Habari MsetoSiasa

MBADI na Kimunya bado hawaelewani kuhusu uanachama bungeni

July 7th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

VUTA nikuvute kuhusu uteuzi wa wanachama wa kamati mbili za bunge Jumatatu iliendelea kutokota chama cha ODM kiliibua hofu kuwa wawakilishi wa Jubilee katika kamati hiyo watahujumu mchakato wa maridhiano, BBI.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema wabunge waliopendekezwa na Jubilee kuiwakisilisha katika Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) na Kamati ya Bunge kuhusu Sheria Mbadala (Committee on Delegate Legislation) ni wakosoaji wa BBI.

Katika kile kinachoonyesha kuwa kudhoofika kwa ukuruba kati ya Jubilee na ODM, kwa moyo wa handisheki, Bw Mbadi alidai kuwa hatua ya Jubilee kujuisha wabunge wa mrengo wa tangatanga katika kamati hizo “kunaonyesha kuwa sasa hawana haja na BBI”.

“Kamati hizi mbili zitatekeleza wajibu mkubwa katika utayarishaji wa sheria zitakazofanikisha kupitishwa kwa ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) ambayo hivi karibuni itawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wetu Raila Odinga. Kwa hivyo, wanachama wazo wanapasa kuwa wabunge wanaounga mkono mchakato huu,” akasema Bw Mbadi.

Mbunge huyo wa Suba Kusini alisema kuwa wabunge wa tangatanga waliopendekezwa kuhudumu katika kamati hizo ni wengi kiasi kwamba wanaweza kuhujumu mpanngo wa BBI.

“Ripoti hii ni muhimu kwa sababu itasheheni mapendekezo kuhusu mageuzi ya Katiba ambayo Rais na Mheshimiwa Odinga wamekuwa wakiupigia debe,” akaeleza Bw Mbadi.

Kwa mfano, akasema, ni wabunge watatu pekee miongoni mwa wabunge 12 wa Jubilee waliopendekezwa kuhudumu katika JLAC, wanaunga mkono BBI na handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga. Kamati hiyo inapasa kuwa na wanachama 19 ambapo saba miongoni mwa ni wa mrengo wa upinzani, NASA.

“Ikiwa miongoni mwa wabunge 12 wa Jubilee waliopendekezwa, tisa ni wanachama wa tangatanga ni watatu pekee wanaweza kutegemewa. Hii ina maana kuwa wanaweza kuhujumu ajenda ya BBI,” Bw Mbadi akasema.

“Nilimwambia kiongozi wa wengi Bw Amos Kimunya kuwa sikuwa na imani na wabunge kama Gladys Shollei (Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu), Gitonga Murugara (Tharaka), Johna Kiarie (Dagoreti Kusini) kuwa wanachama wsa JLAC kwa sababu hawa ni watu ambao wamekuwa wakikosoa handisheki na BBI,” akaongeza.

Bw Mbadi alisema kuwa wengi wa wawakilishi wa Jubilee katika Kamati ya Sheria Mbadala pia ni wanachama wa tangatanga ambao watahujumu mchakato wa BBI

“Kile tunaomba ni kwa upande wa Jubilee kuteuwa wabunge ambao wataendeleza ajenda ya Rais kuhusiana na mageuzi yanayopendekezwa katika BBI,” akasema.

Lakini Bw Kimunya alisema kuwa kamati hizo haziundwi upya kupitisha ripoti ya BBI bali kutekeleza “wajibu wa kuwa kiungo muhimu cha bunge katika mchakato wa utungaji sheria.”

Wiki jana Kimunya alilazimishwa kuondoa orodha ya wanachama wa Jubilee katika kamati mbalimbali za bunge zilizoundwa upya baada ya wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto kuondolewa, baada ya mrengo wa wachache kupinga orodha ya wawakilishi wa Jubilee katika kamati hizo mbili.

“Walisema wanataka mashauriano zaidi lakini hawawezi kushauriana kuhusu wanachama wetu,” Bw Kimunya akasema Jumatatu.

“Ni makosa kwa watu wengine kudhani kuwa shughuli zima la kuundwa upya kamati za bunge ilidhamiria kuwaondoa wale wabunge wanaosawiriwa kuwa wanachama wa tangatanga. Lengo sio kuwaondoa watu fulani walivyodhani. Siwezi kuwaondoa watu kwa sababu watu fulani wanataka nifanye hivyo,” akasema.

Bw Kimunya alisema upande wa upinzani unapasa kujizatiti kupalilia umoja bungeni namna ambavyo Rais Kenyatta anajizatiti kuunganisha nchini.

Naibu kiranja wa wengi Maoka Maore na mwenzake wa upinzani Junet Mohammed pia wanapanga kuandaa mkutano kuleta maridhiano kuhusu suala la uanachama wa kamati hizo mbili.