Mbappe na Di Maria wasaidia PSG kuendeleza presha kwa Lille

Mbappe na Di Maria wasaidia PSG kuendeleza presha kwa Lille

Na MASHIRIKA

WASHAMBULIAJI Angel di Maria na Kylian Mbappe walicheka na nyavu za Nimes mnamo Februari 3, 2021 na kusaidia waajiri wao Paris Saint-Germain (PSG) kuendeleza presha dhidi ya Lille na Olympique Lyon wanaoshikilia nafasi mbili za kwanza kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Nyota raia wa Argentina, Di Maria, aliwafungulia PSG ukurasa wa magoli kunako dakika ya 18 kabla ya kuchangia bao la pili lililojazwa kimiani na Pablo Sarabia katika dakika ya 36.

Mbappe ndiye aliyezamisha kabisa chombo cha wageni wao kwa kufunga bao la tatu na la mwisho kwa upande wa PSG dakika 22 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa. PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligue 1 walikosa huduma za fowadi mahiri Neymar Jr katika pambano hilo.

Ushindi dhidi ya Nimes uliwapaisha PSG hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 48, moja nyuma ya nambari Lyon. Lille waliowacharaza Bordeaux 3-0 ugenini, wanadhibiti usukani wa jedwali kwa pointi 51, sita mbele ya AS Monaco wanaofunga mduara wa nne-bora.

Mkia wa jedwali hilo la Ligue 1 unavutwa sasa na Nimes ambao sawa ana Dijon, wamejizolea alama 15 pekee kutokana na mechi 22 zilizopita. Lorient nao wanakamilisha orodha ya vikosi vitatu vya mwisho vilivyopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Februari 3):

PSG 3-0 Nimes

Bordeaux 0-3 Lille

Metz 1-1 Montpellier

Reims 0-0 Angers

Rennes 1-1 Lorient

Strasbourg 2-2 Brest

Dijon 0-1 Lyon

Lens 2-2 Marseille

Monaco 2-1 Nice

Saint-Etinne 1-1 Nantes

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Barcelona waponea kuondolewa na Granada kwenye Copa del Rey

Man-City wacharaza Burnley tena na kujiweka pazuri kutwaa...