Habari Mseto

Mbunge ahimiza wakazi kujitokeza wahesabiwe

August 25th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Juja na vitongoji vyake walifuata mwito wa serikali kwa kufunga baa zote ili kwenda kuhesabiwa.

Mbunge wa Juja Bw Francis ‘Wakape’ Waititu, na familia yake walifuata mwito huo kwa kuhesabiwa nyumbani kwake mwendo wa saa moja za usiku.

Maafisa wa kuhesabu watu na wale wa usalama walijipanga mapema na ilipofika saa kumi na moja jioni walionekana wakisafirishwa maeneo tofauti wakijianda kwa zoezi hilo.

Mbunge huyo aliwahimiza wakazi wa Juja washirikiane vilivyo na maafisa hao ili kufanikisha zoezi hilo.

“Ninawahimiza wakazi wa Juja kujitokeza na kujibu maswali yote watakazoulizwa bila kubishana na maafisa wa kuhesabu watu. Eneo ubunge langu la Juja nakadiria zaidi ya watu 200,000 kwa sababu mji huo umekua kwa kiwango kikubwa chini ya miaka kumi pekee,” alisema Bw Waititu.

Lakini alikiri miji ya Thika na Ruiru ina wakazi wengi kulingana na hali ya biashara katika maeneo hayo.

Alisema baada ya zoezi hilo serikali itakuwa na nafasi nzuri ya kupanga mikakati yake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu kwenye maeneo yao.

Mbunge wa Juja Francis Waititu (kushoto) alipohesabiwa pamoja na mkewe Susan Waititu (kulia) na mwanawe Martin Munyua (pili kushoto) Agosti 24, 2019 nyumbani kwake. Picha/ Lawrence Ongaro

Mwito wa serikali kutoa amri maskani za pombe kufungwa wakati wa zoezi hilo ilifuatwa kikamiifu kwani baa nyingi zilibaki mahame huku zikifungwa na watu kurejea makwao.

Naibu kamishna wa Kaunti Ndogo ya Juja Bw Charles Mureithi, aliyeandamana na maafisa wa usalama kwa boma la Bw Waititu alisema tayari wameweka mikakakti yote ya usalama.

Tunatarajia hakuna chochote kibaya kitatokea kwani hali ya usalama umeimarishwa vilivyo,” alisema Bw Mureithi.

Alitoa wito kwa wananchi popote walipo kushirikiana vyema na maafisa hao wa usalama na makarani wote wa kuhesabu watu.

“Hakuna haja ya kuzua fujo kwani maafisa hao wote wamepewa mafunzo jinsi ya kushirikiana pamoja na wananchi,” alisema Bw Mureithi.

Alisema Polisi wamesambazwa kila sehemu ambapo hali ya usalama katika mitaa itakuwa shwari.

“Hatungetaka kusikia kuwa kuna shida yoyote ama mvutano lakini lengo letu kuu ni kutumikia wananchi ipasavyo. Kwa hivyo kila mmoja ashirikiane vyema,” afisa huyo wa serikali alifafanua.