MakalaSiasa

Mazishi ya Moi yanavyozidi kusambaratisha uhusiano wa Uhuru na Ruto

February 9th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KUTENGWA kwa Naibu wa Rais William Ruto katika mipango ya mazishi ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi kumedhihirisha ufa serikalini.

Wadadisi wanasema kuwa kutengwa kwa Naibu wa Rais katika mipango hiyo pia kumedhihirisha uhasama wa kisiasa baina ya Dkt Ruto na familia ya Mzee Moi.

Mara baada ya kifo cha Rais Mstaafu kutangazwa Jumanne alfajiri, waziri wa Usalama Fred Matiang’i alisema kwamba aliagizwa na Rais Kenyatta kuunda kamati ya kuandaa mazishi ya kitaifa.

Rais Kenyatta alikuwa ziarani nchini Amerika na kulingana na Katiba, Dkt Ruto ndiye alifaa kuendesha mipango ya mazishi akiwa Naibu wa Rais.

Dkt Ruto aliyeonekana kutengwa, Jumanne, alihutubia kikao cha wanahabari ambapo alisema kuwa ilikuwa risala za rambirambi za serikali kwa familia ya Mzee Moi.

Dkt Ruto alipokuwa akihutubia wanahabari, Dkt Matiang’i, Mkuu wa Majeshi Jenerali Samson Mwathethe, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho walikuwa wakiendelea na shughuli ya kuunda kamati ya mazishi.

Baada ya hotuba, alielekea katika hifadhi ya maiti ya Lee Funeral Home ambapo alizuiliwa kutazama mwili wa Mzee Moi.

Dkt Ruto aliyeonekana mwenye hasira, alifunga safari na kuelekea katika Kaunti ya Kakamega kufariji wazazi wa watoto 14 waliofariki katika mkanyagano katika Shule ya Msingi ya Kakamega.

Alipotoka Kakamega, Dkt Ruto alifululiza hadi nyumbani kwa Mzee Moi katika eneo la Kabarnet Gardens jijini Nairobi ambapo alilakiwa na wana wa rais wa pili wa Kenya; Seneta wa Baringo Gideon Moi na mbunge wa Rongai Raymond Moi.

“Mzee Moi alikuwa shujaa. Tumepoteza kiongozi shupavu na baba yetu. Serikali ya Kenya imesimama na familia ya Moi wakati huo wa majonzi,” akasema Dkt Ruto katika hotiba yake.

Dkt Ruto alimpongeza Mzee Moi kwa kukubali kuachilia mamlaka mnamo 2002 kwa amani na kumkabidhi Rais Mwai Kibaki.

Kauli hiyo imefasiliwa na baadhi ya wadadisi wa kisiasa kuwa huenda alimwelekezea Rais Kenyatta ambaye mrengo wa Tangatanga umekuwa ukidai kuwa anapanga njama ya kusalia mamlakani kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Wanasiasa wa kundi la Tangatanga ambalo linaunga mkono harakati za Dkt Ruto kuwania urais 2022, wamekuwa wakidai kuwa Rais Kenyatta analenga kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu kupitia BBI ili kuendelea kusalia mamlakani licha ya kukamilisha muhula wake wa pili.

Mgawanyiko baina ya Rais Kenyatta na naibu wake Dkt Ruto umedhihirika wazi katika siku za hivi karibuni.

Wiki mbili zilizopita, Rais Kenyatta, kupitia lugha ya mafumbo, alionekana kumzima Dkt Ruto kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo ya serikali.

Rais Kenyatta alipokuwa katika eneo la Kinangop alisema kuwa ‘mafisi’ aliowatuma kukagua miradi ya serikali sasa wanaitumia kujitafutia umaarufu wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Rais Kenyatta alisema sasa atakuwa akizunguka mwenyewe kukagua miradi hiyo.Lakini siku mbili baadaye, Dkt Ruto alimjibu akisema kuwa atendelea kukagua miradi ya maendeleo ‘kwani hiyo ndiyo kazi ninalipwa mshahara na Wakenya kufanya’.

Lakini Wakili Felix Odhiambo anasema kuwa huenda agizo la kumzuia Dkt Ruto kujihusisha na mipango ya mazishi lilitoka kwa familia ya Mzee Moi.

Uhasama baina ya familia ya Mzee Moi ulitokana na mvutano kuhusu ubabe wa siasa za Bonde la Ufa. Kwa sasa Dkt Ruto ana uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo ikilinganishwa na Bw Gideon Moi ambaye ana ufuasi katika Kaunti ya Baringo tu.

Kundi la Tangatanga, Jumanne liliahirisha mkutano wao wa kupigia debe ripoti ya BBI uliofaa kufanyika jana katika Kaunti ya Nakuru kufuatia kifo cha Mzee Moi.