MAZINGIRA NA SAYANSI: Mombasa hatarini kuzama baharini, wataalamu waonya

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mombasa hatarini kuzama baharini, wataalamu waonya

Na LEONARD ONYANGO

JIJI la Mombasa huenda likazama baharini ndani ya kupindi cha miaka 30 ijayo, wanasayansi wameonya.

Utafiti uliofanywa na shirika la Climate Central la nchini Amerika, miji iliyoko karibu na bahari kote duniani, ikiwemo Mombasa, Lamu na maeneo mengineyo yaliyo karibu na Bahari ya Hindi yatazama majini endapo joto litaendelea kuongezeka hadi mwaka wa 2050.

Serikali ya Kenya inakadiria kuwa watu 267,000 katika maeneo yaliyoko karibu na Bahari Hindi wataathiriwa na mafuriko yatakayosababishwa na ongezeko la maji baharini kufikia 2030.

“Ongezeko la maji baharini kwa sentimita 30 linaweza kusababisha asilimia 17 ya maeneo ya Pwani kuzama,” unasema mpango wa Kenya kuhusu jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (NCCAP) 2018-2022.

“Kenya ina ufukwe wa urefu wa kilomita 1,420 na iwapo maji ya baharini yataongezeka basi eneo la kati ya kilomita 4 na 7 kutoka ufukweni litamezwa na maji.

“Kaunti ya Mombasa ndiyo iko kwenye hatari zaidi,” unaongezea mpango huo.

Mpango huo wa serikali unakadiria kuwa iwapo maji ya bahari yataongezeka, Kenya itapata hasara ya zaidi ya Sh50 bilioni.

Ripoti ya Climate Central inakadiria kuwa watu milioni 110 kote duniani wanaishi katika maeneo yaliyo hatari ya kusombwa na mafuriko endapo kiwango cha maji baharini kitaongezeka.

Benki ya Dunia nayo inasema zaidi ya watu milioni 10 katika mataifa ya Afrika Mashariki (Kenya na Tanzania) watalazimika kuhama makao yao kutokana na ongezeko la maji katika Bahari ya Hindi kufikia 2050.

Jiji la Dar-es-Salaam, Tanzania, kwa mfano lina wakazi milioni tano wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kumezwa na maji ya bahari.

Hiyo inamaanisha kwamba katika miaka michache ijayo hakutakuwa na fukwe za watu kuvinjari kwani zitakuwa zimemezwa na maji.

Mwaka jana, Shirika la Kusimamia Makavazi ya Kitaifa (NMK) lililalama kwamba eneo la Fort Jesus, ambalo linatambuliwa na Shirika la Kimataifa kuhusu Utamaduni (Unesco) kuwa eneo maalumu la kihistoria duniani, huenda likaharibiwa na mawimbi makali ya baharini kutokana na ongezeko la maji.

Mnara wa Fort Jesus uko katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Kisiwa cha Mombasa karibu na bandari ya zamani ya Mombasa.

Ripoti ya Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN Habitat) ya 2010 ilidokeza kwamba fukwe za kuvinjari, maeneo ya kihistoria, mahoteli, viwanda na hata bandari zitaathiriwa kutokana na ongezeko la maji ya baharini.

Ripoti ya Baraza la Kushughulikia Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa (IPCC) ya 2013 ilitabiri kwamba jiji la Mombasa na miji mingineyo iliyoko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi yatatoweka kufikia 2080.

Benki ya Dunia inasema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mafuriko katika maeneo ya Pwani ishara kwamba yataathiriwa pakubwa kutokana na ongezeko la maji ya baharini kufikia 2050.

Watafiti hao wanatabiri kuwa eneo la Kusini mwa Vietnam litafunikwa na bahari na kutoweka.

Watu zaidi ya milioni 20, ambao ni sawa na asilimia 25 ya watu Vietnam, wanaishi katika maeneo yanayotishiwa kumezwa na maji ya baharini.

Mji wa Ho Chi Minh ambao ni kitovu cha uchumi nchini Vietnam, utazama baharini, kulingana na ripoti ya watafiti hao iliyochapishwa katika jarida la Nature Communications.

Nchini Thailand, zaidi ya asilimia 10 ya raia wake wanaishi katika maeneo ambayo huenda yakaathiriwa na ongezeko la maji ya baharini.Jiji la Shanghai nchini China na Mumbai (India) pia huenda yakatoweka kwa kumezwa na maji ya baharini, kulingana na ripoti ya Climate Central.

Eneo la kitamaduni la Alexandria la nchini Misri pia litamezwa na maji, kwa mujibu wa watafiti hao.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa mji wa Basra ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Iraq, pia hautakuwepo kufikia 2050.

Ujenzi wa kuta na matuta

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UN Environment), serikali ya Tanzania imeanzisha juhudi za kujenga kuta na matuta ya kuzuia maji ya baharini kudhuru watu wanaoishi katika ufukwe wake wenye urefu wa mita 2,400.

UN pia inasema kwamba inashirikiana na serikali ya Tanzania kujennga mitaro ya kuhakikisha kuwa maji ya mafuriko yanaingia baharini bila kusababisha uharibifu.

Je, ni nini kinasababisha maji ya baharini kuongezeka?

IPCC inakadiria kuwa maji ya baharini yameongezeka kwa kati ya milimita 180 na 200 ikilinganishwa na miaka ya 1800 kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Maji ya baharini yanaongezeka kutokana na sababu mbalimbali kati yazo ikiwa kuyeyuka kwa barafu iliyoko katika milima.

Karibu asilimia 80 ya barafu iliyokuwa katika kilele cha Mlima Kenya imeyeyuka.

Mlima Kenya ndicho chanzo cha mito mbalimbali ukiwemo Mto Tana. Barafu iliyoko kwenye milima inapoyeyuka huishia kwenye mito na kuingia baharini hivyo kusababisha maji kuongezeka.

Ongezeko la joto duniani pia linasababisha maji ya baharini kuongezeka. Inakadiriwa kuwa joto limechangia maji kuongezeka kwa milimita 19.

You can share this post!

TEKNOHAMA: Simu, TV hudumaza ubongo wa watoto wachanga...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Tafadhali fafanua ‘siku...

adminleo