Michezo

Mbamba wa Uswidi amezea kuisakatia Stars

February 20th, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

MKENYA Chris Mbamba anayepiga gozi la kulipwa nchini Uswidi amesema yupo tayari kusakatia timu ya Harambee Stars.

Mvamizi huyo ambaye pia anaweza kucheza kama winga huchezea Oskarshams AIK nchini humo.

”Linaweza kuwa jambo zuri endapo naweza fanikiwa kuvalia jezi ya timu ya taifa ya Kenya,” alisema na kuongeza kwamba itakuwa furaha kwake kutimiza ndoto hiyo.

Mbamba mwenye umri wa miaka 26 alisema endapo kocha wa Harambee Stars, Sebastian Migne itafikia wakati amuite katika kikosi cha Harambee Stars anaamini ana uwezo tosha kuonyesha soka la kupendeza. Alidokeza kwamba ana ndoto ya kuwakilisha taifa hili katika soka la kimataifa hivi karibuni.

Alijipiga kifua kwamba ameiva vizuri anakojivunia ujuzi wa kuunda nafasi za kufunga magoli. Mchezaji huyo aliyezaliwa mjini Harare, Zimbabwe kisha kuelekea nchini humo alikojipatia mafunzo ya kusakata kandanda anajivunia kuzipigia Club Hamkam nchini Norway pia Club Port Vale inayoshiriki English League One.

Kijana huyo akiwa Club Port Vale anajivunia kuwepo dimbani ilipokabili Bolton Wanderers katika mchezo wa ligi.