Habari

Mbona amri za Uhuru zapuuzwa?

September 10th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

AMRI za Rais Uhuru Kenyatta zinazopuuzwa mara kwa mara zimeibua maswali kuhusu sababu ya watumishi wa umma kutozitilia maanani.

Tangu alipoingia mamlakani 2013, Rais Kenyatta ametoa amri nyingi kwa matamshi au kupitia kwa barua rasmi ingawa nyingi zinaendelea kupuuzwa hadi sasa.

Mchanganuzi wa siasa, Bw Morris Odhiambo anasema katika kipindi cha mwisho cha utawala, marais hupuuzwa kwa vile wanasiasa wanaamini hawana mamlaka tena kuamua hatima ya watakaogombea nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi ujao.

“Kuanzia kwa naibu wake, mawaziri, wabunge na wengineo, wote wanamezea mate nyadhifa za uongozi 2022. Wanaona hatakuwa muhimu kwao ifikapo 2022,” akaeleza Bw Odhiambo.

Kulingana na Bw Odhiambo, ukaidi huu dhidi ya Rais ni sawa na jinsi serikali yake imekuwa ikikiuka amri nyingi zinazotolewa na mahakama.

“Tatizo kubwa lililopo ni kuwa serikali yake imedharau sheria tangu alipoingia mamlakani kwa kiwango cha kuwa sasa anapotoa amri, hakuna anayemchukulia kwa uzito. Matendo yake ya awali ndiyo yanamwandama sasa,” akasema.

Inahofiwa kuwa, mtindo huu unaweza kuigwa na umma ambao hatimaye watapuuza sheria na amri zinazotolewa kwao, hali itakayosababisha ukosefu wa utulivu wa nchi.

Amri ambayo imepuuzwa zaidi ni kuhusu hitaji la viongozi kukomesha siasa, huku tayari taharuki ikianza kuenea kuhusu uwezekano wa ghasia kwa sababu ya matamshi ya chuki yanayoenezwa na baadhi ya wanasiasa.

Katika chama anachoongoza cha Jubilee, viongozi wote wakiwemo wanaoegemea upande wake na wale wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakizuru maeneo mbalimbali kushambuliana kwa maneno wakijitafutia ubabe.

Mtindo huu haujaacha nyuma mawaziri ambao kikatiba wanastahili kujiepusha na siasa.

Mwaka huu, Rais alisisitiza amri yake ya kusitisha siasa hasa mikutano ya umma kwa sababu ya janga la corona.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa na wataalamu wa masuala ya uongozi, maagizo ya kiongozi wa taifa yanapopuuzwa kuna hatari ya nchi kukosa mwelekeo wa uongozi bora.

Kando na kampeni za mapema, amri nyingine ya Rais ambayo inaendelea kupuuzwa mwaka huu ni kuhusu ushirikiano kati ya Gavana wa Nairobi Mike Sonko na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Huduma za Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi.

Licha ya viongozi hao wawili kuonekana hadharani majuzi na kutangaza wamejitolea kushirikiana, imebainika kungali kuna mivutano kati yao kuhusu usimamizi wa jiji kuu.

Ni mivutano hii ambayo imefanya wafanyakazi wa kaunti kutishia kufanya mgomo, kwani imeathiri mfumo wa kulipa mishahara ambayo sasa inachelewa.

Amri nyingine ambayo ilibainika kupuuzwa hivi majuzi ni kuhusu usimamizi wa zabuni za idara za serikali, ambazo Rais aliagiza zianikwe mtandaoni ili kuzuia ufisadi.

Baada ya sakata ya ufisadi kufichuliwa katika Mamlaka ya Usambazaji Dawa nchini (Kemsa), Rais aliagiza shirika hilo kuchapisha zabuni zake mtandaoni ili wananchi wajionee ufisadi inapotendeka.

Hii haikuwa mara yake ya kwanza kutoa agizo aina hii kutolewa na Rais Kenyatta.

Katika mwaka wa 2018, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua aliagiza wasimamizi wa fedha wa wizara, idara na mashirika yote ya serikali kuchapisha mitandaoni habari zote kuhusu zabuni wanazotoa.

Katika mwaka wa 2019, ilifichuka kulikuwa na mashirika 56 ambayo yalipuuza sharti hilo licha ya kutoa zabuni za mabilioni ya pesa.

Wiki mbili zilizopita wakati Rais Kenyatta alipoagiza Kemsa kuchapisha zabuni zake, ilionekana wazi amri hiyo ilikuwa haifuatwi.

Kando na haya, katika mwaka uliopita, Rais aliwaagiza watumishi wa umma wawe wakivaa mavazi ya ‘Kikenya’ kila Ijumaa.

Hata hivyo, uchunguzi wa kina umebainisha watumishi wengi wa umma wakiwemo mawaziri hupuuza agizo hili na kuendelea kuvaa masuti.