Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Vifaa vya kielektroniki vina sumu hatari

August 20th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANARIADHA 11,090 kutoka nchi 206, ikiwemo Kenya, wanaendelea na maandalizi motomoto kwa ajili ya makala ya 2020 ya mashindano ya mbio za Olimpiki yatakayofanyika jijini Tokyo, Japan.

Mashindano hayo yatang’oa nanga Julai 24 na kumalizika Agosti 9.

Wanariadha wa Kenya ambao kwa kawaida hutia fora katika mbio, watakita kambi katika jiji la Kurume, kulingana na Kamati ya Olimpiki nchini (NOC-K).

Katika makala ya 2016 yaliyofanyika jijini Rio de Janeiro, Brazil, Kenya iliibuka katika nafasi ya 15 baada ya kupata nishani sita za dhahabu, nishani sita za fedha na nishani moja ya shaba.

Tofauti na mashindano ya 2016, makala ya mwaka ujao, washindi watatuzwa nishani zilizotengenezwa kwa simu kuukuu.

Kulingana na kamati andalizi, nishani za dhahabu, fedha na shaba zimetengenezwa kwa madini yaliyotolewa katika simu milioni sita zilizoharibika.

Kamati ya maandalizi ya mashindano ya Olimpiki makala ya 2020 ilitangaza azma yake ya kutaka kutengeneza nishani kutokana na simu zilizoharibika mnamo 2017.

Baadaye ilikusanya simu zilizoharibika nchini Japan hadi Machi 2019.

Kulingana na mtandao wa USA Today, serikali ya Japan ilifanikiwa kukusanya tani 80,000 ya vifaa vilivyoharibika vya kielektroniki, zikiwemo simu milioni 6.21.

Wanakandarasi walifanikiwa kupata kilo 31 za dhahabu, kilo 3.5 za fedha na kilo 2200 za shaba kutoka kwa vifaa hivyo vya kielektroniki.

Hatua hiyo ya kamati ya Olimpiki ni habari njema kwa wanaharakati wa utunzaji wa mazingira.

Kenya ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya vifaa vya kielektroniki kama vile simu, televisheni, kompyuta, kamera, na kadhalika.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), vifaa hivyo vinapoharibika na kutupwa kiholela, ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu na wanyama.

Uchafu unaotokana na vifaa vya kielektroniki zikiwemo simu, umesheheni sumu hatari ambayo huathiri kila kiungo cha mwili. Baadhi ya maradhi yanayosababishwa na sumu inayopatikana katika vifaa vya kielektroniki vilivyoharibika ni kansa, shinikizo la damu, maradhi ya mapafu, ini, figo kati ya magonjwa mengineyo.

Sumu inayotoka kwenye vifaa hivyo pia huchafua hewa na maji hivyo, kuathiri wanyama na viumbe wa majini, kulingana na WHO.

Sumu hiyo pia huathiri udongo na hata kupunguza uzalishaji wa mazao.

Shirika la WHO pia linaonya kuwa mafundi wanaotengeneza vifaa vya kielektroniki pia wako katika hatari ya kupumua hewa chafu yenye sumu.

Samwel Matonda, Mwanakemia na Mkurugenzi wa Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa, anaonya kuwa vifaa vingi vya kieletroniki vimetengenezwa kwa kemikali ambazo ni hatari kwa mazingira na afya haswa zinapoingia ndani ya vyanzo vya maji. “Kemikali hizo na chembechembe za vyuma zinaweza kusababisha maradhi ya kansa na hata ugonjwa wa ngozi. Kemikali hizo zinapoingia ndani ya mito, zinaweka hatarini afya ya wanyama, samaki na viumbe wengineo,” anasema Bw Matonda.

Kuteketeza

Wataalamu pia wanaonya kuwa kuchoma vifaa vya kielektroniki ni hatari zaidi kwani vinatoa hewa chafu ambayo huenda ikadhuru afya.

Tofauti na nchi zilizostawi kiuchumi zilizo na utaratibu wa kukusanya vifaa vya kielektroniki vilivyoharibika na kuvitumia kutengeneza vitu vinginevyo, Kenya haina hata sheria au mwongozo kuhusu utupaji wa vifaa hivyo.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Unep) mnamo 2014, ulibaini kuwa Wakenya hutupa kiholela tani 44,000 za vifaa vya kielektroniki kila mwaka.

Wanaharakati wa mazingira wanasema kuwa ongezeko la vifaa vya kunasa kawi ya jua, maarufu kama sola, pia huenda kukasababisha kuongezeka kwa uchafu wa vifaa vya kielektroniki ndani ya miaka 10 ijayo.