Habari Mseto

Mbinu mpya ya wizi inayotumiwa na wanawake wanaojifanya wajawazito

October 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KUNA genge la majambazi wanawake wanaojifanya ni wajawazito na kuwapora wananchi jijini Nairobi.

Wanachama wa genge hili la wanawake wanahudumu kati ya Tea Room, River Road na eneo la Jamia Mosque.

Wanawake hawa ni wajanja kwa vile wanamtazama wanayetaka kumlaghai na kujitambulisha kwake kuwa wako na shida na wamewasili kutoka mashambani na waliyetazamia awalaki hajafika na wameingiwa na wasiwasi.

Wanadada hawa wanaelewa barabara wanachotenda.

Ili wamkanganye mteja wao wanajifanya wamebeba kiwango kikubwa cha pesa na wanahofia watanyang’anywa.

Mmoja wa wahasiriwa hao Ijumaa jioni mwendo wa saa mbili jioni  alimpora mwanamke mkoba uliokuwa na faili za afisi, kitambulisho cha kitaifa na cha kazini.

Mhasiriwa alielezwa na mwanamke huyo mwenye umri kati ya 22-30  amewasili jijini akitoka Naivasha na hakumwona shemeji yake wapeleke Sh600,000 kwa Benki ya Barclays tawi la Queensway.

Tapeli huyo alimwelezea mlalamishi kuwa ni mja mzito na alikuwa anahisi uchungu na mshtuko baada ya kumkosa shemejiye.

Tapeli huyo aliyejitambua kwa jina Elizabeth Wanjiru alimkabidhi mlalamishi mkoba aliodai uko na kitita cha Sh600,000 ambebee kwa vile alikuwa anaogopa kuvuka vuka barabara za Nairobi akiwa na pesa hizo.

“Naogopa kunyang’anywa kabla hatujafika kituo cha Petroli cha Shell karibu na jengo la Odeon. Nibebee pesa hizi tafadhali,” alisema mlalamishi aliyezugumza na Taifa Dijitali.

Hata kabla ya kufika katika kituo cha mafuta cha Shell “Elizabeth Wanjiru” alitoweka na mfuko wa mlalamishi.

Mlalamishi alifufuliza moja kwa moja hadi kituo cha Polisi cha Central na kupeana mkoba alioachiwa na tapeli huyo na kwa mshtuko na mshangao aligudua “mkoba ulikuwa na karatasi tupu na wala sio Sh600,000.”

Mlalamishi alielezwa na Polisi kwamba eneo hilo la Tea Room na Jamia Mosque wanatoka eneo la Meru na polisi wanaendelea kuwawinda.

Polisi wamewatahadharisha wanaosafiri kutoka nje ya Nairobi wawe macho wasiporwe na wakora hawa.