Makala

Mbona magari ya miraa yasiwekwe majokofu kupunguza ajali?

January 30th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA watu wengi katika barabara kuu ya kutoka Meru kuelekea Nairobi, magari ya kubebea miraa si taswira geni kwao.

Huwa yanaitwa ‘Ndege za Barabarani’ kutokana na mwendo wa kasi ambao huwa yanaendeshwa kwayo na madereva wake.

Ingawa wengi huyafananisha na magari hayo na yale yanayoshiriki kwenye mashindano ya Safari Rally, mwendo huo wa kasi mara kwa mara umekuwa ukigeuka kuwa mauti  kwa madereva na watumizi wa barabara yanayozitumia.

Kwanza, madereva hao husema kuwa sababu ya kusafirisha magari hayo kwa mwendo wa kasi ni kuhakikisha kuwa miraa inayopakiwa haiharibiki kwa kukaa sana.

Watu wawili watazama mabaki ya gari aina ya probox katika kituo cha polisi cha Makuyu. Gari hilo liligongana na gari lingine katika eneo la Mung’etho na kusababisha vifo vya watu watatu papo hapo huku wawili wakijeruhiwa mnamo Julai 6, 2016. PICHA | MAKTABA

Wanasema kuwa watumiaji wake—wengi wakiwa kutoka jamii za Wasomali, Waborana na jamii nyingine za kaskazini mashariki mwa nchi—huwa wanapenda zao hilo likiwa halijakaa sana baada ya kuvunwa kutoka shambani.

“Watumiaji wake hupenda kutumia zao hilo likiwa bado na unyevunyevu wake, kwani hilo ndilo hulifanya kuwa tamu na la kuvutia miongoni mwa watumiaji hao,” akasema Bw Maurice Mutwiri, ambaye amekuwa dereva wa magari hayo kwa muda mrefu.

Anasema kuwa hilo ndilo huwafanya madereva wa magari hayo kuyaendesha kwa kasi, kwani huwa kuna hatari watumiaji wake kutolinunua, ikiwa litakuwa limekaa sana baada ya kuvunwa.

“Si mara moja tumelazimika kutupa mzigo mkubwa wa zao hilo tuliousafirisha kutoka Meru hadi Nairobi kwa kutowavutia watumiaji. Hivyo, huwa tunahakikisha kuwa umefika jijini angaa saa 24 baada ya kuchunwa,” akasema.

Hata hivyo, kasi ambayo magari hayo yamekuwa yakiendeshwa imetajwa kuchangia ajali nyingi, ambazo baadaye husababisha vifo vya madereva wake na watumiaji wa barabara.

Kwa mfano, mnamo Jumamosi, watu wawili walinusurika kifo katika kituo cha kibiashara cha Nyangati, Kaunti ya Kirinyaga, kwenye barabara ya Mwea-Embu, baada ya gari la kusafirisha miraa kupoteza mwendo na kugonga gari ndogo aina ya Saloon.

Kulingana na Bi Agnes Wangechi, ambaye ni mkazi wa eneo hilo, ajali hiyo ni moja tu ya nyingi ambazo zimekuwa zikitokea, hasa kwenye barabara ya Embu-Mwea.

“Ni bahati nzuri hakukuwa na maafa yotote kwenye ajali hii. Sikitiko ni kuwa, huwa hakukosi maafa ama majeraha mabaya kwenye kila ajali inayosababishwa na magari ya kusafirisha miraa,” akasema.

Kulingana na wakazi waliozungumza na Taifa Leo, imefikia wakati serikali iweke mikakati kuhakikisha imelainisha usafirishaji wa zao hilo.

Kwa mujibu wa Dkt Mbugua Njenga, ambaye ni mtaalamu wa mazao, kuna haja serikali kusisitiza magari hayo kuwekwa majokofu ili kuhakikisha kuwa si lazima yaendeshwe kwa mwendo wa kasi ili kulifikisha zao hilo kwa watumiaji wake.

“Kisayansi, zao la miraa haliwezi kupoteza utamu au ladha iliyo kwenye majimaji yake, ikiwa linaweza kuhifadhia kwenye majokofu. Hiyo ndiyo njia pekee serikali inaweza kuchukua ili kuhakikisha usafirishaji wa zao hilo umelainishwa. Hilo pia litapunguza ajali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila mara zinazoyahusisha magari hayo,” akasema.