Michezo

MBOGA YAJA: Liverpool yazuru Carrow Road kukabiliana na Norwich

February 15th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NORWICH, Uingereza

MASAIBU ya Norwich inayovuta mkia kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) yanatarajiwa kuongezeka itakapoalika viongozi Liverpool uwanjani Carrow Road baada ya likizo fupi ya katikati ya msimu.

Norwich inashindwa kwa alama 55 nyuma ya vijana wa Jurgen Klopp wanaotarajiwa kuendeleza ukatili wao wanapodhamiria kumaliza ukame wa miaka 30 bila taji la EPL.

Timu ya Norwich ilikuwa ya kwanza kuonja makali ya Liverpool msimu huu ilipolemewa 4-1 uwanjani Anfield mwezi Agosti mwaka jana.

Tangu wakati huo, Norwich imehangaika sana kiasi cha kukodolewa macho na shoka, masaibu ambayo yatairejesha katika Ligi ya Daraja ya Pili kutokana na msururu wa matokeo mabaya.

Kwa upande wa Liverpool, mambo yamekuwa mazuri tangu ushindi huo na itaingia uwanjani ikilenga ushindi wake wa 25 katika mechi 26. Vijana wa Klopp, ambao wamekuwa wakivunja rekodi kila siku ya mechi, hawajapoteza mechi yoyote ligini msimu huu.

Matokeo yao mabaya yalikuwa 1-1 dhidi ya mahasimu wao wa tangu jadi, Manchester United mwezi Oktoba mwaka jana.

Norwich itahitaji miujiza sio tu ya kupiga breki Liverpool, bali pia kusalia kwenye Ligi Kuu. Ilitarajiwa kufanya vyema kuliko ilivyo sasa baada ya kurejea EPL msimu huu. Ilibabaisha Liverpool katika mechi ya mkondo wa kwanza licha ya kuwa iliishia kupokea kichapo hicho kikali. Hata hivyo, hakuna aliyetarajia kuwa Liverpool itatawala msimu huu jinsi inavyofanya.

Mechi 24 baadaye, mabingwa mara 18 Liverpool wako alama 22 mbele ya mabingwa watetezi Manchester City. Mchuano huu unaipa Liverpool nafasi kubwa ya kuongeza mwanya huo hadi mechi 25. Mechi kati ya City na West Ham iliyoratibiwa kusakatwa wikendi iliyopita, iliahirishwa kutokana na kimbunga cha Ciara.

Hakuna timu katika historia ya ligi tano kubwa barani Ulaya (Uingereza, Uhispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa) iliyoweza kufikia rekodi hiyo ya Liverpool msimu huu. Liverpool haijapoteza mechi ligini kwa karibu mwaka mzima sasa. Mara ya mwisho ilipochapwa ligini ilikuwa 2-1 dhidi ya Manchester City ya Pep Guardiola, Januari 2019.

Liverpool imevunja rekodi kadhaa na inatarajiwa kuvunja rekodi zaidi katika kampeni hii yake ambayo huenda haitawahi kushuhudiwa tena. Klopp amekuwa akisisitiza kuwa vijana wake wanaangazia mechi baada ya nyingine na kuchukulia kila mchuano kwa uzingativu mkuu.

Makali ya vijana wake, hata hivyo, huenda yakapimwa katika kipindi cha wiki moja ambapo pia watalimana na Atletico Madrid katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Likizo hiyo fupi ya majira ya baridi haitarajiwi kupunguza makali ya Liverpool ambayo ilienda mapumziko hayo baada ya kuaibisha Southampton kwa mabao 4-0 kupitia mabao ya Mohamed Salah (2) na Alex Oxlade-Chamberlain na Jordan Henderson.

Liverpool itatumia vifaa hivyo pamoja na Roberto Firmino na Sadio Mane. Itafikisha mechi 43 bila kupoteza ikiepuka kuduwazwa na Norwich. Mane anatarajiwa kurejea ulingoni baada ya kupona jeraha.

Arsenal inashikilia rekodi ya mechi nyingi za ligi bila kupoteza baada ya kufikisha 49, matokeo yaliyoisaidia kutwaa taji la msimu 2003-2004 na kubandikwa jina Invincibles (wasioshindwa).

Licha ya kuwa tangu Desemba mwaka jana Norwich ya Daniel Farke imeokota alama dhidi ya Arsenal, Leicester na Tottenham, italazimika kufanya kazi ya ziada kupata kitu kutoka kwa mechi zake saba zijazo.

Baada ya Liverpool, Norwich itamenyana na Wolves, Leicester na Sheffield United na pia itakutana na Chelsea na Manchester City baadaye. Teemu Pukki, Emiliano Buendia na Ben Godfrey ni baadhi ya wachezaji ambao Norwich itatumai wataisaidia kukwepa masaibu leo.