Mbadi atofautiana na Orengo

Mbadi atofautiana na Orengo

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa ODM John Mbadi amepuuzilia madai ya Seneta wa Siaya James Orengo kwamba kiongozi wa chama hicho Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wamekubaliana kushirikiana katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini, amesema chama hicho hakitajiunga na muungano wowote wa kisiasa, akisema madai ya Orengo ni ya kibinafsi na hayawakilishi msimamo rasmi wa chama.

“Ningependa ieleweke kuwa ODM haibuni muungano na chama au mtu yeyote. Msimamo wowote unaokinzana na huu unafaa kuchukuliwa kama wa kibinafsi,” akasema Mbadi.

Akiongea na wanahabari afisini mwake katika majengo ya bunge Alhamisi, Bw Mbadi alisema muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga uliotiwa saini Machi 2018 haukuhusu masuala ya siasa na uchaguzi mkuu wa 2022.

“Kwa hivyo, ni makosa kwa mtu kudai kuwa tumebuni mwafaka wa kisiasa na mtu yeyote. Labda haya ni matamanio ya Bw Orengo ambayo sio mbaya lakini hafai kuwakanya wafuasi wetu na Wakenya kwa jumla kwamba ni msimamo wa chama chetu,” Bw Mbadi akasema.

Mbunge huyo ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa alisema msimamo wa ODM ni kwamba huu sio wakati wa kuchapa siasa za 2022 na msimamo huo haujabadilika.

“Kama chama tumekuwa tukiwaonya wanachama wetu dhidi ya kuanza kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa 2022 na kamwe hatujabadili msimamo huo,” akasema Bw Mbadi.

Urais

Mnamo Jumatatu, akihojiwa katika runinga ya KTN, Bw Orengo alisema ODM inafanya kazi kichinichini na Rais Kenyatta kwa lengo la kumwezesha Bw Odinga kutwaa urais mnamo 2022.

“ODM inalenga mamlaka ya kisiasa; na tunafanya mikutano kama hii. Macho yetu yanaelekezwa katika uchaguzi mkuu wa 2022. Ung’ang’aniaji huu wa mamlaka utaendelezwa na muungano katika ya ODM kwa upande mmoja na Jubilee kwa upande mwingine na Uhuru Kenyatta anachangia mchakato wa kuundwa kwa muungano huu,” Bw Orengo akasema.

Seneta huyo ambaye ni kiongozi wa wachache katika Seneti pia alisema kuwa amefanya mkutano wa faragha na Rais Kenyatta kwa saa nne ambapo alimshawishi kuwa ataunga mkono azma ya Odinga kuingia Ikulu mwaka 2022.

You can share this post!

Mazao yaliyokuzwa kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai yana...

Iravaya Obiri mambo mazuri kwake Olimpiki kwa wenye ulemavu

adminleo