Makala

Mazingira safi yatasaidia kudhibiti maradhi ya kansa

May 2nd, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

VISA vya maradhi ya saratani vimeendelea kuripotiwa nchini huku idadi ya waliougua ugonjwa huo au walioathiriwa ikiendelea kuongezeka kila siku.

Idadi ya Wakenya ambao huaga dunia kwa sababu ya kansa ni 32,987, kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na mataifa mengine Afrika Mashariki.

Kansa nchini imekuwa ni janga la kitaifa na ingawa haijaitangazwa janga, ukweli ni kwamba wananchi wanahisi uzito wa ugonjwa huo.

Kumekuwa na nadharia tofauti kuhusiana na kiini cha ongezeko la kansa nchini. Baadhi ya saratani ni za kurithi, zingine zinatokana na mitindo ya maisha ya watu na zingine zinaaminika kutokana na kemikali ndani ya vyakula au baadhi ya bidhaa ambazo watu wanatumia.

Lakini kuna suala ambalo linaweza kuwa kiini kikuu cha saratani – mazingira chafu.

Kwa mfano, uchafuaji wa vyanzo vya maji kwa kemikali sumu kutoka kwa kampuni nchini unaweza kuwa sababu kubwa baadhi ya watu wana kansa nchini.

Tukiangalia baadhi ya maeneo nchini, ukweli ni kwamba maji ambayo hutumiwa na watu wengi sio safi.

Mto Athi, ambao hutumiwa na watu kutoka takriban kaunti 10, ni moja ya mito iliyochafuliwa zaidi. Baadhi ya kampuni Nairobi, Machakos na Kiambu huachilia maji chafu yenye kemikali kuingiliana na mikondo ya maji.

Zaidi, mitaa ya mabanda kando ya mito, hasa Nairobi, Machakos na Kiambu ni kiini kikubwa cha maji chafu ambayo humiminika mtoni humo. Maelfu ya watu hutumia maji hayo kwa kilimo, kunywesha mifugo wao au hata kutumia nyumbani.

Kutokana na hilo, ukweli ni kwamba watu wanakula kemikali moja kwa moja katika nyama, mboga au mazao mengine ya shambani, au hata kuinywa ndani ya maji bila kujua.

Zaidi, hewa pia imechafuliwa na baadhi ya mvuke wa kemikali zitumiwazo na baadhi ya kampuni kutengeneza bidhaa.

Ni kutokana na hayo ambapo visa vya kansa vinazidi kuongezeka nchini. Hii ni kumaanisha kuwa, ikiwa tunataka kukabiliana na kansa, lazima kwanza tusafishe mazingira yetu.

Mazingira safi ndio msingi wa afya bora. Hata hivyo kwa kuangalia tu, baadhi ya maeneo hasa mijini yamejawa na takataka, ambazo pia kwa kiwango kikubwa huwa na kemikali mbaya ambazo huathiri wananchi kiafya.

La sivyo, wananchi, watoto kwa wakubwa, matajiri kwa maskini, watazidi kuangamizwa na kansa zinazoweza kukabiliwa.Mzigo wa matibabu kwa wanaougua au kuathiriwa na ugonjwa huo ni mkubwa na mzito mno.

Ingawa kumekuwa na kampeni nyingi kuhusu usafi wa mazingira, ni wakati wa serikali kuchukua hatua dhabiti kuhakikisha kuwa mazingira ni safi, kwanza kabisa kwa kuhakikisha kuwa kampuni zinafuata sheria za mazingira na haki za wananchi.

Pili, serikali inahitaji kutengeneza mfumo mzuri ambapo takataka kama vile karatasi, chupa na kadhalika, zitaweza kutumika up, badala ya kusambaa kila mahali na kuathiri afya ya wananchi.