Michezo

Mbappe kuuguza jeraha kwa muda mrefu

July 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG) atakuwa nje kwa kipindi kirefu baada ya kupata jeraha baya la kifundo cha mguu wa kulia wakati wa fainali ya kuwania ubingwa wa French Cup dhidi ya Saint-Etienne mnamo Julai 24, 2020.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa PSG kusakata tangu kutamatishwa rasmi kwa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Aprili 2020 ambapo PSG walitawazwa mabingwa.

Mbappe, 21, aliondolewa uwanjani kwa machela akiwa anatiririkwa na machozi baada ya kuchezewa visivyo na beki Loic Perrin katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, alirejea uwanjani baadaye kwa usaidizi wa mikongojo na kukalia katika eneo la wachezaji wa akiba wa PSG.

PSG wamesema kwamba madaktari wao watatathmini upya jeraha la Mbappe chini ya kipindi cha saa 72 zijazo na kupendekeza ni lini atakapofanyiwa upasuaji kabla ya kutoa taarifa rasmi kuhusu urefu wa muda atakaohitaji ili kupona kikamilifu.

PSG kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Olympique Lyon katika fainali ya French League Cup mnamo Julai 31, 2020 kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Atalanta ya Italia kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 12, 2020.

Iwapo PSG ambao kwa sasa wananolewa na kocha Thomas Tuchel watasonga mbele kwenye UEFA, basi watanogesha nusu-fainali za kivumbi hicho mnamo Agosti 18-19, 2020 huku fainali ikiratibiwa kupigwa jijini Lisbon, Ureno mnao Agosti 23.

Mbappe ambaye ni mzawa wa Ufaransa, anajivunia kufungia PSG jumla ya mabao 29 kutokana na mechi 33 za hadi kufikia sasa msimu.