Habari

Mbadi akanusha mzozo bungeni kati ya ODM, Jubilee kuhusu BBI

July 5th, 2020 2 min read

GEORGE ODIWUOR na IBRAHIM ORUKO

KIONGOZI wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Bw John Mbadi, amekanusha madai kuwa wabunge wa ODM na Jubilee walitofautiana kuhusu kubuniwa kwa kamati zitakazosimamia utekelezaji wa ripoti ya Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kulikuwa na madai kuwa wabunge wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na wale wa mrengo wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, walitofautiana kuhusu utaratibu wa ugavi wa nafasi zilizobaki wazi, baada ya kuondolewa kwa wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na ripoti hizo, ilidaiwa kuwa wabunge wa Jubilee walitaka tu kutengewa nyadhifa zenye ushawishi, kama Kamati ya Bunge kuhusu Masuala ya Sheria na Kamati Simamizi Kuhusu Sheria Maalum.

Bw Mbadi alikanusha madai hayo, akisema kuwa alitofautiana tu na Kiongozi wa Wengi, Bw Amos Kimunya kuhusu kujumuishwa kwa baadhi ya wabunge katika kamati mbalimbali.

“Hali hiyo ilitiliwa chumvi, kwani madai hayo si ya kweli. Ni mimi tu na Bw Kimunya tuliotofautiana kidogo kuhusu taratibu za kubuniwa kwa baadhi ya kamati hizo kwenye Bunge,” akasema.

Akihutubu katika kituo cha kibiashara cha Kiyabuya, Suba Kusini, alipozuru mradi wa ujenzi wa barabara ya Mbita-Sindo-Maguga, Bw Mbadi alisema kuwa hakuridhishwa na ujumuishaji wa wanachama wa kamati hizo mbili kutoka kwa upande wa Jubilee.

Kulingana naye, baadhi ya wabunge huenda wakavuruga utekelezaji wa ripoti hiyo, ilhali wamewekwa katika kamati hizo muhimu.

“Mchakato wa BBI unahitaji watu ambao wamejitolea kabisa kushiriki kikamilifu. Hata hivyo, wabunge wengi hawako tayari, ambapo ndipo tulipendekeza baadhi ya majina kubadilishwa. Huenda baadhi ya wabunge wakasusia vikao kuijadili ripoti hiyo katika kiwango cha kamati, ili kuwanyima wenzao nafasi ya kuchangia itakapowasilishwa rasmi bungeni,” akasema.

Mbunge huyo alisema kuwa wabunge ambao hawaungi mkono ripoti hiyo wanapaswa kuondolewa kwenye kamati hizo.

“Sitaki kuona majina ya wabunge kama Gladys Shollei (Uasin Gishu), William Cheptumo (Baringo Kaskazini) na wengine waliojumuishwa kwenye kamati hizo. Nilimwambia Bw Kimunya kuwaondoa kwani walikuwa wakiipinga ripoti,” akasema.

Kwingineko, Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala ametangaza kuwa atamenyana na Musalia Mudavadi katika juhudi za kuwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC).

Alipuuza uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho kumfurusha kwa kuunga mkono mwaniaji wa chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

“Sijafanya lolote la kusababisha nifukuzwe chamani. Uamuzi huo hauna msingi kwa sababu Baraza halikubuniwa kisheria. Sitajisumbua kwenda kortini. Ninajiandaa kuwa kinara wa chama uchaguzi ukiitishwa,” akasema.