Michezo

Mbappe avunjika pua Ujerumani ikisaka ushindi dhidi ya Hungary


KYLIAN Mbappe wa Ufaransa alipata jeraha la pua Jumatatu usiku katika mechi ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Austria kwenye fainali za Euro 2024, ingawa hatahitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura.

Katika mechi nyingine Kundi D, Romania ilicharaza Ukraine 3-0 katika Kundi E, huku wachezaji wengi wa Ukraine wakieleza vile wanavurugwa akili kutokana na jinsi miji yao nyumbani inavyovamiwa na makombora ya Urusi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ukraine kushiriki katika mashindano makubwa tangu Rais Vladimir Putin wa Urusi aamuru majeshi yake kuvamia Ukraine mnamo Februari 2022.

Romania inaorodheshwa katika nafasi ya 24 kwenye viwango vya kimataifa vya Fifa, huku Ukraine wakishikilia nafasi ya 22 katika viwango hivyo.

Lakini matokeo ya kustaajabisha zaidi yalipatikana wakati Ubelgiji walipigwa 1-0 na Slovakia katika mechi ya Kundi E iliyochezewa Frankfurt. Ubelgiji inakamata nafasi ya pili, wakati Slovakia ikiwa ya 48 kwenye msimamo huo wa timu 210.

Shirikisho la Soka Ufaransa limesema Mbappe ambaye ndio nahodha wa timu ya taifa atavalia barakoa kwa muda, ijapo haijulikani iwapo atacheza dhidi ya Uholanzi, Ijumaa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23, alilazimika kuondoka uwanjani baada ya uso wake kugongana na Kevin Danso wakiwanaia mpira wa hewani kwenye pambano hilo ambalo Ufaransa ilishinda 1-0.

Alikimbizwa Dusseldorf Hospital ambako madaktari walithibitisha kuvunjika kwa pua lake. Baadaye alirejeshwa katika kambi ya kikosi cha Ufaransa anakotarajiwa kuendelea kutibiwa, lakini upasuaji wa dharura hautafanyika.

Pigo kuu kwa kikosi chake

Kocha Didier Deschamps alisema kuumia kwa mchezaji huyo ni pigo kuu kwa kikosi chake ambacho kilikumbwa na upinzani mkubwa katika mechi hiyo.

Mbappe ameifungia Ufaransa mabao 47 katika mechi 80, na ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemewa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Euro 2024.

Alichangia katika bao la ishindi baada ya krosi yake kufungwa na Max Wober aliyekuwa akijaribu kuokoa hatari langoni mwake.

Mchezaji huyo wa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ambaye anajiandaa kujiunga na Real Madrid hajawahi kufunga bao katika mashindano ya Euro 2024, lakini amefunga 12 katika Kombe la Dunia.

Alipoulizwa iwapo atacheza Ijumaa dhidi ya Uholanzi, kocha Deschamps alisema daima timu ya Ufaransa itakuwa nzuri zaidi akiwa kikosini. “Iwapo madktari wataamua asicheze, itabidi tukubali akae nje.

Mchezaji mwenzake, Adrien Rabiot aliambia waandishi kwamba Mbappe alisema “pengine atakuwa tayari kucheza mechi ya tatu dhidi ya Poland, Jumanne ijayo.”

Matokeo ya mechi za Jumatatu: Austria o Ufaransa 1, Ubelgiji 0 Slovakia 1, Romania 3 Ukriane 0.

Baada ya ushindi mkubwa wa 5-1 dhidi ya Scotland katika mechi ya kwanza katika Kundi A, Ujerumani wanarejea uwanjani leo usiku kutafuta ushindi wa pili dhidi ya Hungary.

Ushindi huo ulikuwa mkubwa zaidi kwa wenyeji hao tangu wacharaze Brazil 7-1 kwenye nusu-fainali ya Kombe la Dunia la 2024 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil.