Habari

Maziwa ya mursik hasababisha gonjwa la kansa – Utafiti

November 16th, 2018 2 min read

NASIBO KABALE na PETER MBURU

UNYWAJI wa maziwa mala ya kitamaduni yanayoandaliwa na jamii ya Kalenjin, maarufu kama mursik mara kwa mara umebainika kuwa kiini kikuu cha watu wanaoishi maeneo ya Kaskazini mwa Kenya na Bonde la Ufa kuugua gonjwa la saratani ya koromeo.

Vilevile, watu wanaotumia Miraa pamoja na chai moto huugua saratani hiyo, utafiti wa Taasisi ya Kitaifa kuhusu Saratani umebaini.

Taasisi hiyo Alhamisi lilisema kuwa maeneo ya Bonde la Ufa, Mashariki na Kaskazini Mashariki yalirekodi visa vingi zaidi vya Saratani ya Koromeo kutokana na hulka hizo za vyakula wanavyotumia wakazi wa huko.

Saratani hii ndiyo husababisha vifo vingi zaidi nchini kati ya saratani zingine, ikifuatwa na ile ya njia ya uzazi kwa wanawake, ya matiti, tumbo nay a uume. Saratani ya koromeo imerekodiwa kusababisha vifo 4,354 kila mwaka.

“Utafiti uliotekelezwa eneo la Tenwek unaonyesha kuwa vinywaji moto na unywaji wa Mursik ulichangia kupata kansa ya koromeo,” akasema Bw Alfred Karagu, kaimu Afisa Mkuu Msimamizi wa Taasisi hiyo.

Alisema kuwa wkazi wa maeneo hayo hutumia mursik mara kadha kwa siku na kwa kuwa kinywaji hicho kina kiwango fulani cha chembechembe ambazo husababisha saratani, hali hiyo inaweza kuanzisha kujengeka kwa saratani ya Koromeo.

Na japo unywaji wa chai moto uko sehemu nyingi za taifa, mtu anapotumia chai moto pamoja na Miraa hali hiyo huongeza uwezekano wa kupata saratani hiyo, utafiti huo ukasema.

Bw Karagu alisema kuchanganya chembechembe za tumbaku zilizoko kwenye majani chai na Miraa kunasababisha kuadhirika kwa ngozi nyororo ya ndani ya mshipa unaopitisha chakula kwenye koo.

Malkia wa Urembo Kaunti ya Nandi Zitah Jepkemboi (kulia), ampa Celestine Masinde wa timu ya raga nchini maziwa ya jamii ya Kalenjin almaarufu ‘mursik’, mjini Nandi miezi minne iliyopita. Picha/ Maktaba

Alisema kuwa sababu inayofanya wagonjwa wengi wa ugonjwa huo kufa ni kwa kuwa mshipa wa kupitisha chakula huwa umeharibika kabisa, haswa ugonjwa unapotambulika ukiwa umeadhiri mwili.

“Wagonjwa wengi hutafuta matibabu wakiwa wamechelewa na hivyo hatuwi na nafasi ya kusaidia sana kwani saratani huwa tayari imeadhiri mshipa wa kupitisha chakula. Wanaposhindwa kula, wagonjwa huishia kufariki,” Bw Karagu akasema.

Taasisi hiyo sasa inawashauri watu ambao wamekuwa na hulka hizo ama kushuhudia dalili kama kuwa na wakati mgumu kumeza chakula, kuhisi kama kuna kitu kilichokwama kooni ama kukonda kutafuta ushauri wa daktari kwani unaweza kuwa ugonjwa huo.

Matibabu ya ugonjwa huo huwa kuchinjwa na kutolewa kwa baadhi ya sehemu am ahata sehemu nyingi za koromeo ambazo zimeadhirika.

Hata hivyo, taasisi hiyo ilisema kuwa zoezi hilo hugharimu pesa nyingi na huwa wagonjwa wengi hawana uwezo.

Bw Karagu alisema kuwa hali ya ugonjwa huo kutambuliwa ukiwa umechelewa ama wagonjwa ambao tayari wametambuliwa kukosa kujua dalili za kuibuka tena zinapojitokeza pia ni kiini cha vifo vingi.

Saratani hiyo aidha imehusishwa na kula mchanga wa aina ya Volkano, unywaji wa pombe na kuvuta ama kula tumbaku.

Katika ripoti yake, Shirika la Afya Ulimwenguni baada ya utafiti wa visa vipya na vifo miongoni mwa wanaume na wanawake lilisema kuwa Wakenya 4,354 hufa kila mwaka kutokana na saratani ya Koromeo.