Michezo

Mbappe kumtwaa rasmi kimwana Alicia Aylies

December 10th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, 19, amekiri kwamba anapania kumfanya kidosho Alicia Aylies wake wa halali mapema 2019.

Akiwazungumzia wanaudaku wa gazeti la The Sun mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbappe alifichua kuwa kwa sasa anashughulikia maandalizi ya sherehe za harusi zitakazomshuhudia hatimaye akifunga pingu za maisha na Alicia, kidosho aliyetawazwa mshindi wa Miss France mnamo 2017.

Japo Mbappe alitaka maandalizi ya hafla hiyo yasalie kuwa siri kubwa, Alicia ndiye aliyeudokezea ulimwengu wa udaku kuhusu mpango wao kwa kurushia mitandaoni picha alizopigwa kwa pamoja na mwanasoka huyo ambaye upekee wa maarifa yake unazidi kutegemewa sasa na kocha Thomas Tuchel uwanjani Parc des Princes.

Kwenye picha hiyo, Alicia alipania kuonyesha zaidi kidole chake kilichovishwa pete ya thamani kubwa japo hakuweka bayana iwapo ni pete ya uchumba kutoka kwa Mbappe au la.

Hata hivyo, aliandika, “Wachache sana wa sampuli yako. Hivi karibuni nitakupokeza rasmi funguo za mzinga wangu na kinachosalia tu ni sisi kuweka sawa mipango ya ndoa ambayo sina shaka itafana sana”.

Kwa upande wake, Mbappe alisema kwa sasa kinachomfanya kukuna kichwa ni nani wa kumteua kuwa msimamizi wa ndoa yao katika orodha ndefu ya wanasoka marafiki zake.