Mbinu za kuzima Ruto Mlimani zaanza kusukwa

Mbinu za kuzima Ruto Mlimani zaanza kusukwa

Na BENSON MATHEKA

WASHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta kutoka eneo la Mlima Kenya wameanza kusuka mikakati ya kupunguza umaarufu wa Naibu Raise eneo lao na kumvumisha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Mikakati hiyo inadhamiria kumsawiri Bw Odinga kama rafiki wa eneo hilo ambaye serikali yake itajali na kulinda maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya.

Mnamo Jumanne, baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta waliahidi Bw Odinga kwamba watamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao wakimtaja kama rafiki wa jamii hiyo kwa miaka mingi.

Duru zinasema kwamba kwa baraka za Rais Kenyatta, wanasiasa wanaounga handisheki wataendesha kampeni kutumia vyombo vya habari hasa vituo vya redio vya lugha za jamii za eneo hilo kumjenga Bw Odinga.

“Tuna mikakati yetu na wakati huu, wanaodhani ni jogoo wa kuwika Mlima Kenya watajua kwamba tunamtambua Bw Odinga kama jamba,” alisema mbunge mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake asionekane kumwaga mtama mapema.

Alisema kwamba wamepanga kuhakikisha kuwa Bw Odinga atamrithi Rais Kenyatta kwa kuwa amedhihirisha hana kisasi au chuki na jamii yoyote Kenya.

Mnamo Alhamisi, baraza la watu mashuhuri katika Kaunti ya Murang’a ambalo lina ushawishi mkubwa katika kaunti hiyo na Mlima Kenya kwa jumla lilikutana kujadili hali ya siasa.

Ingawa waliyojadili hayakubainika mara moja, duru zinasema walijadili athari za siasa kwa eneo lao na anayeweza kulinda maslahi ya wakazi.

Mkutano wao ulijiri siku mbili baada ya mfanyabiashara SK Macharia, mmoja wa wanachama wa baraza hilo, kuwa mwenyeji wa Bw Odinga katika hafla aliyoandaa eneo la Ndakaini ambapo waliozungumza walimsifu Bw Odinga na kuahidi kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru zinasema kuwa miongoni mwa mikakati ya washirika wa Rais Kenyatta ni kuondoa hofu ya wakazi kumhusu Raila ambayo imeenezwa na kukita mizizi kwa miaka mingi na uongo ambao washirika wa Naibu Rais wamekuwa wakieneza kumhusu.

“Wapinzani wetu wamekuwa wakitangatanga eneo letu kwa miaka minne na kudanganya watu wetu kwamba Raila ni hatari kwa eneo lao ilhali ‘Baba’ hajawahi kufanya lolote baya. Tunataka kuondoa uongo huu,” alisema mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda.

Kulingana na mbunge huyo, moja ya mikakati yao ni kufuta uongo wa Naibu Rais, Dkt Ruto na washirika wake na kuleta ‘pumzi’ mpya katika siasa za eneo la Mlima Kenya.

Alisema wakati umefika wa kuondoa propaganda na kueleza wakazi ukweli.

Ijumaa, washirika wa Rais Kenyatta walitarajiwa kukutana kusuka mikakati kuanzia madiwani, wabunge, magavana na viongozi wa kijamii wenye ushawishi.

Lengo la washirika na wanamikakati wa Rais Kenyatta ni kufuta kauli-mbiu ya Hasla ambayo Dkt Ruto ametumia kupenya na ‘kuteka’ eneo hilo kwenye safari yake ya kuelekea ikulu 2022.

Ujumbe wao kwa wakazi utakuwa ni kwamba Bw Odinga ametekeleza wajibu mkubwa kwa nchi hii si tu kuanzia handisheki yake na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018 bali kuanzia 1963 baba yake aliposaidia Mzee Kenyatta kuachiliwa huru na wakoloni, kupigania demokrasia wanayofurahia na kumwezesha Mwai Kibaki kushinda urais 2002.

You can share this post!

CHOCHEO: Usiwe mwepesi wa kumeza chambo

Omanyala atinga nusu-fainali ya mbio za mita 100 Olimpiki