Michezo

Mbotela Kamaliza yapigiwa chapuo kuonja ubingwa

June 24th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Mbotela Kamaliza inapigiwa chapuo kuibuka mabingwa wa mechi za Kundi A taji la Nairobi East Regional League (NERL) msimu huu.

Hata hivyo, kikosi hicho kinaolenga kujikatia tiketi ya kufuzu kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao kinakabiliwa na ushindani wa mkali mbele ya Uprising FC bila kuweka katika kaburi la sahau washiriki wenzao wa Nairobi Water.

”Bila kujipigia debe tumeketi mkao wa subira tukiwa na matamanio ya kutwaa ubingwa na kujizolea nafasi ya kupanda ngazi msimu ujao,” kocha wake mkuu, Eric ‘Bobby’ Otieno anasema na kuongeza kuwa wameratibiwa kupiga mechi nne zilizosalia ili kumaliza ratiba ya kipute hicho ambapo lazima washinde zote ili kujiweka mpangoni.

Anatetea wanasoka wake waliopelekea wafuasi wao kuondoka kiwanjani bila wakinuna baada ya kubanwa mabao 2-1 na Vision FC Juzi Jumapili iliyopita.

Anadai kuwa kwenye patashika hiyo alikosa huduma za wachana nyavu wanne muhimu baada ya kuapata majeraha mazoezini.

”Ingawa tulijipata kwenye wakati mgumu na kuyeyusha pointi tatu muhimu nashukuru vijana wangu kwa kuonyesha ubabe wao vilivyo ambapo ninaamini tutafanikiwa kutimiza malengo yetu kupanda ngazi kushiriki kampeni za soka la ligi ya hadhi ya juu,” asema.

Kocha huyo anasema akishirikiana na kamati nzima ya kiufundi ya klabu hiyo wanahimiza wachezaji wao kujiepusha kabisa na presha kipindi hicho wanashiriki mechi zilizosalia.

Anasisitiza kuwa hawana la ziada mbali mechi zote zilizosalia wamenuia kucheza kila moja kama fainali pia kwa kujiamini wanaweza.

Kwenye msimamo wa kipute hicho, Mbotela Kamaliza imekamata usukani kwa kukusanya pointi 30, sawa na mahasimu wao Uprising FC tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Uprising FC ambayo hunolewa na kocha, Collins Omondi imecheza mechi 17, moja zaidi ya Mbotela Kamaliza.

Mbotela Kamaliza imeratibiwa kushiriki mechi nne dhidi ya Dream Team, Nairobi Water, Young Rovers na Tena United.

Nao wanasoka wa Uprising FC wamebakisha patashika tatu ambapo wameratibiwa kuvaana na FC Barca ya saba kwenye jedwali, Makadara Youth ya nane na Tena United inayo kati ya mduara wa nafasi mbili za mwisho na ikiteleza tu itashushwa ngazi bila huruma.

Katika mpango mzima naibu kocha wa Mbotela Kamaliza, Kelly Ametesha anasema “Tuna imani ya kujikatia tiketi ya kusonga mbele ila hatuwezi kuwapuuza wapinzani wetu soka halina heshima chochote kinaweza kutokea kama mambo yalivyogeuka kwenye mechi yetu na Vision FC.” Pia anadai kuwa kamwe hawakuwazia kama wangepoteza mchezo huo.

Ofisa mwenzake katika benchi ya ufundi, Washington Bululu anasema ”Msimu huu vijana wetu wetu wamejaa motisha tayari kutesa wapinzani wao hali ambayo imewabeba na kujikuta kileleni mwa kinyang’anyiro cha msimu huu kinyume na matarajio ya wengi.”

Anaelezea kuwa tangia mwanzo wa mechi hizo hakuna aliyewazia kwamba Mbotela Kamaliza ingebahatika kuongoza kundi la timu 11.

Anataka wachezaji hao kuwa makini na kutolegeza msimamo wa azimio lao kunasa tiketi ya kusonga mbele baada ya kuitafuta kwa zaidi ya miaka kumi.

”Kulingana na msimamo wa mechi za kipute hicho tayari tunatetemesha wengi ambao hawakutarajia tungeibua ujio mpya kwenye kampeni za muhula huu,” asema.

Mbotela Kamaliza ilianzishwa miaka 37 iliyopita ambapo muhula huu inajumuisha wachezaji kama: Brandon Oduor, Emmanuel Atulo, Benson Kitur, Victor Odera, Vincent Chagala, Brian Ode, Vitalis Opiyo, Patrick Kadenge, Stephen Babu, Tom Odongo, Kenneth Okubasu, Patrick Opimbi na Hannington Young. Pia wapo Christopher Gitau, Martin Linyonyi, Elvis Barasa, Roy Obuya, Felix Omondi, Mike Tyson, Eugene Oloo, Paul Amala, Lyone Omondi, Christopher Kamau, David Ochieng, Riddick Omondi, Churchil Olavi na Edger Ochieng.

Klabu hii inajivunia kutwaa mataji mbali mbali miaka ya awali ikiwemo Kombe la Mutai Kagwe (1999), Extreme Super Eight (2004), pia mataji ya Athi River na Ramogi miaka ya 2011 na 2006.