Habari Mseto

Mbinu mpya za walanguzi kusafirisha mihadarati zaanikwa

July 17th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

IMEFICHUKA kuwa walanguzi wa dawa za kulevya sasa wanatumia mbinu mpya za kusafirisha mihadarati humu nchini ili wasibambwe na polisi.

Mbinu hizo zinajumuisha kutumia wanawake wazee kusafirisha mihadarati, watoto, mavazi ya kidini, magari ya wanasiasa na serikali, yale ya kusafirisha bidhaa maalumu na wakati mwingine kutumia walemavu.

Kisa cha majuzi zaidi kilihusu nyanya mwenye umri wa miaka 83, ambaye alikiri mahakamani kwamba alipatikana na gramu 268 za bangi mnamo Julai 10, katika Kaunti ya Nyeri.

Katika kisa hicho, mahakama iliambiwa kwamba maafisa wa polisi walipata habari kutoka kwa umma kuwa nyanya huyo alikuwa katika matatu akisafirisha bangi kutoka mji wa Nyeri akielekea Muthiga ndipo wakamnasa.

Mnamo Aprili, mwanamke wa miaka 62 alikamatwa pamoja na mwenzake wa miaka 40 wakiwa na kilo moja ya heroin inayogharimu Sh3 milioni katika Kaunti ya Mombasa.

Salima Bakari na Zainab Abdi Farah walishtakiwa na wakaachiliwa kwa bondi ya Sh500,000 pesa taslimu au dhamana ya Sh200,000.

Polisi waliohojiwa walisema utumizi wa wanawake, hasa wenye umri mkubwa kusafirisha mihadarati, unatokana na jinsi msako dhidi ya washukiwa wakuu wa ulanguzi ambao wengi ni wanaume ulivyoimarika.

Kulingana na ripoti ya Afisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya Mihadarati na Uhalifu, wakati mwingi walanguzi hutumia wanawake ambao wako katika hali mbaya kimaisha na huhitaji usaidizi wa kifedha kwa dharura.

Lakini wakati mwingine, wao wenyewe ndio walanguzi halisi baada ya kujifunza biashara hiyo kwa muda.

“Kuna sababu nyingi ambazo zimedhihirika kusukuma wanawake katika biashara ya mihadarati, lakini sana sana huwa ni kutokana na udhaifu wao katika jamii, ghasia, uhusiano wa kimapenzi au masuala ya kiuchumi,” ikasema ripoti hiyo ya 2018.

Imebainika walanguzi hawajahurumia hata watoto kwenye biashara hii. Katika eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, mwalimu wa shule moja ya msingi alifichua jinsi yeye na wenzake walivyoshtuka kupata misokoto ya bangi ndani ya mkoba wa mwanafunzi wa Darasa la Kwanza.

“Tulipomhoji alitwambia yeye hupewa mzigo huo na mamake kumpelekea mwanamume fulani anayemtambua kama mjomba wake, lakini leo hakumpata alipoenda kwake ndipo akaja na mzigo huo shuleni,” akasema mwalimu huyo.

Kando na haya, mavazi ya kidini kama vile buibui za Kiislamu na vilemba vya Akorino yameibuka kutumiwa kuficha dawa za kulevya zinaposafirishwa.

Mwezi uliopita, wanawake wawili waliotambuliwa kama Zainab Adan na Insene Bakala Guyo walikamatwa wakiwa na kilo nne za bangi katika Kaunti ya Marsabit, kwenye basi lililokuwa likielekea Nairobi.

Polisi walisema wanawake hao walikuwa wamefunga bidhaa hizo mwilini mwao kisha wakavaa buibui.

Katika Kaunti ya Murang’a ambapo idadi ya vijana wanaoathiriwa na utumizi wa dawa za kulevya na pombe haramu imeongezeka kwa kasi, Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini, Bw John Ondit alithibitisha kuna watu wanaovaa vilemba vya Akorino na kofia za Rasta kuficha bangi vichwani mwao.

“Kuna waumini wa dini ya Akorino na Rasta ambao wamepotoka na kuingilia biashara ya bangi. Murang’a Kusini imeathirika zaidi. Katika barabara ya Nairobi-Kenol-Moyale, bangi pia hufichwa kwenye trela za kusafirisha mafuta na tunaomba umma kutusaidia kukabiliana na dawa hizi za kulevya,” akasema.

Kumekuwepo visa ambapo mihadarati ilipatikana ikisafirishwa kwenye magari ya wanasiasa na yale ya serikali katika miezi ya hivi majuzi.

Aliyekuwa mgombeaji urais Jaffer Isaak Sora, alikamatwa mwezi uliopita akidaiwa kusafirisha kilo 445 za bangi zinazogharimu Sh13.35 milioni mjini Marsabit.

Bw Sora, 45, alikanusha mashtaka ya ulanguzi katika Mahakama Kuu ya Meru na akaachiliwa kwa bondi ya Sh6 milioni au dhamana ya Sh3 milioni pesa taslimu.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba walanguzi huamini si rahisi gari la mwanasiasa au la serikali kusimamishwa na polisi barabarani.

Vilevile, ilisemekana kuna wanaohadaa walemavu wenye mahitaji ili wafiche mihadarati kwenye vifaa kama vile mikongojo na viti vya magurudumu kisha kusafirisha hadi mahali kuna wateja wanaosubiri.