Mbappe afunga mabao matatu dhidi ya Metz na kuibuka Mfungaji Bora wa Ligue 1 msimu wa 2021-22

Mbappe afunga mabao matatu dhidi ya Metz na kuibuka Mfungaji Bora wa Ligue 1 msimu wa 2021-22

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe alisherehekea maamuzi ya kutia saini mkataba mpya wa miaka mitatu kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) kwa kufunga mabao matatu dhidi ya Metz katika mchuano wa mwisho wa kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu.

Nyota huyo raia wa Ufaransa alishuka dimbani saa chache baada ya kutangaza kwamba alikuwa amefutilia mbali ofa aliyokuwa akipokezwa na Real Madrid ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ushindi wa 5-0 uliosajiliwa na PSG katika mechi hiyo ugani Parc des Princes ulishuhudia Metz wakiteremshwa ngazi kwenye soka ya Ligue 1 msimu huu.

Fowadi matata raia wa Brazil, Neymar naye alicheka na nyavu za Metz na bao hilo lake lilikuwa la 100 akivalia jezi za PSG tangu ajiunge nao kutoka Barcelona mnamo 2017. Goli jingine la PSG lilijazwa kimiani na Angel di Maria aliyekuwa akichezea waajiri wake hao kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza kutafuta hifadhi mpya kwingineko.

Di Maria amechezea PSG kwa miaka saba na anahusishwa pakubwa na Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Mabao matatu yaliyofungwa na Mbappe dhidi ya Metz yanamweka kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa Ligue 1 msimu huu kwa magoli 28, matatu zaidi kuliko Wissam bne Yerder wa AS Monaco.

Metz watashiriki soka ya Ligue 2 msimu ujao baada ya kushushwa ngazi kwa pamoja na Bordeaux walioteremshwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30. Bordeaux waliokamilisha msimu kwa alama 31 sawa na Metz walishushwa daraja licha ya kusajili ushindi wa 4-2 dhidi ya Brest ugenini.

St Etienne waliokota alama moja baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Nantes na kukamilisha kampeni katika nafasi ya 18 na hivyo kufuzu kwa mchujo dhidi ya Auxerre katika juhudi za kubaini nani kati yao atashuka ngazi au kupanda daraja.

Mbappe, 23, alisaidia Ufaransa kunyanyua Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi na amekuwa akihusishwa pakubwa na Real Madrid kabla ya kuwaruka na kurefusha muda wa kuhudumu kwake PSG kwa miaka mitatu zaidi.

Maamuzi hayo ya Mbappe yamekera zaidi Real wanaotishia sasa kuwasilisha malalamishi rasmi dhidi ya Mbappe na PSG kwa vinara wa Uefa na mamlaka ya soka nchini Ufaransa na bara Ulaya.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Tammy Abraham aweka rekodi mpya ya ufungaji wa mabao...

PAUKWA: Madhila ang’amua subira huvuta heri

T L