Habari MsetoSiasa

Mbunge afokea wanaopinga mradi wa nishati ya makaa Lamu

July 30th, 2018 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

MBUNGE wa Lamu Mashariki, Athman Sharif, amewataka wakazi wa Lamu wanaopinga kuanzishwa kwa mradi wa nishati ya makaa ya mawe eneo hilo kukoma kulalamika.

Akizungumza kwenye ukumbi wa Huduma Centre mjini Lamu wakati wa kikao kilichowakutanisha wakazi na kamati ya bunge la kitaifa kuhusu mazingira na maliasili mwishoni mwa juma, Bw Sharif aliwakashifu wale wanaoendeleza shinikizo za kupinga kuanzishwa kwa mradi huo Lamu kwa kukosa kutafakari iwapo mwekezaji wa mradi huo amefuata sheria kikamilifu hadi kufikia hatua iliyopo.

Mradi wa nishati ya makaa ya mawe ambao unakadiriwa kugharimu kima cha Sh 200 bilioni uko chini ya udhamini wa kampuni ya Amu Power.

Mradi huo unatarajiwa kujengwa eneo la Kwasasi, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.

Kufikia sasa jumla ya ekari 975 za ardhi tayari zimetengwa eneo la Kwasasi ili kufanikisha ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 1,050 za umeme punde utakapokamilika.

Bw Sharif alisema hairidhishi kwamba kila mara kumekuwa na utata na pingamizi tele miongoni mwa wakazi na mashirika ya kijamii kila mara kunapokuwa na mijadala kuhusu mradi wa nishati ya makaa ya mawe.

Alisisitizia wakazi kutambua kwamba bunge la awali la kaunti ya Lamu tayari lilipitisha mradi huo, hivyo akawataka viongozi na wakazi kuja pamoja ili kuafikiana ni jinsi gani dukuduku zilizopo kuhusu mradi huo zitatatuliwa.

“Tusikimbilia tu kupinga au kuunga mkono mradi wa nishati ya makaa ya mawe. Cha msingi ni kuangalia je, mwekezaji amefuata sheria kikamilifu au la? Kwa wale wanaokimbilia kupinga, ningewataka wafahamu kwamba bunge lenu la awali la kaunti ya Lamu tayari limepitisha mradi huo.

Lazima pia itambulike kwamba hata tukapinga au kuunga mkono mradi, ni asilimia kidogo sana iliyobakia kubadilisha lolote kuhusiana na kuanzishwa kwa mradi huo hapa Lamu.

Cha msingi ni sisi viongozi na wakazi kuja pamoja na kujadiliana ni jinsi gani dukuduku zilizopo zitatatuliwa kabla ya mradi uanze,” akasema Bw Sharif.