Michezo

Mbappe apuuza Arsenal, Man Utd na Chelsea na kuyoyomea Real Madrid

February 21st, 2024 2 min read

PARIS, UFARANSA

SASA ni rasmi mshambuliaji matata Kylian Mbappe ataondoka Paris Saint Germain (PSG) ya Ligue 1 na kujiunga na Real Madrid ya La Liga nchini Uhispania.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 25 tayari ameijulisha PSG kwamba ataondoka mwishoni mwa msimu huu hapo Juni, 2024.

Habari zaidi kuhusu mkataba huo mpya zinasema tayari amesaini kandarasi ya kujiunga na Real Madrid, lakini hakukubaliwa kusema chochote kutokana na vikwazo kwenye mkataba wake na klabu ya PSG ambayo ameifungia mabao 244 tangu 2017.

Staa huyo alitaka mpango wake wa kuondoka ukamilike kufikia mwezi ujao wa Mei, na tayari amekutana na rais wa PSG, Nasser al Khelaifi na kumueleza rasmi kwamba ataondoka pale mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Mara tu habari hizo zilipotangazwa rasmi, PSG haikumjumuisha katika kikosi cha kwanza kilichocheza na Nantes wikendi iliyopita, lakini aliingia na kuwafungia penalti ambayo imewakitisha kileleni mwa msimamo wa Ligue 1 kwa pengo la pointi 14.

Amekubali mkataba wa miaka mitano, ambapo atakuwa akipokea Sh2.4 bilioni kila msimu, mbali na Sh23.5 bilioni za kusaini mkataba huo pamoja na marupurupu mengine kwa kipindi cha miaka hiyo mitano.

Kadhalika staa huyo atakubaliwa kuvuna kiasi fulani cha haki ya picha zake zitakazotumika kupamba matangazo ya biashara.
Mbappe amekuwa akipokea mshahara wa Sh4 bilioni kwa mwaka akiwa PSG.

Kocha Carlo Ancelotti tayari amefikiria jinsi atakavyomtumia nyota huyo kikosini, pamoja na kiungo Muingereza Jude Bellingham anayetarajiwa kumuandalia mipira.

Katika mfumo huo, kinda Vinicius Junior wa Brazil atacheza akitokea upande wa kushoto, Mbappe akishambulia akitokea upande wa kulia na kusaidiana na mshambuliaji wa katikati.

Iwapo kiungo Luka Modric ataondoka klabuni mwishoni mwa msimu huu, Mbappe atarithi jezi yake nambari 10 anayovaa akichezea timu ya taifa ya Ufaransa.

Mbappe alisaidia Monaco kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Ligue 1 kabla ya kujiunga na PSG akiwa na umri wa miaka 18 mnamo 2017 kwa mkopo kabla ya kusajiliwa rasmi kwa mkataba wa kudumu uliogharimu Sh30.4 bilioni.

Kwa jumla, ameifungia vigogo hao wa Ufaransa mabao 244 pamoja na kutoa pasi 93 za uhakika katika mechi 291, mbali na kuisaidia kushinda ubingwa wa Ligue 1 mara tano.

Alitarajiwa kuagana na PSG kama mchezaji huru msimu wa 2021/2022, lakini akakubali kuendelea kuichezea baada ya kurefusha mkataba wake kwa miaka miwili.

Lakini sasa ameweka wazi kwamba hatakubali mkataba mpya wa mwaka mmoja, siku chache tu baada ya kukataa kukutana na mabwanyenye wa klabu ya Al-Hilal inayoshiriki ligiku ya Saudi Arabia, Saudi Pro League.

Mashabiki wa Real Madrid wamemsubiri kwa hamu ugani Santiago Bernabeu kumuona akisakatia klabu yao ambayo kwa sasa iko kileleni mwa ligi kuu ya La Liga, nchini Uhispania.

Mapema wiki hii uvumi ulizuka kuwa mwanasoka huyo amewasiliana na Arsenal na Manchester City za Uingereza zilizotaka kumsajili.