Michezo

MBOGA YA MAN CITY: Manchester City kuanza kutetea ubingwa League Cup dhidi ya Preston

August 30th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MANCHESTER City itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wake wa soka ya League Cup dhidi ya klabu ya Preston kutoka Ligi ya Daraja ya Pili katika raundi ya tatu Septemba 2019.

Katika droo ya raundi hiyo iliyofanywa Jumatano, Liverpool italimana na MK Dons. Preston itakuwa timu ya kwanza kujaribu kuzuia City kushinda mataji matatu katika msimu mmoja.

City walio mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na League Cup, wataalikwa na Preston uwanjani Deepdale. Vijana wa Pep Guardiola walishinda 3-1 walipozuru Preston mara ya mwisho mnamo 2007 katika FA Cup.

Preston ya kocha Alex Neil ilijikatia tiketi ya raundi ya tatu baada ya kunyamazisha wanafainali wa mwaka 2013, Bradford 4-0 mnamo Jumanne.

Mabingwa wa Bara Ulaya, Liverpool, walibanduliwa nje na Chelsea katika raundi ya tatu ya League Cup msimu uliopita, lakini wanatarajiwa kuwaona kama ‘mswaki’ MK Dons wanaoshiriki Ligi ya Daraja ya Tatu.

Vijana hao wa Jurgen Klopp wanashikilia rekodi ya mataji mengi ya League Cup (manane).

Mahasimu wa tangu jadi Portsmouth na Southampton watafufua uadui wao uwanjani Fratton Park. Portsmouth inashiriki ligi ya daraja ya tatu. Ilifuzu kupepetana na washiriki hao wa Ligi Kuu baada ya kuchapa QPR ya Ligi ya Daraja ya Pili 2-0 mnamo Jumatano.

Chelsea, ambayo ilipigwa na City kwa njia ya penalti 4-3 katika fainali ya League Cup msimu uliopita, itaalika Grimsby ama Macclesfield, ambao mechi yao ilikatizwa na mvua kubwa Jumanne.

Arsenal itakaribisha Nottingham Forest uwanjani Emirates nayo Spurs itazuru Colchester.

Manchester United itatembelewa na majirani wao Rochdale uwanjani Old Trafford.

Mechi za raundi ya tatu zitasakatwa kuanzia Septemba 23.

Wakati huo huo, bao la kwanza la Alex Iwobi lilisaidia Everton kunyamazisha Lincoln kutoka ligi ya daraja ya tatu 4-2 katika raundi ya pili ya League Cup mnamo Jumatano.

Washiriki hawa wa Ligi Kuu waliponea kufungishwa virago katika mchuano huo.

Burnley, pia kutoka Ligi Kuu, haikuwa na bahati baada ya kuchapwa 3-1 na Sunderland.

Anderson acheka na nyavu

Everton, ambayo imefunga bao moja pekee katika mechi tatu za Ligi Kuu msimu huu na ilipoteza 2-0 dhidi ya Aston Villa juma lililopita, ilijipata bao moja nyuma dakika ya kwanza Harry Anderson alipocheka na nyavu.

Lucas Digne alisawazisha dakika ya 36 naye Gylfi Sigurdsson akaimarisha uongozi huo 2-1 kupitia penalti dakika ya 59.

Bruno Andrade alifungia Lincoln bao la pili dakika ya 70 kabla ya mchezaji wa zamani wa Arsenal, Iwobi kufuma wavuni kichwa kisafi dakika ya 81 na kisha Richarlison akahakikishia Everton ushindi dakika ya 88.

Sajili wengine wapya wa Everton, Moise Kean, Djibril Sidibe, Iwobi na Fabian Delph pia walishiriki mchuano huu.

Naye Kasper Schmeichel alipangua penalti mbili klabu yake ya Leicester ikiondoa Newcastle mashindanoni baada ya muda wa kawaida kutamatika 1-1 uwanjani St James Park.

Bournemouth iliponea tundu la sindano kuaga mashindano haya mapema ilipozidia ujanja Forest Green kutoka ligi ya daraja ya nne katika upigaji wa penalti.