Habari

Mbona sikuelewi Rais?

August 29th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto, anataka maelezo kuhusu mpango wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kurekebisha katiba kwa namna ambayo itamtuza mgombeaji urais anayeshindwa uchaguzini.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta alirejelea msimamo wake kwamba, mojawapo ya sababu zinazofanya Kenya irekebishe katiba yake ni ghasia ambazo hushuhudiwa kila baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Waandalizi wa katiba hii walituambia haikuwa kamilifu. Kwa hivyo tuliipitisha kwa ahadi kuwa, katika siku za usoni, tungeirekebisha. Miaka kumi baadaye, wakati huo ni sasa. Badala ya katiba ambayo inatoa nafasi ya ushindani ambapo mshindi hutwaa kila kitu, huu ni wakati mwafaka kuunda katiba ambayo itahakikishia Wakenya usalama na amani ya kudumu, na ustawi wa kiuchumi,” alisema Rais alipohutubia taifa.

Mchakato mzima wa kurekebisha katiba unaendeshwa kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) ulioanzishwa kufuatia handisheki kati ya Rais na Bw Odinga mnamo 2018.

Lakini kwenye mahojiano na Citizen TV Alhamisi usiku, Dkt Ruto alionekana kutoelewa kile ambacho Rais alimaanisha wala kulenga.

Vile vile, alidai maoni yanayotolewa na wanachama wa Jubilee wanaounga mkono urekebishaji katiba ni yao ya kibinafsi kwa kuwa chama hicho kinachoongozwa na Rais Kenyatta hakijapitisha makubaliano kama hayo.

Alisema kuwa, kufikia sasa, hajashawishiwa kuhusu hitaji la kurekebisha katiba, hasa kwa vile hajui yaliyomo kwenye mapendekezo ambayo bado yanasubiriwa kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga.

“Hili suala la kurekebisha hali ambapo ‘mshindi hutwaa kila kitu’ lamaanisha nini? Katika mashindano, lazima kuwe na mshindi na mshindwa. Hiyo ndiyo demokrasia,” akasema.

Dkt Ruto na wandani wake katika linalosifika kama ‘Tangatanga’ hutilia shaka mipango ya kurekebisha katiba wakidai ni njama ya kumharibia nafasi ya kushinda urais ifikapo 2022.

Ingawa ripoti ya mwisho ya BBI haijatolewa rasmi, duru zasema kuna mapendekezo ya kubuni nafasi za Waziri Mkuu na wasaidizi wake. Wadadisi wanasema, ikipitishwa huenda ikawa rahisi kwa anayeshinda urais kuungana na aliyeshindwa ili kuunda serikali ya mseto.

Imeripotiwa pia kuna mpango wa kutambuliwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani ambaye atakuwa na mamlaka na rasilimali kadhaa kutoka kwa serikali kutekeleza majukumu yake.

Dkt Ruto alionekana kuwa gizani kuhusu mipango inayofanywa na chama chake cha Jubilee.

“Hatujawahi kukutana kama chama kutoa msimamo kuhusu BBI. Mimi nina maoni yangu ya kibinafsi kuhusu urekebishaji katiba. Nahitaji kushawishiwa kuhusu sehemu ambazo zimetambuliwa kuwa zinahitaji marekebisho. Kama kuna sehemu yoyote ambayo itafanya katiba iwe bora kuliko ilivyo sasa, tutafanya utathmini ili tuone kama ni marekebisho yanayofaa kisha Wakenya waamue,” akasema.

Licha ya misimamo yake, alisisitiza kuwa totauti za kimaoni si ishara kwamba uhusiano wake na rais si mzuri.

Wakati huo huo, Dkt Ruto alidokeza kuwa hatasita kuhama Jubilee ikiwa misukosuko inayoendelea itadumu hadi 2022.

Alilalamika kuwa chama hicho kimetekwa na watu wasiokitakia mema, akaendelea kulaumu handisheki kwa kuvuruga mipango ya maendeleo ambayo serikali ililenga kutimiza.

Baadhi ya wanachama, wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, husisitiza kuwa Rais Kenyatta hatakubali kumuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais ifikapo 2022.

Hivi majuzi, Bw Murathe alidai Rais ataunga mkono azima ya Bw Odinga kuwania urais na kuongoza kwa muhula mmoja ili kuweka msingi bora wa uongozi wa taifa sawa na alivyofanya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela.

Bw Odinga hukwepa mara kwa mara kutangaza kama atawania tena urais katika uchaguzi ujao.