.

Watafiti hao walisema kuna faida tele mtu anapotangamana na mazingira ya kiasili kwa zaidi ya saa mbili.

“Tulishangazwa mno na faida nyingi za kiafya zinazoletwa na mazingira ya kiasili. Kupumzika katika maeneo yenye miti, maua na mimea mingineyo kunaboresha hali ya kiafya sawa na mazoezi au kula matunda na mboga,” akasema White.

Wanasayansi hao, hata hivyo, wangali hawajabaini kinachosababisha mazingira ya asili kuboresha afya.

Lakini wanaamini kuwa mtu anapoketi kwenye mazingira yaliyo na miti, hupata utulivu wa akili ambao huwa na manufaa kiafya.

“Watu wengi huwa na mzongo wa mawazo. Unapoenda kuzuru maeneo yaliyo na miti, maua na mimea mingineyo ya kiasili, mwili hutulia na kivyo kukufanya kutuliza mawazo,” anasema White.

“Katika utafiti huo, tumebaini kuwa mazingira ya kupendeza kwa mfano yaliyo na maua ya kuvutia, yanatuliza mawazo,” akaongezea.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Derby cha Uingereza kwa ushirikiano na shirika la The Wildlife Trusts mnamo 2016, ulipata matokeo sawa.

Chuo hicho kilianzisha zoezi lililojulikana kama ‘30 Days Wild’ ambapo washiriki 18,500 walitakiwa kwenda misituni kutazama au kucheza na maua, miti, ndege, wadudu na hata wanyama kwa muda wa siku 30.

Baada ya siku 30, idadi kubwa walisema kuwa walikuwa wenye furaha na walihisi hali yao ya afya iliimarika.

Watoto walioshiriki utafiti huo walisema kuwa walihisi kuwa jasiri.

Watafiti walioendesha utafiti huo walisema watoto wanapotangamana na mazingira, wanakuwa wasikivu zaidi darasani.

Dkt Miles Richardson mtaalamu wa afya ya akili Chuoni Derby aliyeongoza utafiti huo, alisema watu walio na matatizo ya mzongo wa mawazo wanaweza kupona haraka wanapozuru mazingira yaliyo na mimea ya kiasili.

“Unapoenda misituni kutazama maua, wanyama au maua kwa muda mrefu unakuwa na afya njema na mwenye furaha,” akasema Richardson.

Kulingana na Dkt Richardson, kuna ushahidi wa kutosha kuwa kutangamana na mazingira kunapunguza maradhi ya shinikizo ya damu, moyo na kupumua.

“Watu wanaopendelea kutembelea mazingira asili wanakuwa wasikivu, wenye furaha na hufurahia maisha zaidi ikilinganishwa na wenzao ambao hutumia mrefu wakiwa nyumbani,” akasema.

Utafiti mwingine uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan, Amerika, pia ulibaini kuwa kutembea katika mazingira yaliyo na miti mingi, wadudu, wanyama au maua kunapunguza kiwango cha homoni ambazo husababisha mzongo wa kiakili.

Watu walioshiriki katika utafiti huo, walitakiwa kwenda katika mazingira yaliyo na miti na kucheza na maua, wanyama, wadudu au ndege kwa angalau dakika 10 mara tatu kwa wiki.

Kabla ya kuanza utafiti huo, mate ya washiriki yalipimwa kubaini kiwango cha homoni za ‘cortisol’ ambazo husababisha mzongo wa kiakili.

Baada ya miezi minane, ilibainika kuwa kiwango cha homoni hizo kilipungua kwa kiasi kikubwa katika mate ya washiriki.