Michezo

Mbotela Kamaliza yakosa taji

July 9th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MAMBO yalituendea mrama. Kocha wa Mbotela Kamaliza FC, Eric ‘Bobby’ Otieno ametaja hayo baada ya kikosi hicho kulimwa mabao 2-1 na Tena United kwenye mechi Kundi A kuwania taji la Nairobi East Regional League (NERL).

Mbotela Kamaliza FC ilipigiwa upatu kutwaa ubingwa huo ilipoibandua Uprising FC kileleni mwa ngarambe hiyo huku ikiwa imebakisha patashika nne kukamilisha ratiba ya muhula huu.

Wachezaji wa Mbotela Kamaliza waliteremka dimbani huku wakiwa wamejaa matumaini ya kuvuna pointi tatu muhimu na kurukia uongozi wa kidumbwedumbe hicho huku imebakisha mchezo mmoja sawa na mahasimu wao Uprising FC. Bao la kufuta machozi la Mbotela Kamaliza lilifunikwa kimiani na mchana nyavu machachari Vincent Chagala.

Matokeo hayo yameyeyusha ndoto ya Mbotela Kamaliza kutwaa ubingwa wa taji hilo na kunasa tikiti ya kupandishwa ngazi msimu ujao.

”Kusema kweli hatuna la ziada mbali tukubali yaishe maana Uprising FC imekaa pazuri kubeba taji la msimu huu,” alisema na kuongeza kuwa kikosi hicho kuibuka mabingwa iwe kwa muujiza tu.

Kwa hesabu rahisi ili Mbotela Kamaliza FC kutawazwa mafahali wa ngarambe hiyo itahitaji kupigana kwa udi na uvumba kuhakikisha imezima Young Rovers kisha iombe Uprising FC itandikwe na Tena United maana zinatofautiana kwa alama mbili. Mechi hizo zimeratibiwa kuchezwa wikendi ijayo kwa wakati mmoja ili kuepuka upande mmoja kupendelea mwingine.

Naye Alfred Njumwa alicheka na wavu mara mbili na kubeba Young Rovers kukomoa Tena United mabao 2-0. Nayo Makadara Youth iliandikisha magoli 3-2 mbele ya Creative Hands FC wafungaji walikuwa Innocent Oute, Chrispin Abongo na Joshua Kipkemoi waliotikisa wavu mara moja kila mmoja. Kwenye jedwali, Uprising FC ya kocha, Collins Omondi ingali kifua mbele kwa alama 36, mbili mbele ya Mbotela Kamaliza.