Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Vitu vinavyoweza kuleta virusi vya corona nyumbani

March 24th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

VIRUSI vya corona vinaenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kusalimiana kwa mikono, kugusana na kuwa karibu na mwathiriwa anapochemua au kukohoa.

Wataalamu pia wanasema kuwa virusi hivyo vinaenezwa kupitia vitu kama vile simu, nguo na wageni.

Kwa mfano, unaposhikwa kwenye nguo na mwathiriwa wa virusi vya corona kwenye matatu na kisha ukifika nyumbani watoto waguse katika eneo hilo na waweke mkono kwenye mdomo au puani, wanakuwa katika hatari ya kuambukizwa viini vya maradhi hayo.

Wageni

Ukitembelewa na mwathiriwa wa corona nyumbani, kuna uwezekano mkubwa kwamba familia nzima huenda ikawa katika hatari ya kuambukizwa.

Unapotembelewa na mgeni wakati huu ambapo maradhi haya yanaenea kwa kasi, wataalamu wanashauri kuwa ukae mbali naye.

Hakikisha kuwa vitu vyote vinavyoguswa na mgeni kama vile rimoti ya televisheni, sahani, vijiko, vikombe au kiti vinasafishwa kwa maji na sabuni au dawa ya kuua viini baada ya mgeni kuondoka, kabla ya kuanza kuvitumia.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa virusi hivi vinaweza kukaa hewani kwa saa nne mwathiriwa anapokohoa au kupiga chafya.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa virusi hivyo vinaweza kuishi nje ya mwili kwenye vitu vigumu kama vile viti, nguo au simu kwa muda wa hadi siku tisa.

Wakati wa kusafisha vitu vilivyoguswa na mgeni, epuka kugusa pua mdomo au macho.

Sahani, vijiko au visu vinaweza kusafishwa kwa kutumia maji moto na sabuni.

Nguo

Kadhalika wataalamu wanaamini kuwa muda ambao virusi hivi vinaishi kwenye nguo unategemea aina ya nyuzi zilizotumika kutengeza.

Robert Amler ambaye ni Mkuu wa Kitivo cha Matibabu katika Chuo cha New York, Amerika alinukuliwa na mtandao wa HuffPost akisema kuwa virusi vinakaa kwa muda mfupi katika nguo zilizotengenezwa kwa pamba (cotton) ikilinganishwa na zile zilizotengenezwa kwa ‘polyester’.

“Nguo iliyotengenezwa kwa pamba hupitisha hewa hivyo hufanya virusi au bakteria kukauka haraka na kufa. Kadhalika, vinakuwa kwa muda mfupi kwenye nguo laini za kuteleza kama vile majaketi ya mvua,”anasema Amler.

Nguo zilizotengenewa kwa ‘polyester’, zinashikilia viini kwa muda mrefu, kulingana na mtaalamu huyo wa afya.

“Kwa ufupi ni kwamba aina zote za nguo zinaweza kusambaza virusi vya corona kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Hivyo hatua za usafi zinafaa kuzingatiwa,” anasema.

Wataalamu wanashauri kwamba uvue nguo na kuzitenga mara tu baada ya kuwasili nyumbani na kisha unawe mikono kabla ya kuanza kutangamana na watu wengine nyumbani.

Wataalamu wa afya wanashauri kuwa nguo hizo zifuliwe mara moja badala ya kuzirundika kwenye nguo chafu.

Je, maji yanaweza kueneza virusi vya corona nyumbani?

Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema kuwa hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba virusi vya corona vinaweza kuenezwa kupitia maji ya kunywa.

Kadhalika, WHO inasisitiza kuwa hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa virusi vya corona vinaweza kusambazwa kupitia maji machafu ya mtaroni.

“Maji ya kunywa ya mifereji hutibiwa hivyo hakuna uwezekano wa kuwa na virusi vya corona,” linasema shirika la WHO.

Shirika hilo linasema kuwa kuchemsha maji ya kunywa ni muhimu katika kukabiliana na maambukuzi ya bakteria wengineo lakini si njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini wataalamu wanaonya kuwa maeneo yasiyokuwa na maji safi ya kunawa ni hatari kwa wakazi kwani huenda virusi vya corona vikaendelea kusambaa kwa kasi licha yao kusafisha mikono.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) mnamo 2017 ilionyesha kuwa asilimia 40 ya kaya, hazina maji safi ya kunywa na kufanyia matumizi mengine kama vile kunawa, kuosha vyombo na hata kunywesha mifugo.

Waathiriwa wa corona wanafaa kufanya nini nyumbani?

Ikiwa wewe ndiye umeathiriwa na virusi vya corona wataalamu wanashauri kwamba usitoke nyumbani kwenda kutembelea jamaa zako, kwenda kanisani au kazini. Jitenge nyumbani na usitangamane na watu wa familia yako.

Unapokuwa umejitenga, hakikisha kuwa unapumzika vyema na kunywa maji ya kutosha.

Wataalamu wanasema kuwa maji ni muhimu kwa mwili lakini hayaui virusi vya corona kama ambavyo imekuwa ikidaiwa katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya watu wamekuwa wakishauri watu kunywa maji kila baada ya dakika 15 kama njia mojawapo ya kukabiliana na virusi vya corona.

Habari hizo za kupotosha zimekuwa zikidai kuwa maji yanaweza kusukuma virusi kutoka kooni hadi tumboni ambapo vinauawa na asidi.

Lakini wataalamu wanasema kuwa asidi iliyo tumboni haina makali ya kuua virusi vya corona.

Wataalamu wanashauri kuwa usiruhusu watu wengine kutumia vifaa vyako vya kibinafsi kama vile nguo, shuka za kitandani, taulo, sahani na vifaa vinginevyo vya kutumia mezani.

 

Ikiwa dalili zitaendelea, pigia simu maafisa wa afya kupitia 719 au 0729471414 au 0732353535.