Michezo

Mbio za Gusii Sports Legends Series zaahirishwa

June 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MAKALA ya tatu ya mbio za Gusii Sports Legends Series yaliyokuwa yaandaliwe katika Kaunti ya Nyamira mnamo Juni 6, 2020, sasa yameahirishwa kwa muda usiojulikana.

Alfred Momanyi ambaye ni mkurugenzi wa mashindano hayo, amesema duru ya Kebabe Cross Country iliyokuwa inogeshe makala ya mwaka huu, itafanyika pindi baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo humu nchini.

Makala ya kwanza ya riadha hizo za Gusii Sports Legends yaliandaliwa katika eneo la Getacho chini ya udhamini wa Mbunge wa eneo la Nyaribari Masaba, Ezekiel Machogu. Kivumbi cha pili kilichofanyika 2019 kilinogeshwa katika eneo la Kebirichi, Nyamira kwa udhamini wa watimkaji wa zamani wazawa wa Kaunti za Kisii na Nyamira.

Duru nyinginezo katika mashindano ya Gusii Sports Legends ni mbio za Manga Cross Country zilizoanzishwa na marehemu Robert Ouko aliyewahi kushinda nishani ya dhahabu katika Olimpiki za 1972, na riadha za Nyanturago zilizoasisiwa na mwanaolimpiki Dan Omwanza.

“Tunasikitika kuahirisha makala ya Gusii Sports Legends hadi tarehe mpya itakayotolewa baada ya janga la corona kudhibitiwa,” akasema Momanyi.

Momanyi ni mwasisi wa Mwanyagetinge, mojawapo ya klabu za kwanza kabisa za riadha katika eneo la Gusii. Kinara huyo wa zamani wa Chama cha Riadha cha Nyanza Kusini (AK South Nyanza), kwa sasa amepania kukuza vipaji miongoni mwa chipukizi wengi katika eneo la Nyanza Kusini huku akishirikiana na wanariadha wa zamani kutoka Kisii na Nyamira.

Bingwa wa zamani wa marathon, Gladys Asiba ni Mwenyekiti wa kundi la Gusii Sports Legends. Sammy Nyangicha ambaye pia ni bingwa wa zamani wa marathon ndiye Naibu Mwenyekiti huku Edwin Nyakeriga wa KDF akiwa Katibu.

Maafisa wengine wa kundi hilo ni Isabella Ochichi (Naibu Katibu), Jackline Maranga (Mhazini) na Naftali Mayoyo ambaye ni anasimamia kitengo cha mahusiano mema.

Ochichi alitia kibindoni nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za 2004 zilizoandaliwa jijini Athens, Ugiriki. Alisajili muda wa dakika 14:48.19, sekunde 2.5 pekee nyuma ya Meseret Defar wa Ethiopia aliyejizolea dhahabu.